(UKAWA)
TAARIFA KWA UMMA
Utangulizi
Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), uliasisiwa
wakati wa Bunge Maalum la Katiba. Lengo likiwa kuunganisha nguvu za Wajumbe
wote wa Bunge hilo walioamini katika kuheshimu maoni ya wananchi
yaliyowasilishwa kupitia Rasimu ya Katiba iliyotayarishwa na Tume ya Mabadiliko
ya Katiba iliyoongozwa na Waziri Mkuu MstaafuJaji Joseph Sinde Warioba.
Kundi hili lilihusisha baadhi ya Wajumbe
kutoka makundi yote. Baadaye, kundi hili lilipungua na kubaki na wajumbe kutoka
vyama vya NLD, NCCR - Mageuzi, CUF na CHADEMA. Aidha, Wajumbe toka kundi la 201
walibaki wachache ambao walikataa kuyumbishwa.
Nje ya BungeMaalum, viongozi na
wanachama wa vyama vya siasa,makundi mbalimbali yakiwemo ya kijamii, kidini,
kitaaluma, kiraia na hata raia mmoja mmoja yaliendelea kushiriki katika
mijadala na wengi wao wakitaka maoni ya wananchi kama yalivyoratibiwa na Tume
ya Mabadiliko ya Katiba na kuungwa mkono na UKAWA yaheshimiwe.
Baada ya mvutano wa muda mrefu, ni wazi
sasa kuwa zoezi la kuipatia nchi yetu Katiba mpya chini ya serikali ya awamu ya
nne ya uongozi limekwama.
Katiba mpya inayotokana na maoni ya
wananchi ni nyezo yakufikia malengo mapana zaidi ya kuwa na taifa la wananchi
walioelimika na kujitambua, wenye afya bora,kujenga uchumi imara na unaoongeza
ajira kwa vijana wetu, kutokomeza umasikini, kutumia raslimali na maliasili za
nchi kwa manufaa ya wananchi wote na kuwa taifa lenye utu, uzalendo, uadilifi,
umoja, uwazi na uwajibikaji.
Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2015
Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2015 ni fursa ya
kipekee ya kuleta mabadiliko makubwa katika nchi yetu ya kuondoa mfumo kandamizi
uliojikita ndani ya CCM. Watanzania wanahitaji mabadiliko yatakayowapatia
serikali madhubuti yenye fikra mpya na bunifu kwa maslahi yao.
Watanzania wanahitaji mabadiliko
yatakayojenga demokrasia ya kweli na kuachana na uonevu, udhalilishaji, fitna
na majungu unaoendelezwa na CCM.
Taifa letu linakabiliwa na ombwe la
uongozi ambao umesababisha nchi yetu kuyumba na kuwa na mipasuko hatari ndani
ya jamii. Watanzania wanahitaji uongozi thabiti wenye dira, nidhamu na uadilifu
utakaolipelekambele taifa letu.
Uchaguzi wa Oktoba 2015, ukitumiwa
vizuri na kimkakati utaleta mabadiliko makubwa yanayotakiwa na
wananchi.Uchaguzi huu ni fursa muhimu ya kujenga mshikamano wa Taifa. Kwa
mantiki hii UKAWA unaamini katika kuweka mbele maslahi mapana ya wananchi kwa
kujenga mshikamano ndani na nje ya vyama vyetu tunapoelekea katika Uchaguzi
Mkuu na hata baada ya Uchaguzi Mkuu.
Ili tulete mabadiliko yatakayotupatia
katiba bora na kufikia malengo tajwa hapo juu ni muhimu UKAWA ushinde uchaguzi
wa 2015.
Watanzania wameshuhudia hadaa, uonevu, udhalilishaji,
upendeleo na ukandamizaji katika mchakato wa kupata Mgombea Urais kwa tiketi ya
CCM.Kulikuwa na ukiukwaji mkubwa wa taratibu, kanuni na katiba ya chama chao.
Katika kutafakari kwa kina maslahi
mapana ya Taifa letu, UKAWA tunahitaji viongozi wenye sifa, uwezo na weledi
katika kulinda, kuheshimu na kusimamia rasilimali za Taifa kwa maslahi ya Watanzania
wote.
Aidha, viongozi wa aina hii hawawezi
kuwa ndani ya CCM maana mfumo wa CCM haumpi kiongozi binafsi kutumia vipaji
vyake au ubunifu wake binafsi katika kusimamia maslahi ya taifa letu.
UKAWA tunaamini kuwa kwa maslahi mapana
ya taifa letu tunamuhitaji kila Mtanzania ambaye yuko tayari kujiunga nasi
katika kuhakikisha kuwa taifa letu linakuwa salama na lenye amani ya kweli
ambayo msingi wake ni haki.
Hivyo basi, ni rai ya UKAWA kwa kila Mtanzania
ambaye yuko tayari kuuondoa mfumo huu kandamizi na dhalimu wa CCM kushirikiana
na UKAWA kwa lengola kujenga Taifa imara.
Tunachukua fursa hii kipekee kumwalika
Waziri Mkuu Mstaafu na Mbunge wa Jimbo la Monduli,Mheshimiwa Edward Lowassa
ajiunge na UKAWA na tuko tayari kushirikiana naye katika kuhakikisha kuwa
tunaiondoa CCM madarakani katika uchaguzi mkuu ujao. Tunaamini Mheshimiwa
Lowassa ana uwezo wa kuhamasisha umma kuikataa CCM yenye kusimamia mifumo
isiyotenda haki. Ni mchapakazi makini na mfuatiliaji wa karibu wa utendaji
katika majukumu anayokabidhiwa.
Ni lengo la UKAWA kushirikiana katika Uchaguzi
Mkuu na tutaweka mgombea mmoja wa udiwani katika kila kata na wadi, mgombea
mmoja wa uwakilishi na ubunge katika kila jimbo, na mgombea mmoja wa Urais wa Zanzibar na
mgombea mmoja wa Urais wa Jamuhuri ya Muungano.
UKAWA ndilo Tumaini la Watanzania.
Tusikubali kunyamaza pale ambapo sauti zetu zinanyamazishwa kwa lazima na bila
sababu. Tusikubali kunyimwa fursa ambazo tuna uwezo nazo. Tuwe tayari kushiriki
michakato ya kidemokrasia ya kuleta mabadiliko na kupata viongozi bora.
Mungu Ibariki Tanzania.
Mungu Ibariki UKAWA.
UKAWA NDILO TUMAINI LETU.
James Francis Mbatia (Mb)
Mwenyekiti wa Taifa NCCR – Mageuzi
(kny Wenyeviti wa UKAWA Tarehe 27 Julai 2015)
Comments