TAARIFA KWA UMMA KUHUSU MGONJWA ANAYEHISIWA KUWA NA UGONJWA WA KUTOKWA DAMU MKOANI KIGOMA

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

WIZARA YA AFYA NA USTAWI WA JAMII


TAARIFA KWA UMMA KUHUSU MGONJWA ANAYEHISIWA KUWA NA UGONJWA WA KUTOKWA DAMU MKOANI KIGOMA


 Utangulizi


Ugonjwa wa Ebola umeendelea kuenea katika nchi za Afrika ya Magharibi ambapo hadi sasa nchi tatu ambazo ni Guinea, Liberia na Siera Leone, zimeendelea kutoa taarifa za wagonjwa wapya. Aidha, mpaka tarehe 19 Julai 2015, idadi ya wagonjwa waliothibitishwa kuwa na ugonjwa huu ni 27,705 na vifo 11,269. Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imejiandaa vyema kudhibiti ugonjwa huu iwapo utaingia nchini ikiwa ni pamoja na kutengeneza mpango kazi wa udhibiti wa ugonjwa huu wa miaka mitatu kuanzia 2015 hadi 2017.


Historia ya Mgonjwa

Mnamo tarehe 9 Agosti 2015, mgonjwa mwenye umri wa miaka 39 kutoka katika kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu alipokelewa katika hospitali ya Mkoa wa Kigoma Maweni akiwa na dalili za kutokwa na damu sehemu mbalimbali za mwili hasusan kwenye fizi, macho na masikio. Vile vile alikuwa na dalili za kuchoka na mwili kuwasha. 
Mgonjwa huyu hakuwa na homa. Alipata matibabu katika hospital hiyo na kwa bahati mbaya mnamo tarehe 10 Agosti, 2015 mgonjwa huyu alifariki dunia. Mgonjwa huyu alikuwa hana historia ya kusafiri kutoka nje ya mkoa wa Kigoma wala kutembelewa na mtu aliyesafiri kutoka nchi za Afrika Magharibi zenye ugonjwa wa Ebola.


Mgonjwa huyu alikuwa ni mkimbizi wa kutoka nchi ya Burundi ambaye ameishi katika kambi ya Nyarugusu kwa miaka mitatu. Mgonjwa huyu alikuwa mmojawapo wa wakimbizi waliokuwa wasafirishwe katika mpango wa kawaida chini ya Shirika la Kimataifa linalohudumia wakimbizi kwenda Marekani. Safari hiyo ilikuwa ianze tarehe 9 Agosti 2015.


Hatua zilizochukuliwa

  1. Mgonjwa huyu alipatiwa matibabu katika hospitali ya Maweni Kigoma mpaka mauti ulipomkuta.
  2. Uongozi wa Afya Kigoma unafuatilia ndugu wa karibu wa mgonjwa huyu, pamoja na wahudumu wa Afya waliomuhudumia mgonjwa huyu kuona kama wataonyesha dalili zinazofanana na ugonjwa aliokuwa nao mgonjwa huyu. Ufuatiliaji huo umeanza tarehe 9 Agosti 2015. Mpaka leo hakuna mtu mwingine, aliyeonyesha dalili za ugonjwa huu.
  3. Sampuli ya mgonjwa huyu imechukuliwa na kupelekwa kwenye maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii, ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii iliyopo Dar es Salaam kwa uchunguzi zaidi ili kujua chanzo cha ugonjwa huu.
  4. Mazishi ya marehemu huyo yamefanyika chini ya uangalizi wa Afya mkoa, kwa kuzingatia Utaratibu wa Kanuni za Kimataifa za kuzuia maambukizi.



Hitimisho

Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inapenda kuwahakikishia wananchi kuwa mpaka sasa, hakuna uthibitisho wowote kuwa mgonjwa huyu amekufa na ugonjwa wa Ebola. Aidha kwa kuwa ugonjwa bado unaendelea nchi za Afrika Magharibi, Wizara inazidi kusisitiza wananchi kuchukua tahadhari za kujikinga na ugonjwa wa Ebola na magonjwa mengine ya kuambukiza. Ikiwa ni pamoja na

  • Kuepuka kugusa au kuingiwa na mate, damu, mkojo, jasho, kinyesi, machozi  na majimaji mengine yanayotoka  mwilini mwa mgonjwa mwenye dalili za ugonjwa  wa Ebola kupitia sehemu zenye michubuko au vidonda.
  • Kuepuka kushughulikia maiti ya mtu aliyekufa akiwa na dalili za ugonjwa wa Ebola; badala yake watoe taarifa kwa uongozi wa kituo cha kutoa huduma za Afya kwa ushauri. Wataalam watasimamia maziko ikiwa kifo kitatokea.
  • Wananchi waepuke mila na desturi zinazoweza kuchelewesha kupata huduma muhimu na kuzidi kueneza ugonjwa wa Ebola.
  • Kutoa taarifa mapema kwa viongozi wa  Serikali na watoa huduma za Afya katika ngazi zote pale anapotokea mtu mwenye  dalili za ugonjwa wa Ebola.
  • Kuwahi katika vituo vya kutolea huduma za  Afya pale mtu anapohisiwa kuwa na dalili za  ugonjwa huu.
  • Kunawa mikono mara kwa mara ili kuepuka kusambaza ugonjwa ikiwa mtu atakuwa ameshika mgonjwa au mazingira yenye maambukizi.
  • Kutumia kemikali za kuua vijidudu kutakasa mikono.



Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii itatoa taarifa pindi majibu ya maabara yatakapopatikana.




Imetolewa na:

Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali – Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii


12 Agosti, 2015

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*