WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda amepokea msaada wa vitabu 895 vyenye thamani ya sh.
milioni 6.5/- ikiwa ni jitihada ya wadau mbalimbali kuchangia shule ya
msingi aliyosoma ya Kakuni iliyoko kijiji cha Kibaoni, wilayani Mlele,
mkoani Katavi.
Waziri Mkuu amepokea msaada huo
jana mchana (Jumanne, Mei 26, 2015) kwenye shule mpya ya msingi Kakuni
ambayo bado inaendelea kujengwa kwenye kijiji cha Kibaoni.
Akizungumza katika hafla hiyo
fupi mara baada ya kupokea msaada huo, Waziri Mkuu Pinda aliishukuru
kampuni ya General Booksellers Ltd ya kutoka Dar es Salaam kwa msaada
huo ambao alisema utachangia kwa kiasi kikubwa kuitimiza ndoto yake
aliyokuwa nayo ya kuisaidia jamii iliyomsomesha.
“Wazo la ujenzi wa shule mpya ya
msingi Kibaoni lilitokana na ukweli kwamba nilisoma na kumaliza kwenye
shule hii ya Kakuni. Nikiwa ni mtumishi wa Serikali, ni Mbunge na sasa
hivi ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nilijiuliza hivi
shule hii ninaweza kuiacha hivi hivi?”
“Nilijiuliza sana ni jambo gani
ambalo naweza kulifanya la kusaidia wanakijiji wenzangu na kata nzima ya
Kibaoni kama shukrani kwa kunilea na kunifikisha hapa nilipo. Ndipo
wazo la kujenga shule niliyosoma likazaliwa kama mwaka mmoja na nusu
uliopita,” alisema Waziri Mkuu wakati akiwahutubia wazazi, walimu na
wanafunzi.
Mapema, akiwasilisha msaada huo,
mwakilishi wa kampuni ya General Booksellers Ltd, Bw. Joachim Masaburi
alisema wameamua kuchangia vitabu hivyo kwa kutambua umuhimu wa elimu
kwa watoto lakini pia wanatambua juhudi za Serikali za kutoa elimu bora.
Akitoa mchanganuo wa vitabu
hivyo, Bw. Masaburi alisema: “Kuna vitabu 600 kwa ajili ya shule ya
awali ambavyo kati yake 300 ni vya ngazi ya chini (nursery) na vitabu
vingine 300 ni vya ngazi ya juu (pre-school). Vyote ni vya hisabati,
Kiingereza na sayansi”.
“Kwa shule ya msingi wao
tunawapatia kivunge cha kufundishia mfumo wa mwili wa binadamu kama
sehemu ya masomo ya sayansi, hiki kina thamani ya sh. 550,000/-,”
alisema.
Pia kampuni hiyo ilitoa msaada wa
vitabu vingine 295 vya Baiolojia, Fizikia, Uraia, Kiswahili kwa ajili
ya shule ya sekondari ya Mizengo Pinda iliyoko kijijini hapo.
Hadi sasa majengo yaliyokamilika
kwenye shule hiyo ni madarasa 14, jengo la utawala lenye ofisi za walimu
na maktaba mbili (wanafunzi na walimu), jengo la TEHAMA la wanafunzi
lenye darasa moja, ukumbi mdogo na ofisi za walimu na jengo moja la choo
lenye matundu 48. Pia ujenzi wa nyumba sita za walimu uko kwenye hatua
ya kuezeka. Nyumba hizo zinajengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).
Ujenzi wa choo kingine chenye matundu 48 umeanza.
Waziri Mkuu aliwaomba wananchi
wengine wamsaidie kutimiza ndoto yake kwani bado anakabiliwa na kazi ya
kuweka umeme, maji, kujenga nyumba nane za walimu, bwalo na jiko,
karakana nne za ufundi, ujenzi wa kituo cha walimu cha mafunzo ya muda
mfupi na utunzaji taarifa (Resource Centre), viwanja vya michezo vya
kisasa vinavyozingatia michezo yote, mfumo wa uvunaji maji ya mvua,
mfumo wa maji safi na maji taka, nyumba mbili za walinzi na uzio wa
shule.
Alitaja vitu vingine ambavyo bado
vinahitaji kuchangiwa ni meza za walimu – za ofisini na darasani, viti
vya walimu – vya ofisini na darasani, madawati ya shule ya msingi na ya
awali, meza na viti vya maktaba zote mbili, meza na viti vya bwalo –
shule ya msingi na shule ya awali.
Comments