AMRI KALI YA MKAPA ILIVYOZIMA VURUGU NEC CCM





Rais Mstaafu, Benjamini Mkapa
Rais Mstaafu, Benjamini Mkapa 
By Mwandishi Wetu, Mwananchi
Dar es Salaam. Kauli ya Rais wa Awamu ya tatu, Benjamin Mkapa ya kutaka wajumbe wa Halmashauri Kuu kupiga kura na wale wasioafiki watoke, ndiyo inaelezwa kuwa ilimaliza mzozo ulioibuka baada ya jina la Edward Lowassa kuenguliwa mapema.
Kikao hicho kilichofanyika Julai 10 kilionekana kuelekea kukumbwa na mtafaruku baada ya wajumbe kumpokea Rais Jakaya Kikwete kwa wimbo wa kuonyesha kuwa wana imani na waziri huyo mkuu wa zamani ambaye jina lake halikuwamo miongoni mwa makada watano waliopitishwa na Kamati Kuu ya CCM.
Habari ambazo Mwananchi imezipata kutoka kwa wajumbe wa Halmashauri Kuu zinasema kuwa baada ya mapumziko ya chakula cha mchana, ulizuka mjadala mkubwa kuhusu kuenguliwa kwa Lowassa, ambaye alionekana kuwa alikuwa akiongoza mbio za urais ndani ya chama hicho.
Habari hizo zinasema wakati wa mjadala huo ndipo wajumbe wa Baraza la Ushauri la Viongozi walipoingilia na kuanza kutoa ushauri mmoja baada ya mwingine kabla ya Mkapa kuzungumza na baadaye kusema “twendeni tukapige kura, asiyetaka atoke”, ndipo hali ya ukimwa ilipotanda na kufuatiwa na kazi ya kupiga kura iliyoashiria kuwa amani imerejea.
Hata hivyo, haikuwa rahisi kwa kikao hicho chenye wajumbe takriba 400 kutulizwa na kufikia hatua ya kupigia kura majina matano ili kupata matatu ambayo yalipelekwa kwenye Mkutano Mkuu.
Habari ambazo Mwananchi imezipata zinaeleza kuwa wajumbe waliokuwa wakimtaka Lowassa walikuwa wakihoji sababu za mbunge huyo wa Monduli kuenguliwa huku jina la Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe likiachwa.
Alikuwa mwenyekiti wa baraza hilo, Ali Hassan Mwinyi aliyeanza kwa kuwaeleza wajumbe historia ya changamoto zilizokipata chama hicho, aliyoyaona mwaka 1995 wakati kulipokuwa na wagombea 17, lakini walioingia kwenye mchujo walikuwa 15, wakiwemo Benjamin Mkapa, Jakaya Kikwete na Cleopa Msuya.
Mwinyi aliwashauri wajumbe kuwa kama wanampenda mtu, wawe na kiasi na kama wanamchukia mtu, wawe na kiasi pia na kwamba wasifanye mambo hayo kwa kupitiliza kwani matokeo yatapokuwa tofauti na walivyotarajia wao ndiyo wataathirika zaidi kuliko muhusika.
Kwa mujibu wa mtoa taarifa mwingine aliyetoa nasaha zake alikuwa Waziri Mkuu wa zamani, John Samuel Malecela, ambaye aliimbia kwenye mbio hizo mwaka 2005 wakati walipojitokeza makada 11 kuwania kuteuliwa na CCM.
Malecela, ambaye wakati huo alikuwa na  wadhifa wa makamu mwenyekiti wa CCM Bara, Malecela aliwaeleza wajumbe hasa walikuwa na mapenzi na Lowassa kwamba hata yeye wakati huo alikuwa na kundi kubwa la watu waliokuwa wanamuunga mkono kutoka Kanda ya Ziwa.
Kwa mujibu wa mtoa taarifa, Malecela aliwaambia wajumbe wa NEC kwamba wafuasi wake walikuwa wakilia kwa uchungu kutokana na jina lake kukatwa, walimshauri mengi ikiwemo ya kuhama chama, lakini  aliwaambia “chama kwanza mtu baadaye”, kwa maana huo ndiyo ulikuwa uamuzi wa chama na unapaswa kuheshimiwa.
Wakati huo, baada ya Rais Kikwete kutangazwa kuwa ndiye ambaye angepeperusha bendera ya CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, alikwenda kumpa mkono wa hongera na kuahidi kumuunga mkono.
Mjumbe mwingine wa baraza hilo, Amani Abeid Karume, ambaye alikuwa Rais wa Zanzibar, anasemekana kuwa aliwaambia wajumbe kwamba wafanye mambo kama watu wazima, kwa kuwa kuna mambo ya mtu yanaweza kuzungumzwa hadharani, lakini kuna mengine yanahitaji staha ili kuepuka kudhalilishana.
Aliwashauri wajumbe wasipende kutaka kila kitu cha mtu wanayedhani anaonewa kiwekwe wazi kwa kuwa kuna mengine hayastahili kuwekwa hadharani, na kuwasisitizia kufikiri kama watu wazima.
habari hizo zinasema kuwa aliyebadilisha kabisa mwelekeo wa kikao alikuwa Rais Mkapa ambaye aliwaeleza wajumbe kwamba mambo yote wanayozungumza kuhusu uonevu siyo sahihi kwa sababu mwenyekiti wa chama, Rais Kikwete ana taarifa kuliko wao kwa kuwa anazo nyenzo za kumpatia taarifa na namna ya kuzithibisha ukweli wake.
 Kwa mujibu wa mtoa taarifa Mkapa baada ya kusema maneno hayo alisema: “Twendeni tukapige kura, asiyetaka atoke.”
Maneno ya wazee hao na hasa ya Mkapa yaliwanyong’oneza wajumbe hasa waliokuwa wakipinga uamuzi wa Kamati Kuu, na baada ya hapo hakuna aliyeinua kinywa chake kutaka kuzungumza kitu au kupinga jambo.
Kikao hicho kilikuwa na usiri mkubwa baada ya wajumbe kuzuiwa kuingia na simu kwenye ukumbi wa mikutano wa ofisi za makao makuu ya CCM, White House uliopo katikati ya mji wa Dodoma.
Baraza la Ushauri linaoongozwa na Rais Mwinyi (mwenyekiti), katibu wake ni Spika wa zamani wa Bunge, Pius Msekwa, wakati wajumbe ni marais wastaafu, Mkapa, Karume, Dk Salmin Amour na Makamu wa Rais wa Pili na Waziri Mkuu mstaafu, John Malecela.
Wastaafu hao walikuwepo kwenye vikao vyote, na Malecela, ambaye alikuwa London nchini Uingereza, aliwasili siku ya kikao cha Kamati Kuu, na kwa umuhimu wake alipotua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere alikuta ndege nyingine ikimsubiri uwanjani hapo kwa ajili ya kumpeleka Dodoma.
Dalili za kuzuka mtafaruku kwenye kikao cha Halmashauri Kuu zilianza mapema. Wakati Mwenyekiti akiingia na viongozi wengine, wajumbe walianza kuimba wimbo wa “tuna imnani na Lowassa”, badala ya maneno yanayotumika kwenye wimbo huo ambao hupachikwa jina la mwenyekiti wa chama.
“Haijapata kutokea,” alisema Rais Kikwete baada ya kukaa kwenye kiti na kuongeza kuwa mambo yote yatazungumzwa taratibu na muafaka utafikiwa.
Mtoa taarifa wetu anasema kuwa Rais Kikwete alikuwa mvumulivu, akitoa mwanya kwa wajumbe wengi kuzungumza licha ya baadhi kumshambulia wakidai familia yake inampigia kampeni Membe.
Habari zinasema pamoja na shutuma zote hizo, Kikwte hakujibu hoja hizo zaidi ya kutoa mwanya kwa wajumbe wengi zaidi kuchangia.
Kwa mujibu wa mtoa taarifa ilifika wakati wajumbe wakaanza kushambuliana wao kwa wao, huku wengine wakisema hawajaenda humo kujadili jina la mtu mmoja.
Source;Mwananchi Gazeti

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA