Trilioni nane zatumika kuboresha umeme ndani ya miaka 10


Na Beatrice Lyimo-Maelezo
Zaidi ya Dola billioni nne za Kimarekani ikiwa sawa na Trilioni nane kwa shilingi ya Kitanzania zimewekezwa katika sekta ya umeme kwenye Miradi yote ya uzalishaji, usambazaji na usafirishaji wa umeme nchini.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la ugavi la umeme nchini (TANESCO) Mhandisi  Felchesmi Mramba wakati akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam.

Amesema kuwa katika kipindi cha miaka 10 (2005-2015), Serikali imeongeza uwezo wa mitambo ya kuzalisha umeme katika Gridi ya Taifa kutoka MW 891 hadi kufika MW 1,501.24 sawa na ongezeko la asilimia 68.5.

“Baadhi ya miradi iliyokamilika  ni pamojaj na mtambo wa kuzalisha umeme MW 100 uliopo Ubungo, na Ujenzi wa mtambo wa kufua umeme MW 45  uliopo Tegeta jijini Dar es salaam. Miradi mingine ni mtambo wa kuanzisha umeme MW 60 Mwanza, na mradi wa umeme wa Somanga Fungu MW 7.5 Mkoani Lindi” amesema Mkurugenzi huyo.

Kwa mujibu wa Mhandisi Mramba, kukamilika kwa Miradi hiyo kumewezesha upatikanaji wa umeme wa uhakika nchini na kufanikisha kuondoa mgawo wa umeme hususani kuanzia mwaka 2012 na hivyo kuboresha ufanisi wa utekelezaji wa shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii.

Mtendaji huyo Mkuu wa TANESCO ameeleza kuwa kumekuwa na mikakati mbalimbali ya kuongeza uzalishaji wa umeme kwenye Gridi ya Taifa na nje ya Gridi ya Taifa ikiwemo utekelezaji wa Mradi wa Kinyerezi 1 (MW 150) kwa kutumia Gesi asilia, mradi wa kupeleka umeme katika miji ya Mpanda, Ngara, na Biharamulo.

Aidha Mkurugenzi huyo ametoa ufafanuzi kuhusu kubadilisha mfumo umeme wa LUKU utakaofanyika tarehe 1/8/2015.

“Zoezi la kubadilisha mfumo wa LUKU litachukua muda wa saa 24 kuanzia usiku wa manane wa Agosti Mosi, 2015 hadi usiku wa manane wa tarehe 2/8/2015 sio siku saba kama ilivyoenezwa katika mitandao  ya kijamii,” amesema.

Lengo la zoezi hili ni kuongeza kasi na kuwawezesha watu wengi kuunganishwa na mfumo mpya wa LUKU utakaohudumia idadi kubwa zaidi ya watu tofauti na hali ilivyo sasa.
MWISHO

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*