MADEREVA WA BODABODA WAENDELEA KUSAJILIWA KWENYE MFUMO MAALUM WA KUMBUKUMBU

 Waendesha bodaboda mkoani Mbeya wakiwa katika maandamano kuelekea kwenye Uwanja wa CCM Iromba kwenye uzinduzi wa mradi wa kuwasajili na kuwapatia sare maalumu za kuwatumbua.



 Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Mh. Nyerembe Mnase akihutubia hadhira kubwa ya waendesha bodaboda katika uzinduzi wa mradi wa kuwasajili katika mfumo wa kumbumbuku pamoja na kuwapatia sare maalumu.



 Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Kampuni ya Matangazo na Masoko ya Alternative Communications Bw. Edward Mgaya akizungumza na hadhira kabla ya kumkaribisha Mgeni rasmi katika uzinduzi wa mradi wa kuwasajiri waendesha bodaboda mkoani Mbeya.



 Meneja wa Kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom kanda ya Nyasa Bw. Minja akitoa salam za kampuni hiyo kama mdhamini wa mradi wa kuwasajili waendesha bodaboda katika mfumo maalumu wa kumbukumbu.


Ule mchakato kabambe wa kuwasajili waendesha bodaboda katika mfumo maalum wa kumbukumbu (database) na kuwakabidhi sare umeendelea kushika kasi ambapo wakati utekelezaji ukiendelea jijini Dar es salaam, mwishoni mwa wiki iliyopita uzinduzi wa mradi huo umefanyika kwa mbwembwe kubwa jijini Mbeya ambapo maelfu ya waendesha bodaboda jijini humo walijitokeza kwa shamrashamra tele kuuzindua mradi huo.
Uzinduzi huo wa aina yake uliofanyika katika Uwanja wa CCM Iromba jijini Mbeya, ni mwendelezo wa mchakato unaofanywa na kampuni ya mawasiliano, masoko na matangazo ya Alternative Communication ya jijini Dar es Salaam, ikishirikiana na jeshi la polisi na kudhaminiwa na kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom, lengo likiwa kuwasaidia waendesha bodaboda na abiria wanaotumia usafiri huo kutambulika kwa urahisi inapotokea wamehusika katika matukio ya kihalifu.
Akiuzindua mradi huo mgeni rasmi katika tukio hilo Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Mh. Nyerembe Mnase, aliwapongeza waendesha bodaboda hao kwa namna walivyoupokea mradi huo, na ameuagiza uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya kuakikisha wanawapa chama cha UWABOM chumba kimoja cha ofisi katika soko jipya la kimataifa la Mwanjelwa, na kwamba mradi wa kuwatambua bodaboda utausaidia uongozi wa jiji kupata takwimu sahihi, wakati ambapo jiji hilo linaandaa mkakati wa kuwatafutia eneo la viwanja vya ujenzi kwa ajili ya waendesha bodaboda. 
“Kwa hatua mliyofikia, tutawatafutia eneo la viwanja vya ujenzi ili muendelee zaidi kwa kuwa na makazi bora. Lakini nawasisitiza muendelee kuwa watii wa sheria barabarani, na kuwafichua wale wasio waaminifu wanaoshiriki katika vitendo vya kihalifu nyuma ya mgongo wa bodaboda.” Alisema. 
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Alternative Communication Bw. Edward Mgaya, aliwamwagia sifa waendesha bodaboda wa mkoani Mbeya kwa namna walivyofanikiwa kwa kiwango kikubwa kuutekeleza mradi huo, hadi kufikia hatua ya kufungua SACCOS ya wanachama wa Chama cha Wamiliki na Waendesha Bodaboda na Bajaj mkoani humo (UWABOM). 
Naye Katibu wa UWABOM Bw. Msumba Mdesa, katika risala kwa mgeni rasmi, uliushukuru mradi huo wa kuwasajili na kupewa sare, na kuongeza kuwa sare hizo zimewafanya wafanikiwe kujenga mshikamano wenye nia ya kujikwamua kwenye janga la umasiki, na wanachama kuwa na nidhamu ya hali ya juu katika kutii sheria bila shuruti.
Mradi wa kuwasajili waendesha bodaboda na kuwapatia sare maalum umekuja kufuatia madai kuwa baadhi yawaendesha bodaboda wasio kuwa waaminifu hujihusisha katika matukio ya kihalifu au kutumiwa na wahalifu kuvunja amani na kupotea bila ya kutambulika.
Kupitia mradi huu waendesha bodaboda waliosajiliwa pia watapata faida ya kupewa huduma ya bima ya afya, mafunzo ya usalama barabarani na  Ujasiriamali, huku kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom ambayo ndio wadhamini wa mradi, ikiwa imewatengea bodaboda kifurushi maalumu cha simu ambacho kina dakika 30 za maongezi, sms 500 na mb 100 za intanet kwa gharama ya shilingi 500 tu, na kikidumu kwa muda wa mwezi mmoja.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI