Watakwimu wa nchi za Afrika wasisitizwa kuzingatia weledi na uwazi


Mwakilishi wa Benki ya Afrika (ADB) nchini Tanzania Tonia Kandiero akizungumza na washiriki wa Warsha  ya Kimataifa ya Watakwimu kutoka nchi za Afrika zinazozungumza lugha ya kiingereza juu ya ushiriki wa ADB katika masuala ya Takwimu katika Bara la Afrika leo jijini Dar es Salaam. 
Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa akiwakaribisha nchini Tanzania washiriki wa mkutano wa kimataifa wa Watakwimu kutoka nchi za Afrika zinazozungumza lugha ya kiingereza leo jijini.Washiriki wa Warsha hiyo wanajadili na kubadilishana uzoefu kuhusu Pato la Taifa. 
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Profesa Adolf  Nkenda akifungua warsha ya siku 5 ya watakwimu kutoka nchi za Afrika zinazozungumza lugha ya Kiingereza, iliyofanyika jana jijini Dar es Salaam. 
Baadhi ya washiriki wa mkutano huo wakifuatilia masuala mbalimbali wakati wa mkutano huo leo. 
Washiriki wa Warsha hiyo ya kimataifa ya Watakwimu kutoka nchi za Afrika zinazozungumza lugha ya kiingereza wakiwa katika picha ya pamoja leo jijini Dar es Salaam.

Na Veronica Kazimoto- Dar es Salaam.
13/7/2015.
SERIKALI imesema kuwa itaendelea kuongeza uwazi katika matumizi ya takwimu zinazokusanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu nchini ili kukidhi vigezo na malengo ya mfumo mpya uliowekwa na Umoja wa Mataifa wa mwaka 2008 wa upataji wa takwimu za pato la Taifa.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Warsha ya kimataifa ya siku 5 ya watakwimu kutoka nchi za Afrika zinazozungumza Kiingereza, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha Prof. Adolf Nkenda amesema kuwa Tanzania inaendelea kukusanya takwimu mbalimbali ili kukidhi mahitaji ya watunga Sera na wananchi.

Amesema kwa kutambua na kuthamini mchango wa takwimu katika maendeleo, Serikali imeamua kuingiza takwimu za ubora wa mazingira na takwimu za matumizi ya simu za mkononi kwenye Pato la Taifa.

Amefafanua kuwa, mabadiliko hayo yataiwezesha Tanzania kuwa na takwimu zenye uhalisia kuhusu shughuli mbalimbali zinazofanyika nchini na mchango wake katika Pato la Taifa.

Prof. Nkenda ametoa wito kwa washiriki wa warsha hiyo kuendelea kuzingatia weledi katika utekeleaji wa majukumu yao ili waweze kutoa takwimu sahihi zinazoonesha hali halisi ya tafiti zinazofanyika katika nchi zao.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS)   Dkt. Albina Chuwa  akizungumza na washiriki wa Mkutano huo wa Kimataifa amesema kuwa Nchi za Afrika zinahitaji Takwimu sahihi ili ziweze kuendelea.

Amesema Tanzania imepiga hatua kwa kuweka kipaumbele katika shughuli mbalimbali za Takwimu ikiwemo kusaini mkataba wa Takwimu wa Afrika kuhusu kuongeza uwazi katika upatikanaji na matumizi ya takwimu  zilizopo kwa Maendeleo ya Taifa.

Ameeleza kuwa kupitia Mfumo mpya wa Umoja wa Mataifa wa kutengeneza Pato la Taifa wa mwaka 2008, Tanzania imefanikiwa kuingiza shughuli mbalimbali katika Pato la Taifa ambazo hapo awali hazikuwemo, zikihusisha shughuli za kitaalam za Sayansi na Teknolojia pamoja na sanaa.

Ili kufanikisha shughuli za takwimu Barani Afrika Dkt. Chuwa ameziomba Serikali zote za Afrika kuutumia na kuheshimu Mkataba wa Afrika wa Takwimu wa mwaka 2008 unaotoa kipaumbele katika uboreshaji wa shughuli za Takwimu.

"Napenda kutumia fursa hii kuziomba Serikali za Afrika kuzijengea uwezo Ofisi za Takwimu ili ziwe na uwezo wa kuzalisha takwimu za masuala mbalimbali kwa muda mfupi maana Takwimu ni sasa kwa ajili ya kukidhi mahitaji na matarajio ya wananchi", amesisitiza Dkt. Chuwa.

Aidha, ameongeza kuwa warsha hiyo ya siku 5 ambayo imewajumuisha watakwimu kutoka nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na baadhi ya nchi za Afrika Magharibi zikiwemo Ghana na Nigeria inalenga kuwajengea uwezo washiriki hao kwa kuwa na uelewa wa pamoja katika kukabiliana na changamoto mbalimbali za Takwimu katika nchi zao.

Naye Mwakilishi wa Benki ya Afrika (ADB) nchini Tanzania Bi.Tonia Kandiero amewataka washiriki wa warsha hiyo kuzingatia mfumo uliowekwa wa upataji wa takwimu za Pato la Taifa ili kuwezesha uwepo wa takwimu sahihi za maendeleo ya nchi husika.

Amesema kuwa wingi wa washiriki wa warsha hiyo waliohudhuria kutoka nchi mbalimbali za Afrika ni ishara tosha kuwa nchi zao zinathamini mchango wa Takwimu katika kuleta maendeleo.

Amesema Benki ya Afrika ambayo yeye ni mwakilishi wake itaendelea kushirikiana na nchi za Afrika ili kuhakikisha kuwa Takwimu mbalimbali zikiwemo za Watu na Makazi, Pato la Taifa na nyinginezo zinapatikana kwa wakati na kuchangia maendeleo ya Afrika. 

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*