DC HAPI ATEMBELEA WANANCHI BUNJU, MBWENI WALIOKUMBWA NA MAFURIKO



Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es salaam Mh. Ally Hapi leo amewatembelea wananchi maeneo ya Bunju na Mbweni waliokuwa na kero mbalimbali.
Katika eneo la Bunju Kilungule, baadhi ya wananchi nyumba zao zimezungukwa na maji kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha. Mkuu wa Wilaya akiambatana na Katibu tawala wa Mkoa wa Dar es salaam na mainjinia wa manispaa alitembelea eneo hilo na kuona adha inayowapata wananchi.
Akipokea maelezo ya Mwenyekiti wa serikali ya mtaa na baadae kuzungumza na wananchi wa eneo hilo, mkuu wa wilaya aliambiwa na baadhi ya wakazi wa asili wa eneo hilo kuwa sehemu hiyo ilikua ni bwawa la maji miaka yote.
Wakazi hao ambao nyumba zao zimezungukwa na maji walimuomba Mkuu wa wilaya kusaidiwa pampu kubwa ili maji hayo yavutwe na kupelekwa kwenye mitaro upande wa pili wa barabara.

Akijibu maombi hayo Mh. Hapi aliwaagiza mainjinia wa manispaa kuhakikisha kuwa wanafanya utaratibu wa kupata pampu kubwa ya kuvuta maji hayo. Aidha, Mkuu huyo wa wilaya ya Kinondoni aliwaambia wananchi kuwa wale wote waliojenga  katika eneo hilo ambalo ramani inaonesha kuwa ni eneo la wazi wajiandae kuondoka.

"Serikali itawasaidia kutoa haya maji kama hatua ya dharura. Lakini suluhu ya kudumu ni kuwa waliojenga hapa wote wamejenga eneo la wazi tena ni bwawa. Hivyo lazima wajiandae kuhama.
Serikali kazi yake ni kuwaambia wananchi ukweli, hata kama ukweli huo utakua na maumivu. Hivyo ukweli wa jambo hili ni kuwa waliojenga hapa wahame."

Akitoa rai kwa viongozi wa serikali ya mtaa ambao wameshiriki katika kuuza eneo hilo kinyume na taratibu mh. Mkuu wa Wilaya aliagiza na kusema

" kila Mwananchi aliyejenga hapa aende ofisi ya mtaa kujisajili akiwa na vielelezo vyote vya kumiliki eneo hili na alikonunua. Kisha nipewe taarifa na uhakiki utafanyika. Kama kuna viongozi wa serikali ya mtaa walishiriki kuuzia watu viwanja hapa kinyume na ramani ambayo wao wana nakala yao basi wajiandae kuwajibishwa."

Katika hatua nyingine Mkuu wa Wilaya alitembelea eneo la Mbweni ambako Mwananchi asiyefahamika amejenga ukuta kuzunguka eneo la wazi. Hapi alifika eneo hilo na kujionea ukuta huo kisha akaagiza mtendaji wa mtaa pamoja na anayejenga ukuta huo kufika ofisini kwake kesho Ijumaa mchana wakiwa na vielelezo vyote na vibali vya ujenzi kama wanavyo.

Ziara ya mkuu wa wilaya inaendelea muda huu katika maeneo ya barabara za Sinza ambazo wakandarasi walipewa kujenga

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI