TAARIFA YA CAG YAWASILISHWA BUNGENI LEO. Isome yote hapa

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad akionesha kwa wanahabari (hawapo pichani), ripoti ya ukaguzi ya mwaka 2014/15 ambayo iliwasilishwa bungeni Dodoma leo.
 Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad akionesha kwa wanahabari (hawapo pichani), ripoti ya ukaguzi ya mwaka 2014/15 ambayo iliwasilishwa bungeni Dodoma jana. Kulia  Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali, Hilary Aeshi
 Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad (katikati), akimkabidhi Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali, Hilary Aeshi  ripoti ya ukaguzi ya mwaka 2014/15  iliyowasilishwa bungeni Dodoma jana.  Kulia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), Abdallah Chikota.

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad (kushoto), akimkabidhi  Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), Abdallah Chikota  ripoti ya ukaguzi ya mwaka 2014/15  iliyowasilishwa bungeni Dodoma

OFISI YA MDHIBITI NA MKAGUZI MKUU WA HESABU ZA SERIKALI
TAARIFA YA CAG KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSIANA NA RIPOTI ZA UKAGUZI ZA MWAKA 2014/15
Muhtasari wa Masuala yaliyopo kwenye Ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali zilizowasilishwa Bungeni, Tarehe 20 Aprili, 2016
 
1.0 Utangulizi
Ndugu wanahabari,
i. Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ni chombo kimojawapo kinachosimamia uwajibikaji kupitia taarifa mbalimbali za ukaguzi zinazotolewa kila mwaka. Taarifa hizo husaidia Bunge na Serikali kuhakikisha kuwa rasilimali za umma zinatumika kwa kuzingatia tija na ufanisi katika kutoa huduma kwa wananchi. Utoaji wa taarifa hizi, huisaidia Serikali kuhakikisha kuwa makusanyo ya maduhuli na fedha zilizoidhinishwa na Bunge zinatumika ipasavyo ili kufikia malengo yaliyowekwa.

ii. Pia kwa kuzingatia Sheria ya Ukaguzi wa Umma Namba 11 ya 2008, kifungu cha 28 inampa Mamlaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kufanya ukaguzi wa ufanisi kwa lengo la kuthibitisha ubanifu, tija na ufanisi wa matumizi yoyote ama matumizi ya rasilimali katika Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, Mashirika ya Umma na Taasisi nyinginezo husika kwa lengo la kujua, kuchunguza na kutoa taarifa.

iii. Ndugu wanahabari, naomba kutoa kwenu na kwa wananchi  muhtasari wa masuala muhimu yaliyopo kwenye ripoti za ukaguzi kwa mwaka wa fedha ulioishia tarehe 30 Juni 2015 zilizowasilishwa leo Bungeni  kwa mujibu wa  Ibara ya 143 inayonitaka kukagua na kutoa taarifa za ukaguzi za  Mihimili mitatu ya Dola ambayo ni (a) Serikali (b) Bunge na (c) Mahakama na kuziwasilisha Bungeni.

1.1 Idadi ya Taasisi zilizokaguliwa na Ripoti zilizotolewa
Ndugu Wanahabari,
Kwa mwaka wa fedha ulioishia tarehe 30 Juni 2015,nimefanya ukaguzi wa Hesabu kwa Taasisi 199 za Serikali Kuu; Mamlaka za Serikali za Mitaa 164 na Mashirika ya Umma102 kati ya mashirika 186. Aidha kwa upande wa miradi ya maendeleo nimetoa ripoti 799na kufanya jumla ya ripoti za ukaguzi wa fedha zilizotolewa kufikia1,264.Kwa upande wa Ripoti za Ukaguzi wa Ufanisi, kwa kipindi kinachoishia Machi 2016, nimeweza kutoa ripoti kumi na moja (11).

2.0 UTEKELEZAJI WA MAPENDEKEZO NILIYOYATOA MIAKA ILIYOPITA
2.1 Hali halisi ya utekelezaji wa mapendekezo ya ripoti kwa miaka iliyopita haditarehe 30 Juni 2015 ni kama ifuatavyo:
Jedwali Na.1:  Hali ya Utekelezaji wa Mapendekezo ya Kaguzi za Fedha
Na. Ripoti Jumla ya Mapendekezo yaliyotolewa Mapendekezo yaliyotekelezwa Mapendekezo ambayo utekelezaji wake unaendelea Mapendekezo ambayo utekelezaji wake haujaanza Asilimia ya mapendezo yasiyotekelezwa
1 Serikali za Mitaa 16 0 6 10 63%
2 Serikali Kuu 46 8 37 1 2%
3 Mashirika ya Umma 37 27 10 0 0
  Jumla 99 35 53 11
  Asilimia 100% 35% 54% 11%


2.2 Mapendekezo Yaliyotolewa katika Ripoti za Ukaguzi wa UfanisiZilizopita
Hali halisi ya utekelezaji wa mapendekezo ya kaguzi za Ufanisi yaliyotolewa katika ripoti za miaka ya nyuma ni kama ifuatavyo;

Ripoti Husika Jumla Idadi ya Mapendekezo yaliyotekelezwa Idadi ya Mapendekezo Yaliyopo Kwenye Utekelezaji Idadi ya Mapendekezo yasiyotekelezwa Asilimia ya Mapendekezo yasiyotekelezwa
Usimamizi, Tathmini, na Mgawanyo wa Bajeti kwa Ajili ya Huduma za Mama Wajawazito Nchini 19 9 9 1 5%
Usimamizi wa Utoaji wa Malipo ya Pensheni kwa Wastaafu Nchini 28 14 10 4 14%
Usimamizi wa Makusanyo ya Mapato ya Ushuru Katika Serikali za Mitaa 6 1 4 1 17%
Usimamizi wa Ukarabati wa Magari Yanayomilikiwa na Taasisi za Serikali 20 2 12 6 30%
Usimamizi wa Uvunaji wa Mazao ya Misitu Nchini 13 0 11 2 15%
Usimamizi wa Utoaji wa Huduma za Maji Mijini 27 3 22 2 7%
Jumla 113 29 68 16
Asilimia 100% 26% 60% 14%

Kwa ujumla Utekelezaji umekuwa si wa kuridhisha kutokana na taasisi za umma kutokuwa na mifumo madhubuti ya kutekeleza mapendekezo ya ukaguzi yanayotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kupitia ripoti anazozitoa.

3.0 HATI ZA UKAGUZI
Kwa mwaka ulioishia tarehe 30 Juni 2015 nilitoa jumla ya Hati za Ukaguzi 465 zinazohusu Serikali Kuu, Serikali za Mitaa na Mashirika ya Umma. Kadhalika, nimetoa Hati 799 zinazohusu Miradi ya Maendeleo kama ilivyoainishwa kwenye Jedwali hapa chini.


Jedwali 3: Mchanganuo wa Hati za Ukaguzi
Na. Taasisi zilizokaguliwa Idadi ya Taasisi zilizokaguliwa Aina ya hati za ukaguzi
Hati Safi Hati yenye shaka Hati isiyoridhisha Hati mbaya
1 Halmashauri 164 47 113 3 1
2 Serikali Kuu 199 180 18 1 0
3 Mashirika ya Umma 102 99 3 0 0
  Jumla Ndogo 465 326 134 4 1
  Asilimia 100% 70% 28.8% 1% 0.2%
4 Miradi 799 739 60 0 0
  Jumla Kuu 1,264 1065 194 4
1

4.0 MASUALAYALIYOJITOKEZA KWENYE TAARIFA ZA UKAGUZI WA SERIKALI KUU,SERIKALI ZA MITAA NA MIRADI YA MAENDELEO
4.1 Udhaifu katika Usimamizi wa Fedha za Umma
i. Katika Mwaka wa fedha 2014/15, kiasi cha Shilingi trilioni 6.45 kilitengwa kwa ajili ya maendeleo kwa Serikali Kuu pamoja na Serikali za Mitaa kukiwa na ongezeko la asilimia 13.60 ikilinganishwa na kiasi cha Shilingi trilioni 5.67 katika mwaka wa fedha 2013/14.  Aidha, Shilingi trilioni 13.41 zilitengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida kukiwa na ongezeko la asilimia 6.6 ikilinganishwa na kiasi cha Shilingi trilioni 12.57 kwa mwaka 2013/14.

ii. Taarifa za Hesabu zilizokaguliwa zilionyesha upungufu wa fedha zilizopelekwa Serikali Kuu pamoja na Serikali za Mitaa kinyume na bajeti iliyo idhinishwa na Bunge. Fedha za matumizi ya kawaida zilizopokelewa  ni Shilingi bilioni 807.65 wakati fedha kwa ajili ya matumizi ya maendeleo zilikuwa Shilingi trilioni 1.82.

iii. Aidha, kwa upande wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo kulikuwa na matumizi ya kiwango kidogo cha fedha. Kwa Serikali Kuu fedha za Miradi ya maendeleo ambazo zilitolewa lakini hazikutumika ni Shilingi bilioni 38.02 sawa na asilimia 1.29 na Shilingi bilioni 101.33 sawa na asilimia 18 kwa Serikali za Mitaa.
Pendekezo
Ninaishauri Serikali kuzipatia Taasisi za Serikali fedha za ruzuku kwa Matumizi ya Kawaida na Maendeleo kwa wakati na kwa kiasi kilichoidhinishwa na Bunge ili ziweze kutoa huduma bora kwa wananchi.

4.2 Ukusanyaji wa Mapato ya Ndani
4.2.1 Mapato yatokanayo na Kodi
Katika mwaka wa fedha 2014/15, mapato halisi yaliyokusanywa kutokana na kodi yalikuwa shilingi trilioni 10.8sawa na asilimia 89 ikilinganishwa na makisio yaliyopitishwa na Bunge ya shilingi trilioni 12 ambayo ni pungufu ya shilingi trilioni 1.2 sawa na asilimia 11.
4.2.2 Mapato yasiyotokana na Kodi
Mapato yasiyotokana na kodi yaliyokusanywa naSerikali Kuu kwa mwaka 2014/15 yalikuwa shilingi bilioni 617sawa na asilimia 86 dhidi ya makisio ya shilingi bilioni 717, hivyo kutofikia lengo la makusanyo kwa shilingi bilioni 100, sawa na asilimia 14 ya makisio yaliyoidhinishwa na Bunge.

Kwa upande wa Serikali za Mitaa kwa mwaka 2014/15 zilikusanywa Shilingi bilioni 409sawa na asilimia87 dhidi ya makisio ya shilingi bilioni 471, hivyo kutofikia lengo la makusanyo kwa shilingi bilioni 62 sawa na asilimia13.

Kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa, nimebaini mapungufu yafuatayo katika usimamizi wa makusanyo ya mapato kutoka vyanzo vya ndani:
i) Halmashauri nyingi hazifanyi tathmini ya kujua kiasi ambacho wakala anakusanya na kuwasilisha. Aidha,Halmashauri hizi zinategemea taarifa za mawakala hivyo kushindwa kukadiria vyanzo vingine vya mapato.

ii) Mamlaka za Serikali za Mitaa 76 hazikupokea kiasi cha shilingibilioni 5.30 kutoka kwa mawakala ikiwa ni mapato ya ndani yaliyokusanywa na mawakala mbalimbali.

iii) Mamlaka za Serikali za Mitaa 136 zilipanga kukusanya shilingi bilioni 319, zikafanikiwa kukusanya bilioni 236sawa na asilimia 74. Hivyohazikuweza kukusanya mapato yaliyotarajiwa ya jumla ya shilingi bilioni83 sawa na asilimia 26 kutoka katika vyanzo mbalimbali.

iv) Jumla ya shilingi bilioni 5 hazikurejeshwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ikiwa ni asilimia 30 ya mapato ya kodi ya viwanja yaliyokusanywa katika Halmashauri 74 kama inavyoelekezwa kwenye Aya ya 8 ya Waraka wa TAMISEMI (Na. CBD.171/261/01/148 wa tarehe 19 Novemba 2012).

4.3 Usimamizi wa Mapato Yatokanayo na Kodi
4.3.1 Usimamizi wa Misamaha ya Kodi
Taarifa ya makusanyo ya Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa mwaka ulioishiatarehe 30 Juni 2015 ilionesha kiasi cha misamaha ya kodi iliyotolewa kuwa ni Shilingi trilioni 1.6 sawa na asimilia 2 ya pato la ndani la Taifa. Kiwango hicho bado ni cha juu ikilinganishwa na lengo la Serikali la kupunguza misamaha hiyo kufikia kiwango kisichozidi asilimia 1ya pato la ndani la Taifa.
4.3.2 Udhaifu katika ushughulikiaji wa mapingamizi ya makadirio ya kodi
Kesi za muda mrefu katika Bodi za Rufaa za Kodi na katika Mahakama ya Rufaa Tanzania zimefikia Shilingi trilioni 6.9 ikiwa ni ongezeko la shilingi trilioni 5.2 sawa na asilimia 75 ikilinganishwa na Shilingi trilioni 1.7 katika mwaka wa fedha 2013/14. Hii imechangiwa na upungufu wa fedha katika Bodi za Rufaa na Mahakama pamoja na udhaifu katika mfumo wa kushughulikia kesi hizi ikiwemo upungufu wa wataalamu katika Bodi za Rufaa ya Kodi na Mahakama.

Aidha, mashauri ya mapingamizi ya kodi yenye thamani ya Shilingi bilioni 581 hayakufanyiwa kazi na kupatiwa ufumbuzi na Kamishna wa Mapato Tanzania hadi kufikia tarehe 30 Juni 2015.

Pia Mamlaka ilishindwa kukusanya amana ya kiasi cha Shilingi bilioni 192 kinyume cha Kifungu Na.12(3) cha Sheria ya Rufaa ya Mapato ya Kodi ya mwaka 2000 (kama iliyorekebishwa mwaka 2006).
4.3.3 Usimamizi wa ukusanyaji wa kodi
i) Bidhaa zenye kodi ya thamani ya Shilingi bilioni 111 zimekaa kwenye maghala ya forodha ya Serikali kwa muda mrefu kinyume na sheria ya usimamizi wa forodha kwa nchi za Afrika Mashariki. Hivyo imepelekea kiasi cha kodi hiyo kutokukusanywa na hivyo kuikosesha Serikali mapato.

ii) Katika mwaka wa fedha 2014/15, Ukaguzi wangu ulibaini uwepo wa bidhaa zilizohifadhiwa katika maghala kwa ajili ya kusafirishwa nje ya nchi ambazo zilipewa msamaha wa kodi wa Shilingi bilioni 9.1. Aidha, ushahidi unaoonyesha mauzo ya bidhaa hizi nje ya nchi haukuweza kupatikana wakati wa ukaguzi. Kwa sababu hiyo sikuweza kujiridhisha kwa kina kuwa bidhaa hizi ziliuzwa nje au ndani ya nchi na hivyo kujua uhalali wa msamaha wa kodi uliotolewa kama ni sawa kwa mujibu wa Kifungu Na. 115 (a) & (b) cha Sheria ya Usimamizi wa Kodi ya Forodha ya Afrika Mashariki ya mwaka 2004.

iii) Miamala 665 ya mafuta na mizigo katika bandari kavu ya ushuru wa forodha wa Shilingi bilioni 89 iliyosafirishwa kwenda Uganda, Burundi na Rwanda kupitia mipaka ya Rusumo, Kabanga na Mutukula haikuwa na ushahidi katika rejesta au kwenye mfumo wa kuthibitisha utokaji wake.

iv) Aidha, Mafuta yenye dhamana ya kodi ya Shilingi bilioni 5yalionekana kwenye mfumo wa forodha (TANCIS) kuwa yamesafirishwa kwenda nje ya nchi kupitia nchini (Transit fuel). Hata hivyo, hakukuwa na ushahidi wa kuthibitisha utokaji wa mafuta hayo.

Mapendekezo
i) Serikali iweke mkazo katika usimamizi wa misamaha ya kodi na marejesho yatokanayo na kodi na kuimarisha ukaguzi na uendeshaji wa misamaha na marejesho yatokanayo na kodi ili kupunguza wadai hewa katika mtandao wa walipa kodi ya ongezeko la thamani, yaani VAT. Aidha, Serikali iendelee kupitia sera na kanuni za misamaha na marejesho ya kodi ili kuimarisha maeneo hayo.

ii) Serikali itoe msamaha au kupunguza kiasi cha riba na tozo kwa wafanyabiashara watakaoweka wazi madeni yao, pia kuwapa nafasi ya kulipa kwa awamu ili kuwawezesha kumaliza madeni na kuokoa mapato ya Serikali.

iii) Serikali iharakishe usikilizwaji wa pingamizi za kodi za mda mrefu katika bodi za rufaa za kodi na mahakama ya rufaa ya Tanzania ili kuwezesha ukusanyaji wa kodi kwa wakati.

iv) Serikali iimarishe kaguzi na pelelezi za walipa kodi ili kuweza kubaini ukwepaji wa kodi; aidha ichukue hatua kali katika kukusanya kodi zilizobainika.

v) Serikali iimarishe uendeshaji na usimamizi wa utoaji wa mizigo na mafuta yanayoingizwa nchini kwa matumizi ya ndani au kusafirishwa kwenda nje ya nchi, kuzuia kuuzwa katika soko la ndani bila kulipiwa ushuru wa forodha stahiki. Aidha, iimarishe ukusanyaji wa kodi kwa haraka endapo bidhaa hizo zitagundulika kuuzwa katika soko la ndani kinyume na sheria.


4.4 Deni la Taifa
Kufikia tarehe 30 Juni, 2015 Deni la Taifa lilikuwa  Shilingi trilioni 33.54.Katika hili, deni la ndani lilikuwa Shilingi trilioni 7.99 na deni la njeni trilioni 25.55.Hili ni ongezeko la trilioni 7.05 sawa na asilimia 27 ikilinganishwa na deni la Shilingi trilioni 26.49 lililoripotiwa Juni 30, 2014.

Uchambuzi wangu umeonyesha kuwa malipo ya kugharamia madeni ya kiasi cha Shilingi trilioni 4.60 mwaka huu ni sawa na asilimia 46 ya makusanyo yandani ya Serikali ya Shilingi trilioni 10.8. Gharama hizo zikijumuisha na gharama nyingine kama vile mishahara ya wafanyakazi na likizo, Serikali hubaki na kiasi  kidogo cha fedha za kugharamia miradi ya maendeleo na huduma nyingine za kijamii.

Mapendekezo
Napendekeza yafuatayo kwa Serikali: (a) Kuongeza jitihada za ndani za kuhamasisha ukusanyaji wa mapato ili kujenga wigo mpana wa kulipa madeni (b) Kuwa na mpango maalum wa kimkakati kuhusu fedha ikiwa ni pamoja na kupunguza gharama na kuongeza mikopo yenye masharti nafuu, pamoja na kuratibu vizuri shughuli za fedha za kigeni hapa nchini.

4.5 Ukaguzi wa Vyama vya Siasa
Kati ya vyama vya siasa 22 vyenye usajili wa kudumu, ni chama kimoja tu  kilichowasilisha hesabu zake za kipindi cha miezi sita, kwa kipindi kinachoanzia Januari mpaka Juni, 2015. Vyama vingine 21 havikuwasilisha vitabu vya hesabu kwa ajili ya ukaguzi kinyume cha Kifungu Na. 14 cha Sheria ya Vyama vya Siasa Na.5 ya mwaka 1992.
Pendekezo
Nashauri Msajili wa Vyama vya Siasa afuatilie suala la uwasilishaji wa taarifa za fedha kwa wakati kulingana na matakwa ya kisheria.

4.6 Udhaifu katika Usimamizi wa Rasilimali-Watu na Taarifa za Mishahara
Suala lausimamizi wa Rasilimaliwatu na taarifa za mishahara limeendelea kuwa tatizo sugu. Licha ya kuripoti kwenye taarifa zangu za miaka ya nyuma, Serikali bado imeendelea kuwa na udhaifu katika usimamizi wa Rasilimaliwatu na taarifa za mishahara kama ifuatavyo:
i) Mishahara iliyolipwa kwa watumishi wa Serikali ambao hawapokazini
Mishahara iliyolipwa kwa watumishi ambao hawapo kazini katika Taasisi 16 za Serikali Kuu imeongezeka kutoka Shilingi milioni 141mwaka 2013/14 hadi kufikia Shilingi milioni 393 mwaka 2014/15. Aidha, kiasi cha Shilingi milioni 61kililipwa kwa Taasisi mbalimbali kama makato ya kisheria katika mishahara iliyolipwa kwa watumishi ambao hawapo kazini.
Kwa upande wa Serikali za Mitaa jumla ya Shilingi bilioni 2.7katika Halmashauri 74 zililipwa kama mishahara kwa wafanyakazi waliofariki, waliotoroka, kufa na kufukuzwa kazi na kiasi cha Shilingi milioni 721 kililipwa kama makato ya kisheria kwa Taasisi kama Mifuko ya Pensheni, Taasisi za Fedha, Bima ya Afya na Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa ajili ya wafanyakazi ambao hawapo kazini.

ii) Mishahara ambayo haikulipwa na haikurudishwa Hazina
Jumla ya Shilingi bilioni 2za mishahara haikulipwa kwa watumishi wa Taasisi moja ya Serikali Kuu na fedha hizo hazikurudishwa Hazina. Aidha, Shilingi bilioni 3 kwa watumishi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa 37 haikuweza kuthibitishwa kurudishwa Hazina.

iii) Makato ya Kisheria kutowasilishwa kwa Taasisi husika
Kiasi cha Shilingi milioni 707za makato ya kutoka Taasisi mbili za Serikali Kuu (RS Kilimanjaro na Katavi) hakikuwasilishwa katika Taasisi husika zikiwemo PSPF, NSSF na NHIF.
Mapendekezo
(a) Serikali inapaswa kuimarisha mfumo wa udhibiti wa ndani ili kuhakikisha kwamba, orodha ya malipo ya mishahara inahakikiwa na makato ya kisheria yanawasilishwa kwa wakati. (b) Kiasi cha malipo ya mishahara ambayo haikulipwa kwa wafanyakazi kirudishweHazina.
4.7 Udhaifu katika Ununuzi na Usimamizi wa Mikataba
Mapungufu yaliyobainishwa katika ripoti ya mwaka huu, yanajumuisha haya yafuatayo;
i) Vifaa vilivyonunuliwa zaidi ya mahitaji katika kipindi cha kuandikisha wapigakura kwenye daftari la kudumu  Shilingi milioni 827.Mpaka ukaguzi unafanyika vifaa vilikuwa bado havijatumika na muda wa mahitaji yake ulishapita;

ii) Ununuzi wa huduma za uchapishaji wenye thamani ya Shilingi bilioni 6 kuhusiana na vitabu vya Katiba Iliyopendekezwa ulikuwa na dosari kutokana na kutofuata sheria ya manunuzi. Aidha, nakala 158,003 za vitabu vya Katiba Iliyopendekezwa vilikuwa bado havijasambazwa kwa walengwa kwa madhumuni ya kuhamasisha Umma juu ya kura ya maoni;

iii) Vifaa vilivyonunuliwa nje ya Mpango wa manunuzi katika Taasisi saba (7)za Serikali Kuu Shilingi bilioni 8.46 na Halmashauri 4Shilingi bilioni 8;

iv) Manunuzi yenye thamani ya Shilingi milioni 494 yalifanyika bila ya idhini ya Bodi ya Manunuzi katika Serikali Kuu na Halmashauri 11 Shilingi milioni 825;

v) Manunuzi yenye thamani ya Shilingi bilioni 27 katika Taasisi nane za Serikali Kuu yalifanyika bila kushindanisha wazabuni.

vi) Bidhaa na huduma zenye thamani ya Shilingi bilioni 15.4 zilinunuliwa katika Taasisi 16 za Serikali Kuu bila kuwapo ukaguzi wa kuthibitisha ubora wakati wa mapokezi.

vii) Manunuzi ya bidhaa na huduma yenye thamani ya Shilingi bilioni 5yalifanyika bila mikatabakatika Taasisi nne za Serikali Kuu;

viii) Bidhaa na huduma zilizolipiwa kiasi cha Shilingi bilioni 3.25 hazikupokelewa wala huduma kutolewa katika Taasisi nne za Serikali Kuu;

ix) Baadhi ya Taasisi hazikusimamia kwa umakini mikataba mbalimbali iliyoingiwa na wakandarasi. Mapungufu hayo yalichangia ucheleweshaji wa ukamilishaji wa miradi mbalimbali na miradi kuwa chini ya kiwango. Taasisi zenye mapungufu zinajumuisha Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na matengenezo ya majengo ya Balozi kadhaa kama vile Maputo, Msumbiji na New York, Marekani.

Pendekezo
Nazishauri Mamlaka husika kutathmini zabuni kwa uwazi nakuhakikisha kuwa haki inatendeka na kanuni zinazotumika kufanya tathmini kwa wazabuni wote zinafanana.

4.8 Udhaifu katika  Usimamizi wa Matumizi
Katika mwaka huu wa fedha nimebaini udhaifu mbalimbali katika usimamizi wa matumizi ya fedha za Serikali katika maeneo yafuatayo:

i) Malipo yaliyofanyika bila ya viambatisho vya kutosha
Hati za malipo hazikupatikana wakati wa ukaguzi, risiti za kielectroniki hazikuambatanishwa, namalipo yasiyoambatanishwa na risitiya Shilingi bilioni 18 kwa Serikali Kuu. Wakati huo huo, Mamlaka za Serikali za Mitaa zilifanya malipo yenye nyaraka pungufu ya kiasi cha Shilingi bilioni 8.

ii) Matumizi yaliyofanyika nje ya bajeti
Matumizi yenye thamani ya Shilingi bilioni 1.3katika Serikali Kuu na Shilingi bilioni 1.6 kwa Halmashauri za Wilayayalifanyika nje ya bajeti iliyoidhinishwa na Bunge. Vilevile, Halmashauri za Wilaya 48 zilitumia kiasi cha Shilingi bilioni 2.9 kugharamia uchaguzi wa Serikali za Mitaa fedha ambazo hazikuwepo kwenye bajeti iliyoidhinishwa na Bunge.

Pia, Halmashauri za Wilaya 34 zilitumia kiasi cha Shilingi bilioni 33 kugharamia ujenzi wa maabara za Sekondari fedha ambazo hazikuwa kwenye bajeti iliyoidhinishwa na Bunge.


iii) Masurufu ya muda mrefu yasiyorejeshwa ya Shilingi milioni 233.
iv) Malipo yasiyokuwa na manufaa yaliyofanyika katika Taasisi nane za Serikali Kuu yaShilingi bilioni 53ikijumuisha tozo mbalimbali, riba na malipo zaidi ya gharama halisi.
v) Malipo yaliyofanywa nje ya bajeti iliyoidhinishwa na Bunge Shilingi bilioni 1.8.
vi) Kodi ya zuio ambayo haijakatwa ya Shilingi milioni 693.


Pendekezo
Bila ya kuwapo kwa kumbukumbu na nyaraka zakutosheleza, malipo yaliyofanyika hayawezi kuthibitika kuwa sahihi; hivyo, fedha za Umma zinaweza kutumika bila utaratibu wa sheria na kwa njia bora. Uongozi wa Taasisi husika unatakiwa uimarishe udhibiti wao wa ndani ili kuhakikisha kwamba, shughuli za usimamizi wa matumizi zinafuata Sheria ya Fedha za Umma na Kanuni zake.

4.9 Udhaifu katika Utendaji wa Wakala wa Serikali
i) Ukaguzi unaonyesha kuwa upungufu umeendelea kuwapo katika kuzingatia sheria na kanuni za Ununuzi, hivyo kuwapo kwa usimamizi mbovu wa mikataba. Ukaguzi ulibaini kutofuatwa kwa taratibu za ununuzi kama vile mabadiliko ya mikataba kutoidhinishwa na Bodi za Zabuni, ununuzi wa mabasi ya mwendo kasi (DART) zaidi ya mahitaji, Kuchelewa kuanza kwa huduma ya mabasi ya mwendo kasi, Magari yaliyolipiwa/nunuliwa ambayo hayajapokelewa kwa muda mrefu, ununuzi uliofanyika nje ya wazabuni waliothibitishwa na kuingia mikataba isiyokuwa na kikomo cha muda wa utekelezaji.

ii) Kulingana na mikataba niliyoikagua, malipo yanatakiwa kufanyika ndani ya siku 28 baada ya kuidhinishwa kwa hati ya malipo. Hata hivyo, kuna ucheleweshwaji wa malipo hadi kufikia siku 100 kuanzia siku hati ya malipo inapoidhinishwa. Mathalani,Wakala wa Barabara Tanzania imedaiwa Shilingi bilioni 5.6 kutokana na riba ya ucheleweshaji wa malipo yaliyoidhinishwa; Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini kuna ongezeko la riba ya mkopo ya asilimia 15 sawa na Shilingi bilioni 13 inayohusu ujenzi wa jengo lake;

iii) Katika usimamizi wa mapato, nilibaini kuwa Wakala wa Majengo (TBA) imeshindwa kukusanya kiasi cha Shilingi million 215 za mauzo ya nyumba. Pia, nilibaini kuwapo kwa udhaifu katika kupeleka mapato benki shilingi milioni 51;

iv) Aidha, nilibaini kiasi cha Shilingi milioni 976kulipwa kwa wazabuni mbalimbali bila kuwapo risiti za kielektroniki (EFD), Shilingi milioni 21.2 malipo ya kodi ya zuio (Withholding Tax), pamoja na hasara ya Shilingi milioni 43 iliyotokana na kutonunuliwa kwa kalenda na vitabu vya shajala zilizotengenezwa na GPSA.

4.10 Udhaifu katika Usimamizi wa Mali
Kasorozilizobainika katika usimamizi wa mali za kudumuni kama ifuatavyo:
i) Kuchelewa kwa kazi ya kuzitambua na kuthamanisha Maliza Kudumu. Katika kufanya ukaguzi wa taarifa za fedha zilizotayarishwa na Mamlaka za Serikali za Mitaa nimebaini kuwa Mamlaka nyingi zimeshindwa kutekeleza matakwa ya Viwango vya Kimataifa vya Utayarishaji wa Hesabu katika Sekta ya Umma (IPSAS 17). Mamlaka zimeshindwa kuthamanisha mali zake ndani ya kipindi cha mpito cha miaka mitano kinachoruhusiwa na aya ya 95 na 96 ya IPSAS 17.
ii) Mamlaka nyingi za Serikali za Mitaahazikuonyesha thamani halisi ya Mali zake za Kudumu na pia Rejista ya mali za kudumu hazikuwa kamilifu;

iii) Baadhi ya nyumba katika Balozi za Tanzania nje ya nchi ziko katika hali mbaya hivyo kuhitaji matengenezo ambazo ni Kinshasa, Pretoria, Kampala, Cairo, Harare, New Delhi, London na Stockholm.Pia Balozi nne (Abuja, Adis Abbaba, Kigali na London) zina viwanja ambavyo havijaendelezwa na hivyo kupelekea hatari ya kuvipoteza kwa kufutiwa umiliki;

iv) Taasisi 14 ya Serikali Kuu zilizokaguliwa zimebainika kuwa na vifaa vyenye thamani ya Shilingi bilioni 4 vilivyonunuliwa ambavyo havikuingizwa katika leja;

v) Ukosefu wa Sera ya kiuhasibu ya kusimamia mali za kudumu inayoendana na mfumo mpya wa uandaaji wa taarifa za fedha katika Taasisi za Umma;

vi) Aidha, ilibainika kuwa Jeshi la Zimamoto halina magari ya zimamoto ya kutosha.Magari yaliyopo ni 55 wakati mahitaji ni 157. Pia, vifaa vya kuzima moto vilivyoko kwenye baadhi ya majengo ya Serikali havifanyiwi matengenezo.

4.11 Udhaifu katika Usimamizi wa Madeni
Nilibaini malimbikizo ya madeni katika Taasisi 91 ikijumuisha Wizara/Idara 52, Sekretarieti za Mikoa 25, na Balozi 14 ambazo, kwa pamoja  zilikuwa na madeni ya kiasi cha Shilingi trilioni 1.4hili ni ongezeko la Shilingi bilioni 671sawa na asilimia 89 ikilinganishwa na mwaka uliopita ambapo madeni yalikuwa Shilingi bilioni 773. Hii imesababisha kuongezeka kwa malimbikizo ya madeni kwa sababu madeni ya miaka ya nyuma yanalipwa kwa kutumia bajeti ya mwaka mwingine.

Deni lililoonyeshwa linajumuisha kiasi cha Shilingi bilioni 28 ambalo ni deni linalotokana na gharama za wagonjwa wanaotibiwa katika hospitali za rufaa nchini India.Aidha, nilibaini malimbikizo ya madeni ya kiasi cha shilingi bilioni 31 yanayohusiana na Wakala wa Serikali.
4.12 Udhaifu katika urejeshaji wa  Mikopo ya Elimu ya Juu kutoka kwa wanufaika
Tathmini niliyoifanya kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa 51 imebaini kuwa wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu inayotolewa na Bodi ya Mikopo “HESLB” yenye jumla ya Shilingi milioni 914hawakukatwa marejesho ya mikopo hiyo kwenye mishahara yao. Suala hili pia lilijitokeza katika Serikali Kuu.

Mapendekezo
Ninaishauri Serikali kuhakikisha kuwa maafisa Masuuliwanawasilisha taarifa za waajiriwa wake katika bodi ya Mikopo zikionesha majina yao halisi na yalewaliyoyatumia kwa ajili ya kuomba mikopo ya elimu ya juu kama inavyotakiwa na Sheria ya Bodi ya Mikopo ya mwaka 2004.

Aidha, nashauri Maafisa Masuuli waiarifu Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) juu ya ajira ya wanufaika na wahakikishe makato yanafanyika kutoka katika mishahara yao na kuiwasilisha kwenye Bodi husika.

5.0MASUALA MUHIMU YALIYOMO KWENYE RIPOTI ZA UKAGUZI WA FEDHA WA MASHIRIKA YA UMMA
5.1 Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) linajiendesha kwa Hasara
i) Katika ukaguzi wangu nimebaini shirika halina ndege za kutosha, gharama za uendeshaji zisizohimilika, uhaba wa mtaji wa kujiendesha pamoja na udhaifu wa menejimenti. Aidha, nimebaini Shirika lina upungufu wa wafanyakazi katika sekta muhimu na wafanyakazikatika eneo la uendeshaji (operational staff) wanaozidi mahitaji. Vilevile ShirikalinatumiaCheti cha Uendeshaji kilichokwisha muda wake toka tarehe 31, Machi 2010.

ii) Ukaguzi umeonyesha kuwa menejimenti ya Shirika la Ndege Tanzania haina mkakati mahsusi wa kulifufua Shirika hilo. Mapitio ya Mipango Mikakati ya Kampuni ya vipindi viwilivya mwaka 2007-2012na mwaka 2015-2020 haionyeshi dalili yoyote ya kulitoa Shirika katika hali yake ya sasa.

iii) Bila kuwa na mpango madhubuti wa kulifufua Shirika, juhudi zinazoendelea za kupata mkopo kwa ajili ya kununua ndege nyingine zinaweza zisiwe na manufaa. Shirika linapaswa kutengeneza mpango mahsusi wa kulifufua wenye malengo ya kulisaidia ili liweze kujiendesha lenyewe kwa faida.

5.2 Mamlaka ya Bandari Tanzania
i) Mita za kupima Mafuta Hazitumiki
Katika ripoti zangu za nyuma, nimekuwa nikiishauri Mamlaka ya Bandari Tanzania kutumia mita za kupimia mafuta yanayoingizwa nchini kwa kupitia bandari. Hata hivyo, mpaka nakamilisha ukaguzi wa mwaka 2014/15 bado Mamlaka hiyo ilikuwa haitumii mita hizo. Naendelea kusisitiza umuhimu wa Mamlaka kutumia mita hizo kwa ajili ya kudhibiti mapato ya Serikali.

ii) Uchakavu waKarakana ya Ketengeneza Meli
Mamlaka ya Bandari ya Dar es Salaam ina karakana ya kutengeneza meli (dry dock) ambayo ilijengwa miaka ya 1950. Mamlaka haijaweka mikakati ya kuifanyia matengenezo makubwa karakana hiyo ili kuiongezea ufanisi.Miundombinu yake imechakaa na haiwezi kutengenezeka na baadhi ya vifaa vilitolewa kufuatia uendelezaji wa karakana namba 13 na 14. Aidha, nilibaini kwamba matengenezo ya matishari kwa muda mrefu sasa yamekuwa yakifanyika katika Bandari ya Mombasa ambapo kiasi cha Shilingi bilioni 1.33 kilitumika kwa matengenezo hayo.iii) Kukosekana kwa Mfumo wa Kutambua Makontena
Nimebaini kuwa Mamlaka ya Bandari Tanzania haina uwezo wa kufahamu na kusimamia taarifa za makontena yanayopokelewa na TICTS kwa kuwa Mamlaka hiyo haina haki ya kuingia katika mfumo wa kompyuta wa TANCIS ambao unatumiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania kuhifadhi taarifa hizo. Hivyo, Mamlaka ya Bandari inategemea taarifa zinazotoka TICTS ambazo zinaweza zisiwe sahihi.

iv) Kasoro Kadhaa Katika Mkataba baina ya TICTS na TPA
Ukaguzi umebaini kasoro kadhaa katika mkataba baina ya TICTS na Mamlaka ya Bandari.Kwanza, umiliki wa asilimia 51 ya hisa wa Kampuni ya TICTS ulihamishwa kwenda kwa Kampuni ya Hutchison International Port Holdingtarehe 30 Desemba, 2005 kinyume na matakwa ya mkataba.

Kulingana na Mkataba, endapo kiwango cha ufanyaji kazi kwa mwaka kitashuka chini ya asilimia 25, mkataba unaweza kutenguliwa. Hata hivyo kwa miaka mitano mfululizo tangu kuingiwa kwa mkataba huo mwaka 2000, TPA haikufanya tathmini ya ufanisi kinyume na makubaliano ya mkataba. Mnamo mwaka 2007, Mamlaka ya Bandari ilifanya tathmini ya ufanisi wa TICTS tangu mwaka 2000 na ikagundua kuwa kiwango cha ufanyaji kazi cha TICTS kilishuka kwa zaidi ya asilimia 25. Hata hivyo pamoja na mapungufu haya kugunduliwa, mkataba huu haukuvunjwa bali walihamisha mkataba kwa Kampuni ya Hutchison International Port Holding.

v) Meli 85 zilizotia nanga hazikuonekana katika mfumo wa mapato waMamlaka ya Bandari
Ukaguzi uliofanyika kwa mwaka 2014/15 umebaini kati ya meli 1,253 zilizotia nanga meli 145 hazikuonekana katika mfumo wa mapato wa Mamlaka hiyo. Menejimenti ilifanikiwa kupata nyaraka zinazohusu meli 60 tu kati ya meli 145 huku ikishindwa kutolea ufafanuzi wa kutoonekana kwa meli 85 zilizosalia.

vi) Tofauti ya Mifumo kati ya TPA na TRA
Kadhalika, Ukaguzi ulibaini kuwepo kwa tofauti kati ya mfumo wa mapato wa Mamlaka ya Bandari na mfumo wa Mamlakaya Mapato Tanzania (TANCIS). Tunashauri kuwepo kwa usuluhishiwa taarifa wa mara kwa mara kati ya Taasisi hizi mbili.

5.3 Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) Kuendeshwa kwa Hasara
Kampuni ya Simu Tanzania imekuwa ikipata hasara kubwa kwa muda mrefu.Hadi kufikia mwisho wa mwaka 2014, Kampuni ilikuwa imepata hasaraya jumla ya kiasi cha Shilingi bilioni 361 (2013: bilioni 334). Hali hii inatokana na mtandao wake wa mawasiliano ya simu za mkononi kutopatikana maeneo mengi; kutokuwa na teknolojia za kisasa, kutokuwa na njia za usambazaji zenye ufanisi na kukosa fedha za kukuza biashara ikilinganishwa na makampuni mengine ya simu.

Pendekezo
TTCL kujengewa mazingira mazuri ya kufanya biashara kwa ushindani katika huduma zake zote.

5.4 Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA)
Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzaniailiingiza nchini bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani milioni 2.3 ambazo ni sawa na Shilingi bilioni 4.6 bila kuzifanyia ukaguzi. Sababu zilizotolewa na Mamlaka ni upungufu wa wafanyakazi.

5.5 Bohari ya Kuu ya Dawa (MSD)
i) Ukaguzi umebaini kuwa kuna bidhaa zenye thamani ya Shilingi bilioni 2 ambazo katika kumbukumbu zinaonekana zipo njiani kutoka katika Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kutoka mwezi Mei, 2012.

ii) Aidha, nilibaini kuwa bidhaa zenye thamani ya shilingi bilioni 18 zilikaa katika maghala ya Bohari kwa muda mrefu na hivyo kuwa katika hatari ya kuharibika.

5.6 Mamlaka ya Udhibiti wa Anga (TCAA)
Udhaifu wa mkataba kati ya TCAA na  COMSOFT Gmbh
Mamlaka ya Udhibiti wa Anga ilikuwa na mikataba na kampuni ya COMSOFT Gmbh ya thamani ya Shilingi bilioni 7.1 kwa ajili ya zabuni tatu za mfumo wa malipo ya bili, ADS-B awamu ya kwanza na awamu ya pili, ambapo mikataba miwili ilisainiwa na mmoja haukusainiwa kutokana na kutokukamilika kwa majadiliano. Yafuatayo yalibainika;

a) Gharama za Mkataba wa ADS-B awamu ya kwanza kama ulivyoainishwa kwenye mpango wa manunuzi ulikuwa ni Shilingi bilioni 1.02. Hata hivyo mkataba ulisainiwa kwa Shilingi bilioni 3.81 bila ya kuwa na kibali cha Bodi.
b) Vilevile kabrasha ya zabuni iliyowasilishwa na COMSOFT Gmbh liliondolewa baadhi ya vipengele muhimu ikiwemo udhibiti wa ndani hivyo kumrahisishia COMSOFT kupata zabuni hii. Hata hivyo October 2015, mzabuni alitangazwa kufilisika kabla ya kukamilisha kazi.
c) Aidha, kulingana na mkataba mfumo wa malipo ya bili ulitakiwa kukamilika mwezi Septemba 2015, lakini hadi Novemba 2015, utekelezaji wa mkataba ulikuwa katika hatua za awali za usanifu.

Pendekezo
Mamlaka inashauriwa kuangalia manufaa ya mradi huu na kuzingatia athari za kufilisika kwa muuzaji wa mfumo huo na hivyo kuchukua hatua stahiki kuepusha Mamlaka kupata hasara.

5.7 Benki ya Maendeleo ya TIB
i) Kutorejeshwa kwa mkopo uliotolewa chini ya mpango wa Kusafirisha Bidhaa Nje kwa Dhamana ya Serikali (Export Credit Guarantee Scheme)
Benki ya Maendeleo ambayo ni (Benki Tanzu ya Benki ya Uwekezaji Tanzania) inaidai Kampuni ya Agricultural and Animal Feed Industry (SAAFI) kiasi cha Shilingi bilioni 2.5 fedha iliyoikopesha kwa ajili ya kuiwezesha Kampuni kulipa mkopo wa shilingi bilioni 15 uliotolewa na Serikali kupitia mpango wa Kusafirisha Bidhaa Nje kwa Dhamana ya Serikali (Export Credit Guarantee Scheme) chini ya usimamizi wa Benki ya Uwekezaji uliolenga kukuza Sekta ya Kilimo na Chakula. Kiasi chote cha Shilingi bilioni 17.5hakijareshwa kwa zaidi ya miaka kumi (10) sasa.

Kwakuwa utendaji wa Kampuni ya SAAFI haukuwa wa kuridhisha, Benki ya Uwekezaji Tanzania iliamua kuubadilisha mkopo huo kuwa asilimia 20 ya uwekezaji wa Benki katika Kampuni hiyo. Menejimenti haikutoa maelezo ya kuridhisha juu ya vigezo vilivyotumika kumiliki asilimia 20 tu wakati sehemu kubwa ya mali za Kampuni hii zimepatikana kwa mkopo wa Serikali.

ii) Aidha, kampuni nyingine tano (5) zilikuwa na deni katika “Mpango wa Kusafirisha Bidhaa Nje kwa Dhamana ya Serikali” lenye jumla ya Shilingi bilioni 45.71. Kampuni hizo ni Arusha Blooms Ltd (bilioni 10.1), Kiliflora Ltd (bilioni 11.8), Tengeru Flowers Ltd (bilioni 7.5); na Mount Meru Flowers (bilioni 16.3).  

Pendekezo
Ninaishauri Menejimenti ya TIBkufuatilia urejeshaji wa madeni haya na mengineyo ili kuepuka kudhoofisha utendaji wa Benki.


5.8 Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC)
Katika mwaka wa fedha 2014/2015, Kampuni ya Songas ililipa gawio la Dola za Marekani milioni 3.9 kwa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC). Hata hivyo, katika mapitio ya vitabu vya hesabu vya Songas vinavyoishia tarehe 31 Desemba, 2014 vilivyokaguliwa, tulibaini kuwa Songas ilitangaza kulipa gawio la kiasi cha Dola za Marekani milioni 15. Kutokana na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania kuhodhi asilimia 29 za hisa katika Kampuni ya Songas, ilipaswa kupokea kiasi cha Dola za Kimarekani Milioni 4.35. Hii inaamanisha kuwa, kiasi cha Dola za Marekani 477,000 sawa na takribani Shilingi milioni 965 hazikulipwa kwa Shirika kama gawio kutoka Songas.

5.9 Kutokuwepo kwa Bodi za Mashirika ya Umma
Katika mwaka wa ukaguzi wa 2014/15, kulikuwa na Mashirika 22 ambayo hayakuwa na Bodi za Wakurugenzi hadi kufikia wakati wa kukamilika kwa ukaguzi wangu mwezi Machi, 2016. Baadhi ya Mashirika hayo hayakuwa na bodi kwa zaidi ya mwaka mmoja wa fedha. Kutokuwepo kwa bodi hizo kunazifanya Taasisi husika kukosa usimamizi.

Pendekezo
Ninapenda kuzishauri Mamlaka za Uteuzi kuunda Bodi hizo ili ziweze kusimamia Taasisi zake kikamilifu.

5.10 Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA)
i) Mamlaka ya mawasiliano Tanzania inaendesha mfumo wa udhibiti wa mawasiliano ya simu (TTMS) ambao unafuatilia mwenendo wa mawasiliano ya simu kutoka kwa watoa huduma za mawasiliano waliopewa leseni. Mfumo huu wa mawasiliano kwa sasa unaweza kudhibiti mapato yatokanayo na mawasiliano ya Kimataifa na haujaweza kudhibiti mapato yatokanayo na mawasiliano ya ndani. Aidha, kukosekana kwa mawasiliano ya kutosha kati ya Taasisi muhimu zinazoweza kunufaika na mtambo huu, kama vile Mamlaka ya Mapato Tanzania na Benki Kuu ya Tanzania kumesababisha Serikali kuendelea kupoteza mapato yatokanayo na mawasiliano ya simu za ndani.

ii) Aidha, nilibaini kukosekana kwa usimamizi wa gharama za simu wakati wa kutuma na kupokea pesa kupitia makampuni ya simu (mobile money banking) kwa Benki Kuu ya Tanzania pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania.

Pendekezo
Upo umuhimu wa kuunganisha Mamlaka ya Mapato Tanzania katika mfumo huo wa mawasiliano na kuhakikisha kuwa usimamizi kupitia Mamlaka husika (Benki Kuu na Mamlaka ya Mapato) unaimarishwa ili kuongeza udhibiti wa mapato unaotokana na mawasiliano ya ndani na nje ya nchi.

5.11 Shirika la Maendeleo la Taifa  (NDC)
i) Malipo ya asilimia 90 ya fedha za Mkataba bila kuwepo kwa dhamana
Shirika la Maendeleo la Taifaliliingia mkataba wa kusanifu, kusambaza, kufunga, kupima na kuweka kiwanda cha uzalishaji wa viuatilifu na ujenzi wa maabara ya kibaolojia na kifamasia (LABIOFAM) wenye thamani ya Yuro milioni 16.8.Lengo ni kupunguza malaria na matumizi ya Serikali kwenye ununuzi wa dawa na gharama nyingine zinatokana na kupambana na malaria. Ukaguzi ulibaini kuwa, Shirika lililipa asilimia 90 ya fedha za mkataba kwa LABIOFAM bila kuwepo kwa dhamana yeyote.
Pamoja na ufunguzi rasmi wa kiwanda uliofanyika tarehe 2 Julai 2015, hadi sasa kiwanda bado hakijaanza uzalishaji kutokana na hitilafu ya kiufundi iliyobainika wakati wa majaribio ya mitambo siku chache kabla ya ufunguzi rasmi.
Sambamba na gharama za matumizi mengine, Shirika la Maendeleo la Taifa bado linalipa mshahara kwa meneja wa mradi ambaye yupo kwenye eneo la ujenzi wa kiwanda. Shirika pia lilianzisha Kampuni ya Tanzania Biotech Products ambayo imeajiri wafanyakazi zaidi ya 130 ambao wanalipwa mishahara kila mwezi licha ya mradi kuchelewa kuanza uzalishaji.

ii) Kutokuthibitishwa kwa kiasi cha Dola za Marekani milioni 600 kama mtaji wa Sichuan Hongda LTD
Mnamo tarehe 21 Septemba, 2011, Shirika la Maendeleo la Taifa, Sichuan Hongda (Group) Company Limited na Tanzania China International Mineral Resources LTD (TCIMRL) walisaini mkataba wa ubia wa kuendesha Tanzania China International Mineral Resources Ltd, ikiwa ni kampuni iliyoanzishwa ilikutekeleza mradi wa Mchuchuma na Liganga.

Sichuan Hongda (Group) Company Ltd ilikubali kuchangia kiasi cha Dola za Marekani milioni 600 kama mtaji kwa TCIMRL ili zitumike kwa ajiliya maendeleo ya utekelezaji wa mradi. Hata hivyo, nilibaini kuwa hapakuwepo na utaratibu uliowekwa wa kuweza kuhakiki na kuthibitisha kiasi cha pesa kilichotolewa na Hongda hadi sasa kama sehemu ya mtaji iliyokubali kutoa.

Baada ya kupitia mkataba wa ubia ilibainika kwamba, Sichuan Hongda (Group) Company Ltd inamiliki asilimia 80 ya hisa za TCIMRL wakati asilimia 20 inamilikiwa na Shirika la Maendeleo la Taifa. Bado uchangiaji wa ziada wa kiasi kisichozidi Dola za Marekani bilioni 2.4 utadhaminiwa na mali za kampuni ya ubia zikijumuisha haki za uchimbaji (mining rights) badala ya rasilimali za Hongda Sichuan (Group).

Umiliki wa asilimia 20 wa Shirika la Maendeleo la Taifa ndani ya TCIMRL haujahusisha ukweli kwamba mkopo huo unadhaminiwa na mali za kampuni ikiwemo haki za uchimbaji.5.12 Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC)
i) Kutowasilishwa kwa taarifa za utekelezaji wa miradi ya TIC
Wakati wa ukaguzi nilipitia wawekezaji 45 waliokuwa wamepewa motisha ya uwekezaji na Kituo. Ukaguzi ulibaini kuwa wawekezaji 41 kati ya 45 sawa na asilimia tisini na moja (91) hawakuwasilisha taarifa kwa Kituo juu ya utekelezaji wa miradi yao.

ii) Kukosekana kwa Mfumo wa Uhakiki wa Misamaha ya Kodi
Kituo cha Uwekezaji huwasilisha orodha ya vifaa vinavyohitaji msamaha wa kodi kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania ili iweze kutoa msamaha huo. Kwa kipindi cha Julai 2012 hadi Juni 2015, Kituo kilifanikiwa kuandikisha jumla ya miradi 2,095 ambayo yote ilipitishwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania kwa ajili ya kupata msamaha. Hata hivyo, ukaguzi ulibaini kuwa, Kituo hakina mfumo unaokiwezesha kufuatilia misamaha hiyo ili kujiridhisha kuwa misamaha hiyo inatumiwa na wawekezaji kwa madhumuni yaliyoombewa. Pia hakuna utaratibu wa uhakiki kutoka TRA kama misamaha inayotolewa ndiyo TIC iliidhinisha.

5.13 Tathmini ya Zoezi la Ubinafsishaji
i) Tofauti ya Mapato kati ya iliyokuwa Kampuni Hodhi ya Mali za Serikali(CHC) na Vitabu vya Ufilisi wa Mashirika
Tumebaini kuwa taarifa za mapato yatokanayo na uuzwaji wa mali za Mashirika yaliyobinafsishwa na iliyokuwa Kampuni Hodhi ya Mali za Serikali (CHC) zamani ikiitwa PSRC haziendani na kiwango cha mauzo kilichopo katika taarifa za ufilisi wa Shirika.

ii) Taarifa za ufilisi katika Idara ya Ufilisi ya CHC na Idara ya Fedha hazikuwa katika mtiririko unaoendana. Kutofanyika kwa usuluhisho wa taarifa ya ufilisi kati ya Kitengo cha Fedha na Idara ya Ufilisi inaweza kupelekea makosa katika taarifa muhimu za Shirika na hivyo kusababisha upotevu wa mali za Mashirika haya yaliyobinafsishwa.
iii) Hati saba (7)za umiliki wa ardhi zilizokuwa za SIMU 2000 hazikuonekana wakati wa ukaguzi.

iv) CHC kutofungua akaunti maalum ya makusanyo ya Ufilisi
Nilibaini kuwa CHC haikufungua akaunti maalum ya makusanyo ya mauzo kinyume cha kifungu cha 34(2) cha Sheria ya Mashirika ya Umma Na. 16 ya mwaka 1993 (kama ilivyorekebishwa). Badala yake, mapato yanayotokana na mauzo ya Mashirika ya Umma yalikuwa yanaingizwa katika akaunti ya jumla.

Pendekezo
Ninashauri kwamba mapato yote yatokanayo na mauzo yajayo, yapelekwe benki kwenye akaunti maalum kulingana na Sheria ya Mashirika ya Umma na kisha kupelekwa Hazina kama Sheria Na. 16 ya mwaka 1993 ya Mashirika ya Umma inavyotaka.

5.14 Kiwanda  cha  Karatasi Mgololo (SPM) kutoilipa Serikali kiasi cha Dola za Marekani Milioni 25
Katika ripoti zangu za nyuma nimekuwa nikiripoti juu ya Kiwanda cha Karatasi Mgololo (SPM) kilichouzwa kwa thamani ya Dola za Marekani milioni 26. Hata hivyo, Serikali ilipokea kiasi cha Dola za Marekani milioni moja tu. Kiasi kilichobaki cha Dola za Marekani milioni 25 kiliwekezwa katika kiwanda. Hata hivyo, Serikali haikupata hisa yoyote kutokana na fedha zilizowekezwa. Hadi naandika taarifa hii, hakuna ushahidi wa hatua yoyote iliyochukuliwa na Serikali kuhusu suala hili.

5.15 Mauzo ya Hisa za Shirika la Usafiri Dar es Salaam
Bodi ya Wakurugenzi ya UDA iliuza hisa za Shirika bila kupata kibali cha Serikali. Hisa za Shirika la UDA zilithaminishwa kwa bei ya Shilingi 744.79 kwa kila hisa mwezi Oktoba, 2009, na mwezi Novemba, 2010 thamani ya kila hisa ikawa 656.15. Hata hivyo, katika uuzaji huo, Bodi ya Wakurugenzi ya UDA ilitoa punguzo la asilimia 60 kwa kila hisa kwa mwekezaji huyo (kwa Tathmini ya bei ya hisa ya mwezi Oktoba, 2009), bila kuwepo na sababu za kufanya hivyo. Kwa mujibu wa majibu ya Mlipaji Mkuu wa Serikali, Serikali haitambui uuzwaji wa hisa hizo.

Kulingana na mkataba wa kuwasilisha hisa wa tarehe 11 Februari, 2011 mnunuzi (mwekezaji) atalipa jumla ya Shilingi bilioni 1.14 kama bei ya ununuzi wa hisa zote ambazo zilikuwa hazijagawiwa, ingawa mkataba haukuonyesha akaunti ya benki ambayo malipo yangefanyika. Mnunuzi (mwekezaji) alilipa kiasi cha Shilingi milioni 285 pekee katika akaunti namba 0J1021393700 ya benki ya CRDB inayomilikiwa na UDA. Hakukuwa na malipo mengine ya ziada yaliyofanywa na mwekezaji kuhusiana na ununuzi wa hisa za UDA. Mwenyekiti wa Bodi alipokea kiasi cha Shilingi milioni 320 kupitia akaunti yake binafsi kutoka kwa Mwekezaji ambayo kwa mujibu wa mwenyekiti huyo ilikuwa ni ada ya ushauri alioutoa kwa Mwekezaji. Malipo haya yalizua mgongano wa kimaslahi. Wakati Serikali haitambui uuzwaji wa hisa za UDA, ninashauri Shirika la UDA lirudishwe chini ya usimamizi wa Serikali hadi hapo mgogoro huu utakapotatuliwa.
Suala hili lilihojiwa katika ripoti zangu za miaka iliyopita na Serikali imewasilisha majibu kwa Ofisi yangu kuwa inaandaa mapendekezo ya kuuza asilimia 49 ya hisa za UDA na kufikishwa mbele ya Baraza la Mawaziri. Hata hivyo, majibu hayo hayaonyeshi kama hisa ambazo ziliuzwa bila kufuata utaratibu zitarejeshwa Serikalini na hatua zilizochukuliwa dhidi ya Bodi ya Wakurugenzi wa UDA kutokana na kukiuka taratibu za uuzaji wa hisa za Shirika hilo.

Pendekezo
Msajili wa hazina anashauriwa kufuatilia utekelezaji kwenye ubinafsishaji wa kiwanda hiki kama ilivyoainishwa katika makubaliano ya mkataba wa mauziano na mlipaji mkuu.

Ndugu Wanahabari
Kama nilivyoeleza awali nimekagua Mashirika 102 kati ya 186,Muhtasari huu umeainisha masuala toka katika baadhi ya Mashirika,hivyo nawashauri msome ripoti zote kwa kina ili muweze kupata kwa undani masuala yaliyoripotiwa katika taarifa za Mashirika hayo.

6.0 MAMBO MUHIMU YALIYOMO KWENYERIPOTI ZAUFANISI
Ndugu Wanahabari,
Katika eneo la ukaguzi wa ufanisi nimetoa ripoti ya Jumla na ripoti za kisekta kama ifuatavyo:

6.1 Ripoti ya Jumla ya Ukaguzi wa Ufanisi
Kwa upande wa Ripoti ya Jumla ya Ukaguzi wa Ufanisi kwa kipindi kinachoishia Machi 2016, nimefanya uchambuzi ili kuangalia jinsi Taasisi za Serikali zinavyosimamia data, upimaji, na ufuatiliaji wa utendaji katika kutekeleza majukumu yake na kubaini yafuatayo:


i) Usimamizi wa data katika Sekta ya Umma
Taasisi za Serikali hazizalishi na kuhifadhi katika kiwango cha kutosha data zinazopatikana kutoka katika vyanzo mbalimbali. Kuna udhaifu katika mapitio ya data zinazopatikana ndani na nje ya Taasisi. Matokeo yake, data potofu zinatumika bila kuzirekebisha. Hii ni kutokana na ukosefu wa utaratibu wa wazi wa kuwezesha kuhakikiwa data zinazozalishwa. Kwa mfano, katika ujenzi wa miradi ya maji ya Bukoba, Musoma na Chalinze mhandisi mshauri aliyetakiwa kuandaa usanifu na makadirio ya ujenzi alifanya makosa katika kuandaa makadirio ya kazi yaliyo sahihi.

Makadirio haya hayakufanyiwa uhakiki na Wizara ya Maji. Wakati wa utekelezaji wa miradi, baadhi ya vitu viliongezwa na hivyo kusababisha ongezeko la ziada la shilingi bilioni 16.31 kama inavyoonekana katika Jedwali hapa chini.

Jedwali 2: Makosa katika vitu vilivyokadiriwa na kuthaminiwa chini ya gharama halisi kwenye makadirio ya ujenzi
Fungu namba Vitu vilivyothaminiwa kwa gharama ya chini (Sh. Milioni) Vitu vilivyoachwa kwenye makadirio ya ujenzi (Sh. Milioni) Jumla (Sh. Milioni)
Fungu la 2 1896.5 246.4 2142.9
Fungu la 3 613.0 17.4 630.4
Fungu la 4 218.0 36.1 254.1
Fungu la 5 766.2
496.3
1262.5
Fungu la 6 1215.9
452.1 1668.0
Fungu la F &H 1623.5
3207.9
4831.4
Bukoba 2003.2 416.6 2419.8
Musoma 2607.1 494.8 101.9
Jumla 10,943.40 5,367.6 16,311


ii) Upimaji wa utendaji katika Sekta ya Umma
Upimaji wa utendaji katika Taasisi za Sekta ya Umma haukufanyika vizuri na hivyo kuonesha udhaifu katika kupima na kuelewa kiwango cha utendaji wa vyombo mbalimbali vya Sekta ya Umma.

Hii inatokana na vyombo vingi vya Serikali kutokuwa na mifumo mizuri ya upimaji wa maendeleo ya utendaji inayoweza kutumika kuongoza na kuelekeza kila Taasisi za Umma namna ya kutathmini utendaji wake katika kutoa huduma kwa wananchi.

iii) Ufuatiliaji katika Sekta ya Umma
Kuna udhaifu katika usimamizi, tathmini, na mawasiliano katika Taasisi zilizokaguliwa. Hii imeathiri utendaji mzima wa shughuli na utoaji wa huduma kwa Umma. Wadau hawatekelezi kwa ufanisi majukumu yao kwa sababu hawapati taarifa kwa wakati muafaka.
Kadhalika, tathmini hazifanyiki katika kiwango cha kutosha. Mapungufu katika ufuatiliaji, tathmini, na mawasiliano ya matokeo ya utendaji yanazuia upatikanaji wa taarifa sahihi ambazo zingeweza kutumika kwa ajili ya maboresho ya siku zijazo.

Mapendekezo
Ofisi ya Waziri Mkuu ihakikishe kuwa Wizara, Idara zinazojitegemea, Mashirika, Wakala na Mamlaka za Serikali za Mitaa zote:

Usimamizi wa data
i) Zinaanzisha na kuboresha mifumo ambayo itawezesha upatikanaji na utunzaji sahihi wa data zinazopatikana kutoka katika vyanzo mbalimbali kwa matumizi ya kiofisi na utekelezaji wa shughuli zilizoainishwa; na
ii) Zinaanzisha mfumo wa mapitio ili kuhakikisha kuwa data zote zinazopokelewa kutoka vyanzo mbalimbali zinahakikiwa kwa lengola kuhakikisha kuwa ni kamili na sahihi kabla ya kutumika.

Upimaji wa utendaji:
i) Kupitisha na kutumia upimaji wa utendaji. Kwa njia hiyo, taarifa za utendaji za mwaka za kila Taasisi zizalishwe na kutumika kama kipimo cha kutathmini kiwango chao cha utendaji katika utoaji wa huduma; na
ii) Kuwepo na utambuzi na uchaguzi sahihi wa viashiria vya utendaji ambavyo vitatumika kupima utendaji na huduma zitolewazo kwa wananchi.

Usimamizi wa ufuatiliaji katika Sekta ya Umma
i) Kubuni mfumo wa ufuatiliaji kwa namna ambayo taarifa zitakusanywa, kuchunguzwa, kujumuishwa na kutumika ipasavyo ili kuongoza na kujifunza ufumbuzi wake; na

ii) Kubuni mfumo wa ufuatiliaji utakaotoa mwongozo wa mtiririko wa taarifa kwa ufanisi kati ya Taasisi na ngazi mbalimbali za utawala ili kurahisisha utoaji wa maamuzi.

6.2 Ripoti za Ukaguzi wa Kisekta
Kuhusu Ukaguzi wa Ufanisi kwa kipindi kinachoishia Machi 2016, niliweza kutoa ripoti kumi na moja (11) katika maeneo yafuatayo:
i) Usimamizi wa Mikataba ya Ujenzi wa Miradi ya Maji Mijini katika Wizara ya Maji na Umwagiliaji;
ii) Usimamizi wa Milipuko ya Magonjwa na Visumbufu vya Mimea;
iii) Mfumo wa Udhibiti wa Ubora wa Elimu Nchini Tanzania;
iv) Udhibiti wa Usafi kwenye Mchakato wa Uzalishaji wa Nyama Nchini;
v) Usimamizi wa Taarifa za Mitetemo, Taarifa za Sampuli za Kijiolojia;
vi) Usimamizi wa Mchakato wa Ugawaji wa Leseni za Utafutaji na Uendelezaji wa Mafuta na Gesi Asilia Nchini Tanzania;
vii) Uendelezaji wa Rasilimaliwatu Katika Sekta ya Mafuta na Gesi Tanzania;
viii) Usimamizi wa Uzingatiaji na Utekelezaji wa Sera, Sheria, na Kanuni za Mazingira katika Shughuli za Utafutaji wa Petroli Tanzania;
ix) Mchakato wa Tathmini ya Athari za Mazingira Katika Miradi ya Maendeleo;
x) Ukaguzi wa Ufanisi katika Utekelezaji wa Masharti ya Ushirikishaji wa Watanzania na Uhakiki wa Urejeshaji wa Gharama za Uwekezaji kwenye Mikataba ya Mgawanyo wa Mapato ya Uzalishaji; na
xi) Ufuatiliaji wa Utekelezaji wa Mapendekezo ya Kaguzi za Ufanisi Yaliyotolewa katika kaguzi zilizopita.

Masuala yaliyoonekana katika kila ripoti ya Ukaguzi wa Ufanisi ni kama yalivyainishwa hapa chini:


6.2.1 USIMAMIZI WA MIKATABA YA UJENZI WA MIRADI YA MAJI MIJINI KATIKA WIZARA YA MAJI NA UMWAGILIAJI
Zaidi ya Shilingi bilioni 500 zimetumika kati ya mwaka 2010/2011 na 2013/14 kutekeleza miradi ya maji. Hata hivyo, yamekuwepo malalamiko kuhusiana na utekelezaji wa miradi hiyo. Kati ya maeneo yaliyolalamikiwa ni udhaifu katika usimamizi wa mikataba.
Lengo la ukaguzi huu lilikuwa ni kutathmini  iwapo Wizara ya Maji na Umwagiliaji ina mfumo bora wa kusimamia ujenzi wa miradi ya maji kwa lengo la kupunguza upotevu wa fedha  unaotokana na kiwango duni cha miradi, nyongeza isiyo ya lazima ya gharama za miradi, na kuchelewa kukamilisha miradi ya maji. Ukaguzi ulihusisha miradi ya maji ya Chalinze, Bukoba na Musoma ambapo mradi wa Chalinze uligawanywa katika vipande 7 wakati miradi ya Bukoba na Musoma haikugawanywa katika vipande.

Ukaguzi ulibaini yafuatayo:
i) Shughuli za Usanifu wa Miradi na Zabuni za Miradi hazikuwa Madhubuti
Kulikuwa na udhaifu katika uandaaji wa mikataba na utekelezaji wa shughuli za awali za mikataba. Mapungufu katika usanifu yalisababisha ongezeko la gharama ya jumla ya Shilingi bilioni 12.5 na Dola za Marekani 38,110 ambazo zilichangia kiasi cha asilimia 45 ya gharama zote za nyongeza katika miradi tisa (9) iliyochaguliwa.

ii) Ucheleweshaji wa utekelezaji wa miradi ya maji
Miradi imechelewa kuanzia miezi 9 hadi miaka 4. Sababu kubwa za ucheleweshaji huu zilikuwa ni: kuchelewa kuwalipa wakandarasi; kuchelewa kuidhinisha mabadiliko ya aina ya mabomba kutoka chuma kwenda plastiki; utendaji mbovu wa wakandarasi; nyongeza ya kazi; pamoja na usimamizi mbovu wa wataalamu washauri.


iii) Ongezeko la gharama za ujenzi
Miradi 8 kati ya 9 iliyokaguliwa ilikuwa na ongezeko la gharama kuanzia asilimia 10 hadi asilimia 229 ya gharama zilizopo kwenye mikataba ambayo ni sawa na jumla ya Shilingi bilioni 30. Sababu kuu za ongezeko hili ni kubadilisha mwelekeo wa mabomba; nyongeza ya muda wa mradi; kuongezeka kwa gharama za awali; mabadiliko ya aina ya mabomba kutoka ya chuma kwenda plastiki; gharama za riba kutokana na kuchelewa kuwalipa wakandarasi; kubadilisha gharama za mradi kimakosa; na gharama za mwajiri kwa ajili ya usimamimizi wa mradi.

iv) Ubora usioridhisha wa miradi
Ubora wa miundombinu ya maji haukuwa wa kuridhisha kwa sababu zifuatazo;
Mkandarasi wa mradi wa Chalinze Kipande F na H hakufuata sifa na vigezo vilivyowekwa kwenye mkataba wake. Matokeo yake alijenga miundombinu yenye kiwango cha chini ambayo ilikuwa na makosa mengi hali iliyosababisha mkataba huo kuvunjwa. Mpaka muda wa kuvunja mkataba mkandarasi alikuwa ameshalipwa jumla ya Shilingi bilioni 7.54 kwa kazi alizokuwa amefanya. Baadaye aliajiriwa mkandarasi mwingine ili afanye kazi ya kurekebisha kazi zilizofanywa vibaya na mkandarasi wa awali kwa gharama ya shilingi bilioni 3.08.
Mabadiliko ya aina ya mabomba kutoka chuma kwenda plastiki. Hili lilifanyika kinyume na mapendekezo ya mkandarasi mshauri. Mabadiliko haya yalisababisha ongezeko la gharama kiasi cha Shilingi bilioni 1.28 pamoja na ongezeko la muda wa miezi 11.

v) Udhaifu wa usimamizi wa mikataba ya miradi ya maji
Wizara ilishindwa kuchukua hatua zinazostahili kwa makosa yaliyoonekana katika utekelezaji wa miradi ikiwa ni pamoja na kutoza faini za ucheleweshaji wa miradi na kuvunja mikataba kwa wakandarasi waliokiuka masharti ya mikataba yao.

Hitimisho lililofikiwa kuhusu usisimamizi wa miradi ya maji
Ukaguzi ulihitimisha kwamba usimamizi wa mikataba ya utekelezaji wa miradi ya maji haulindi maslahi ya Umma. Wizara ya Maji na Umwagiliaji imeshindwa kuchukua hatua zinazostahili ili kuhakikisha kwamba wakandarasi, wataalamu wa ushauri, pamoja na Wizara yenyewe wanatekeleza majukumu yao kama yalivyoainishwa kwenye mikataba.

Pendekezo
Ninapendekeza Wizara ya Maji na Umwagiliaji ihakikishe inafanya uhakiki wa usanifu wa miradi, sifa na vigezo, michoro, pamoja na nukuu za makadirio ili kuzuia makosa katika dodoso la zabuni ikiwa ni pamoja na kuimarisha usimamizi wa miradi ya ujenzi wa maji pamoja na utendaji wa wataalamu washauri.

6.2.2 USIMAMIZI WA MILIPUKO YA MAGONJWA NA VISUMBUFU VYA MIMEA
Ukaguzi ulibaini kuwa karibu mikoa yote nchini imeathiriwa na milipuko mbalimbali ya magonjwa na visumbufu vya mimea. Halmashauri ambazo zimeathirika na wadudu aina ya viwavijeshi ni kati ya Halmashauri 4 hadi 66 ambapo eneo lililoathirika ni kati ya hekta 81 hadi 200,000. Mwaka 2014 madhara yaliyosababishwa na ndege aina ya kweleakwelea kushambulia mashamba, yalikuwa makubwa ambapo hekta 1,344 zinazokadiriwa kuzalisha tani 4,704 za mpunga ziliathiriwa na kusababisha hasara ya takribani Shilingi bilioni 5. Kadhalika, katika Wilaya ya Muleba Mkoani Kagera, jumla ya migomba 2,887,653 yenye thamani ya shilingi billioni 29 iling’olewa kufuatia kushambuliwa na ugonjwa wa mnyauko.

Pia, ilibainika kuwepo kwa udhibiti hafifu wa milipuko ya magonjwa na visumbufu vya mimea nchini; Kukosekana kwa mifumo madhubuti ya kujikinga na milipuko ya magonjwa na visumbufu vya mimea; ukaguzi katika maeneo ya mipakani kutofanyika vizuri kutokana na upungufu wa wakaguzi na vitendeakazi muhimu katika maeneo hayo; wakulima kukosa uelewa wa matumizi ya njia unganishi za kujikinga na visumbufu vya mimea; na upatikanaji mdogo wa mbegu bora za kilimo na viwatilifu ili kuzua milipuko ya magonjwa na visumbufu vya mimea.

Kasoro zingine ni ushirikiano mdogo baina ya wadau katika usimamizi wa milipuko ya magonjwa na visumbufu vya mimea; na kukosekana kwa mfumo wa Ufuatiliaji na Tathmini kwenye milipuko ya magonjwa na visumbufu vya mimea.

Hitimisho la ukaguzi
Ukaguzi ulihitimisha kwamba licha ya kuwa hali ya milipuko ya magonjwa na visumbufu vya mimea kuwa miongoni mwa sababu zinazopelekea upotevu wa mazao ya kilimo, Wizara ya Kilimo, Mifugo, na Maendeleo ya Uvuvi na Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa hazijaweza kuweka na kutekeleza mikakati ya kutosha ya kukabiliana na milipuko ya magonjwa na visumbufu vya mimea nchini.

Pendekezo
Ninapendekeza kwamba Wizara ya Kilimo, Mifugo, na Maendeleo ya Uvuvi itilie mkazo suala la uchunguzi wa kina ili kubaini uwepo wa magonjwa na visumbufu vya mimea kwa lengo la kupunguza upotevu wa mazao na gharama kubwa za kukabiliana na milipuko.

Aidha, Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa inapaswa kuwa na mfumo ambao utaimarisha ushirikiano wa taarifa za milipuko ya magonjwa na visumbufu vya mimea baina yake na Wizara ya Kilimo, Mifugo na Maendelo ya Uvuvi.

6.2.3 MFUMO WA UDHIBITI WA UBORA WA ELIMU NCHINI TANZANIA
Ubora wa elimu ni kati ya mambo ambayo Serikali inajitahidi kuboresha. Hata hivyo, elimu itolewayo bado ina mapungufu katika kuhakikisha mwanafunzi anaongeza ujuzi.
Lengo la ukaguzi lilikuwa ni kubaini kama Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia, na Mafunzo ya Ufundi  na Ofisi ya Rais –Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa zina mfumo madhubuti wa  kudhibiti ubora wa elimu ambao unazingatia na kuhakikisha kwamba Walimu wana sifa stahiki, kuna vitabu mahsusi, vyakutosha na matokeo ya mitihani yanatumika kuboresha elimu nchini.

Ukaguzi wa sampuli ya shule zilizokaguliwa ulibaini yafuatayo:
i) Uwepo wa walimu wasio na sifa. Walimu 969 (sawa na asilimia 0.5) wa shule za msingi na walimu 2,108 (sawa na asilimia 2.2) wa shule za sekondari hawana sifa stahiki.
ii) Uhaba wa mafunzo kazini ambapo walimu 74,701 (sawa na asilimia 69) wa shule za msingi hawakupatiwa mafunzo.
iii) Udhibiti usioridhisha wa utendaji wa walimu hivyo kusababisha walimu kutosimamiwa ipasavyo na hata kutopandishwa madaraja yao kwa wakati muafaka.
iv) Uandishi na uzalishaji wa vitabu unaofanywa na Taasisi ya Elimu Tanzania haukidhi mahitaji. Taasisi ya Elimu haijaandika vitabu mahususi vya kiada kama ilivyotarajiwa.
Matokeo ya mitihani hayajatumika vya kutosha na taasisi husika katika kuleta maboresho na kupelekea mapendekezo hayo kujirudia rudia katika kipindi cha miaka mitatu mfululizo.

Hitimisho la Ukaguzi
Ukaguzi ulihitimisha kwamba mfumo wa kudhibiti ubora wa elimu nchini hautekelezwi kiufanisi ili kuhakikisha kwamba walimu wana sifa zinazohitajika, usahihi na ubora wa vitabu unazingatiwa, na matokeo ya mitihani yanatumika ipasavyo kama chachu ya kuboresha ufundishaji na ujifunzaji.

Pendekezo
Ninapendekeza kwamba Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia, na Mafunzo ya Ufundi ihakikishe kwamba mikakati na mipango endelevu inawekwa ili kuwepo na tathmini ya kudumu kwa lengo la kubaini mapungufu waliyonayo walimu na kuwapatia mafunzo ili kukidhi mahitaji yao ya kitaaluma, maarifa, na mbinu za kufundishia.

Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ihakikishe kwamba inaanzisha utaratibu maalumu utakaoweza kutambua mahitaji ya waalimu kwa kuzingatia mahitaji mahususi ya maeneo husika. Pia, kuwepo na mwongozo na maelekezo ya namna ya kugawa walimu katika maeneo yote nchini.

6.2.4 UDHIBITI WA USAFI KWENYE MCHAKATO WA UZALISHAJI WA NYAMA NCHINI
Ukaguzi ulibaini kuwa machinjio 9 kati ya 12 (sawa na asilimia 75 ya yaliyotembelewa) yalikuwa yanafanya kazi katika hali ya uchafu. Kukosekana kwa vifaa vya kuoshea miguu na mikono kabla ya kuingia kwenye machinjio hali hii ilipelekea uwezekano wa watendaji kutoka maliwatoni na maeneo mengineyo kwenda kwenye uzalishaji nyama bila ya kujifanyia usafi kuondoa vijidudu hatarishi; na kutokuwepo kwa mfumo mzuri wa usimamizi wa uchafu utokanao na shughuli za machinjio ni baadhi ya masuala yaliyobainika.

Kasoro zingine zilizoonekana ni kutofanyika mara kwa mara kwa upimaji wa afya kwa watu wanaofanya kazi kwenye machinjio; nyama kusafirishwa kwenye hali ya uchafu ndani na nje ya machinjio; na udhaifu kwenye ukaguzi wa machinjio.

Uwepo wa machinjio yanayofanya kazi kwenye hali ya uchafu na ambayo hayajasajiliwa. Hali hii imesababishwa na uwepo wa Taasisi zaidi ya moja zilizopewa jukumu la kusajili machinjio. Ukaguzi ulibaini yafuatayo katika Halmashauri saba zilizotembelewa:
i) Machinjio sita kati ya kumi na mbili (sawa na asilimia 50) hayakusajiliwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa kutokana na kutokidhi vigezo vya kusajiliwa.
ii) Machinjio kumi kati ya kumi na mbili (sawa na asilimia 83) hayakusajiliwa na Wizara ya Kilimo, Mifugo, na Maendeleo ya Uvuvi kutokana na kutokidhi viwango. Hata hivyo, machinjio hayo yalikuwa yanaendelea kufanya kazi.
iii) Machinjio matatu kati ya sita yaliyosajiliwa yanafanya kazi katika hali ya uchafu.

Ukaguzi wa wanyama na nyama ulikuwa haufanyiki ipasavyo. Aidha, kulikuwa na usimamizi na ufuatiliaji duni wa udhibiti wa usafi kwenye uzalishaji wa nyama unaofanywa na Wizara na Tawala za Mikoa.
Hitimisho la Ukaguzi
Ukaguzi ulihitimisha kwamba hakuna uhakika kuwa nyama inayopelekwa kwa Umma wa watanzania ni salama kwa matumizi ya binadamu. Vigezo vinavyotumiwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa; Wizara ya Kilimo, Mifugo na Maendeleo ya Uvuvi; na Bodi ya Nyama Tanzania vinatoa mwanya wa kusajili machinjio ambayo yanakosa vigezo  muhimu vya kudhibiti usafi na usalama  wa nyama wakati wa uzalishaji wake.

Pendekezo
Ninapendekeza kwamba shughuli nzima ya usajili wa machinjio iangaliwe upya ikiwa ni pamoja na utangamanishaji wa vigezo vinavyotumika katika usajili. Wizara ya Kilimo, Mifugo, na Maendeleo ya Uvuvi iandae mfumo wa kupima utendaji katika udhibiti wa usafi kwenye uzalishaji wa nyama. Pia waanzishe mfumo utakao hakikisha na kusaidia shughuli za ukaguzi wa nyama na machinjio kufanyika ipasavyo.

6.2.5 MCHAKATO WA TATHMINI YA ATHARI ZA MAZINGIRA KATIKA MIRADI YA MAENDELEO
Ukaguzi ulibaini yafuatayo:
i) Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira halina uwezowa kutambua miradi yote iliyotakiwa kusajiliwa.
ii) Vibali mbalimbali vya uendelezaji miradi vilitolewa pasipo kuonesha uthibitisho kuwa Baraza limeridhia;
iii) Kutohusishwa kwa wadau muhimu wakati wa kupitia nyaraka za awali zinazoelezea miradi ilivyo hasa Serikali za Mitaa ambako miradi husika inatekelezwa;
iv) Mikutano ya kamati ya wataalamu kwa sehemu kubwa ilihusisha maofisa kutoka Baraza bila kuwahusisha maofisa (Wataalamu) kutoka Serikali za Mitaa na Wizara husika za kisekta. Hivyo, mikutano ya kamati ya wataalamu ilikosa maoni ya Wizara, Idara za Serikali, na Serikali za Mitaa;
v) Tathmini za Kimazingira hazikuweza kubaini masuala yenye athari kubwa kwa mazingira kama vile ujenzi wa kituo cha Kuhifadhia Mabasi ya Mradi wa Mabasi yaendayo Kasi katika eneo la Jangwani Dar es salaam;
vi) Uhaba mkubwa wa maofisa mazingira  katika mamlaka za Serikali   za  Mitaa; na
vii) Uhaba wa wakaguzi wa mazingira wenye vibali vya kufanya kazi za kikaguzi.

Hitimisho la ukaguzi
Ukaguzi ulihitimisha kwamba Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira na Ofisi ya Makamu wa Rais- Idaraya Usimamizi wa Mazingira hawasimamii ipasavyo mchakato wa tathmini ya athari za mazingira au ukaguzi wa mazingira katika miradi ya maendeleo. Mchakato hauhakikishi kwamba miradi yote ambayo huenda ikawa na athari hasi kwa mazingira haisajiliwi; na kuhakikisha kuwa miradi yote inatathminiwa na hatua zote stahiki za kupunguza athari zinazooneshwa katika taarifa za tathmini ya athari ya mazingirana zinatekelezwa.

Pendekezo
Ninapendekeza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira liweke mfumo madhubuti wa kutambua miradi yote inayotakiwa kufanyiwa tathmini ikiwa ni pamoja na kuandaa mipango halisi ya kuitathmini. Aidha, Baraza lishirikiane na Ofisi ya Makamu wa Rais- Idara ya Usimamizi wa Mazingira na Ofisi ya Rais-TAMISEMI kuhakikisha kuwa kila Halmashauri imeajiri Ofisa mazingira mwenye sifa zinazotakiwa kwa usimamizi wa mazingira ikiwa ni pamoja na kuwa na muundo wao wa ajira.

6.2.6 UKAGUZI WA UFANISI KATIKA UTEKELEZAJI WA MASHARTI YA USHIRIKISHAJI WA WATANZANIA NA UHAKIKI WA UREJESHAJI WA GHARAMA ZA UWEKEZAJI KWENYE MIKATABA YA MGAWANYO WA MAPATO YA UZALISHAJI
Lengo la ukaguzi lilikuwa ni kutathmini iwapo Wizara ya Nishati na Madini na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania zilihakikisha kikamilifu utekelezaji wa masharti ya ushirikishaji wa watanzania kwenye Mikataba ya Mgawanyo wa Mapato ya Uzalishaji kwenye maeneo ya mafunzo, ajira, na manunuzi ya bidhaa na huduma za ndani na uhakiki wa urejeshaji wa gharama za uwekezaji.

Ukaguzi ulibaini yafuatayo:
i) Mfumo wa Kisheria Ulikuwa na Upungufu
Mfumo uliokuwepo wa ushirikishaji wa watanzania nchini ulikuwa dhaifu. Wizara haikuwa na sera ya ushirikishaji wa watanzania na  haikuandaa kanuni kwa ajili ya ushirikishaji wa watanzania. Aidha, Wizara haikuandaa na kutoa miongozo na taratibu zozote kwa ajili ya kutumiwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli katika ufuatiliaji wa utekelezaji wa masharti ya ushirikishaji wa watanzania kwenye mikataba ya mgawanyo wa mapato ya uzalishaji.
Pia, ukaguzi ulibaini kuwa uhakiki wa urejeshaji wa gharama za uwekezaji uliongozwa na Mikataba ya Mgawanyo wa Mapato ya Uzalishaji. Mbali na hili hakukuwa na miongozo mingine yoyote kama vile Sera, Kanuni au Miongozo ambayo ingewezesha kutekeleza uhakiki wa urejeshaji wa gharama za uwekezaji.

ii) Mfumo wa Kitaasisi Ulikuwa na Upungufu
Wizara kama msimamizi wa shughuli za mkondo wa juu haikuwa na kitengo chochote chenye wajibu wa kufuatilia shughuli za Shirika la Maendeleo ya Petroli kwenye utekelezaji wa masharti ya ushirikishaji wa watanzania kwenye Mikataba ya Mgawanyo wa Mapato ya Uzalishaji.
Shirika la Maendeleo ya Petroli halikuwa na kitengo maalumu cha kuhakiki gharama za uwekezaji. Hali hii ilisababisha gharama za uwekezaji kutohakikiwa kwa zaidi ya miaka miwili. Uhakiki wa gharama za uwekezaji unapaswa kufanyika ndani ya miaka miwili tokea gharama zilipoingiwa.

iii) Masharti Yanayohusu Ajira kwa Watanzania Hayakusimamiwa Ipasavyo Ilibainika kwamba Wizara ambayo ni mdhibiti na Shirika la Maendeleo ya Petroli ambalo ni mmiliki wa leseni hawakufanya ufuatiliaji wa shughuli za wakandarasi washiriki ili kuhakikisha kuwa Watanzania wanaajiriwa ipasavyo na wakandarasi washiriki.
Wizara na Shirika hawakuweka utaratibu sahihi wa kusimamia utoaji wa vibali vya kazi kwa wafanyakazi wa kigeni kwenye Sekta ya Mafuta na Gesi. Ilibainika kwamba si makampuni yote ya kimataifa ya mafuta yanapitisha maombi yao ya vibali vya kazi kwa Wizara na Shirika. Aidha, hakuna mkandarasi mshiriki hata mmoja ambaye alipitisha maombi yake ya vibali vya ajira kwa Wizara na Shirika.

iv) Masharti ya Manunuzi ya Bidhaa na Huduma za Kitanzania Hayakutekelezwa Ipasavyo
Shirika halikuandaa taratibu za zabuni zinazoongozwa na sheria za Tanzania. Hii ilisababisha makampuni ya kimataifa ya mafuta kutotangaza zabuni, hivyo kuyanyima fursa makampuni ya Kitanzania kuomba zabuni.

v) Sehemu ya Gharama za Uwekezaji Hazikuhakikiwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli kwa Wakati
Ukaguzi ulibaini kuwa gharama za uwekezaji za kiasi cha Dola za Marekani bilioni 1.5 hazikuhakikiwa na Shirika. Hii ilisababishwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli kutoweka kwenye mipango yake shughuli za uhakiki wa gharama za uwekezaji katika miaka ya nyuma. Kwa sasa, Shirika linakamilisha kuhakiki gharama zilizoingiwa hapo zamani.

vi) Ufuatiliaji na Tathmini ya Ushirikishaji wa Watanzania na Uhakiki wa Urejeshaji wa Gharama za Uwekezaji Haukufanyika
Ukaguzi umebaini kwamba Shirika la Maendeleo ya Petroli halikufanya ufuatiliaji na tathmini ya shughuli za utekelezaji wa ushirikishaji wa watanzania na uhakiki wa urejeshaji wa gharama za uwekezaji. Kadhalika, Wizara haikufanya ufuatiliaji na tathmini ya shughuli hizo kadri zinavyofanywa na Shirika.

Hitimisho la ukaguzi
Hitimisho la ukaguzi huu ni kwamba mfumo wa kisheria una mapungufu kwa kukosa sera, miongozo na taratibu za kuongoza ushirikishwaji wa watanzania. Pia mfumo wa kitaasisi una upungufu kwa kukosa msimamizi wa shughuli za mkondo wa juu.
Mapendekezo
i) Wizara ya Nishati na Madini inapaswa kuandaa miongozo ya kuwezesha utekelezaji wa masharti ya ushirikishaji wa watanzania yaliyomo kwenye Mikataba ya Mgawanyo wa Mapato ya Uzalishaji.
ii) Wizara inapaswa kuharakisha mchakato wa kuandaa sera za uwezeshaji wa watanzania; kuwezesha kuandaliwa  kwa kanuni za uwezeshaji wa watanzania; na kutoa mara kwa mara miongozo ambayo itasimamia utekelezaji wa ushirikishaji wa watanzania kwenye Sekta ya Mafuta na Gesi.
iii) Wizara inatakiwa kuandaa miongozo ya taratibu za matumizi ya fedha za mafunzo kutoka kwa makapuni ya kimataifa ya mafuta ili kuhakikisha fedha zinatumika kuwajengea uwezo wataalamu zaidi katika Sekta ya Mafuta na Gesi.
iv) Wizara, kwa kushirikina na Wizara ya Elimu, inapaswa kuanzisha mfumo wa ufuatiliaji na tathmini kwa ajili ya kufuatilia na kutathmini shughuli za utekelezaji wa masharti ya ushirikishaji wa watanzaniakwenye mikataba ya mgawanyo wa mapato ya uzalishaji na uhakiki wa urejeshaji wa gharama za uwekezaji.
v) Wizara inapaswa kuweka miongozo kwa ajili ya ajira za wataalamu wa kigeni kwenye makampuni ya kimataifa ya mafuta na makandarasi washiriki kwa ajili ya kutengeneza fursa za ajira kwa Watanzania. Ushiriki wa Wizara ya Nishati na Madini kwenye mchakato wa kutoa vibali vya kazi utiliwe mkazo.

6.2.7 MCHAKATO WA TATHMINI YA ATHARI ZA MAZINGIRA KATIKA MIRADI YA MAENDELEO
Sheria ya usimamizi wa mazingira imeainisha aina ya miradi ya maendeleo inayotakiwa kufanyiwa tathmini ikiwa utekelezaji wake utaathiri mazingira. Usimamizi wa tathmini ya athari zinazoweza kutokea katika mazingira ni muhimu katika kulinda mazingira na maslahi ya umma kwa ujumla. Lengo la ukaguzi ni  kutathmini iwapo  Ofisi ya Makamu wa Rais-Kitengo cha Mazingira  na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira walisimamia kikamilifu mchakato wa tathmini ya athari za mazingira kabla ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Ukaguzi ulibaini yafuatayo:
i) Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira haikuweza kutambua miradi yote iliyotakiwa kusajiliwa ili ifanyiwe tathmini.
ii) Vibali mbalimbali vya uendelezaji miradi vilitolewa pasipo kuonesha uthibitisho kuwa Baraza limeridhia;
iii) Kutohusishwa kwa wadau muhimu wakati wa kupitia nyaraka za awali zinazoelezea miradi ilivyo hasa serikali za mitaa ambako miradi husika inatekelezwa;
iv) Mikutano ya kamati ya wataalamu kwa sehemu kubwa ilihusisha maofisa kutoka Baraza bila kuwahusisha maofisa (Wataalamu) kutoka serikali za mitaa naWizara husika za kisekta. Hivyo, mikutano ya kamati ya wataalamu ilikosa maoni ya Wizara, Idara za serikali, na serikali za mitaa;
v) Tathmini za Kimazingira hazikuweza kubaini masuala yenye athari kubwa kwa mazingira kama vile ujenzi wa kituo cha Kuhifadhia Mabasi ya Mradi wa Mabasi Yaendayo Kasi katika eneo la Jangwani Dar es salaam;
vi) Uhaba mkubwa wa maofisa mazingira  katika mamlaka za serikali   za  mitaa; na
vii) Uhaba wa wakaguzi wa mazingira wenye vibali vya kufanya kazi za kikaguzi.

Hitimisho la ukaguzi
Ukaguzi ulihitimisha kwamba Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira na Ofisi ya Makamu wa Rais-Kitengo cha Mazingira hawasimamii ipasavyo mchakato wa tathmini ya athari za mazingira au ukaguzi wa mazingira katika miradi ya maendeleo. Mchakato hauhakikishi kwamba miradi yote ambayo huenda ikawa na athari hasi kwa mazingira haisajiliwi; na kuhakikisha kuwa miradi yote inatathminiwa na hatua zote stahiki za kupunguza athari zinazooneshwa katika taarifa za tathmini ya athari ya mazingirana zinatekelezwa.

Pendekezo
Ninapendekeza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira liweke mfumo madhubuti wa kutambua miradi yote inayotakiwa kufanyiwa tathmini ikiwa ni pamoja na kuandaa mipango halisi ya kuitathmini. Pia, Baraza lishirikiane na Ofisi ya Makamu wa Rais-Kitengo cha Mazingira na Ofisi ya Rais -TAMISEMI kuhakikisha kuwa kila halmashauri imeajiri Ofisa mazingira mwenye sifa zinazotakiwa kwa usimamizi wa mazingira ikiwa ni pamoja na kuwa na muundo wao wa ajira.

6.2.8 UKAGUZI WA UFANISI KATIKA SEKTA YA MAFUTA NA GESI ASILIA
Nimefanya ukaguzi katika maeneo manne katika Sekta ya Mafuta na Gesi nchini na kuona madhaifu kama ifuatavyo:


6.2.8.1 Usimamizi wa Taarifa za Kijiofizikia za Sampuli za Kijiolojia
i) Kutokuwepo kwa sera ya ndani na mifumo inayotoa mwongozo katika usimamizi wa taarifa za kijiofizikia;
ii) Shirika la Maendeleo ya Petroli halijaandaa mfumo unaotoa mwongozo katika usimamizi wa taarifa za kijiofizikia;
iii) Mazingira ya uhifadhi wa taarifa za kijiofizikia yasiyoridhisha. Kituo cha uhifadhi kilichopo makao makuu ya Shirika la Maendeleo ya Petroli kilionekana kuwa na nyufa katika dari zinazotoa mwanya kwa maji ya mvua kuingia na kuathiri sampuli za kijiolojia zilizohifadhiwa.
iv) Kutokuwepo kwa Sera ndani ya Wizara yenye kuhakikisha uadilifu wa taarifa za kijiofizikia.
Kutokuwepo kwa tathmini huru za kazi za mkondo wa juu (upstream) ambazo zingeweza kubainisha upungufu na kutoa tahadhari ili kufanya maboresho.

Hitimisho la ukaguzi
Ukaguzi umehitimisha kwamba taarifa za kijiofizikia zinazohusiana na gesi asilia hazisimamiwi kiufanisi. Hii imetokana na kutokuwepo kwa ufanisi katika udhibiti pamoja na utaratibu usioridhisha kwenye kutathmini upatikanaji, uendelezaji, uhifadhi, ufikiwaji na umiliki wa taarifa hizo.

Pendekezo
Ninapendekeza Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania kuandaa sera ya ndani yenye kutoa mwongozo ili kuleta ufanisi wa usimamizi wa taarifa za kijiofizikia. Hii ni pamoja na kutengeneza mahitaji ya kina ya utaratibu bora wa uhifadhi wa sampuli za kijiofizikia kwa mujibu wa viwango husika.

Aidha, ninapendekeza Wizara ya Nishati na Madini kuanzisha mfumo wa ufuatiliaji na tathmini ambao utaruhusu kujua maendeleo ya usimamizi wa taarifa za kijiofizikia zinazohusiana na gesi asilia kama zinavyotekelezwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli na kutoa kipaumbele kwa shughuli za usimamizi wa taarifa za kijiofizikia kwenye vitengo husika ndani ya wizara.

6.2.8.2 Usimamizi wa Mchakato wa Ugawaji wa Leseni za Utafutaji na Uendelezaji wa Mafuta na Gesi Asilia
Ukaguzi ulibaini yafuatayo;
i) Upungufu katika uchambuzi wa mahitaji kutokana na kukosekana kwa vigezo vinavyokidhi mahitaji ya kijamii kama vile mahitaji ya mazingira, afya na usalama, na mahitaji mengine ya jamii.
ii) Kukosekana kwa mkakati wa manunuzi ambao ungesaidia kuwepo kwa mgao sahihi wa rasilimali zilizopo na utekelezaji sahihi wa shughuli na upimaji mzuri wa utendaji ili kufikia malengo. Ilibainika kuwa Wizara ya Nishati na Madini  na Shirika la Maendeleo ya Petroli hawana mkakati wa manunuzi zaidi ya mipango ya kila mwaka.
iii) Sheria zilizopo zinazohusu shughuli za mafuta na petroli kutokuwa na vifungu vinavyohusu moja kwa moja mchakato wa upatikanaji wa makampuni ya utafiti wa mafuta na gesi unaofanywa na Shirika la Maendeleo ya Petroli.
iv) Kukosekana kwa ripoti inayotoa tathmini ya mchakato wa upatikanaji wa makampuni ya mafuta nchini iliyofanywa na Wizara au Shirika la Maendeleo ya Petroli. Upungufu huu unaisababishia Serikali kutotambua changamoto mbalimbali katika uboreshaji wa mchakato wa upatikanaji wa makampuni husika.

Hitimisho la ukaguzi
Ukaguzi ulihitimisha kwamba Wizara ya Nishati na Madini na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania hawana mfumo mzuri wenye kuzingatia ufanisi, ubora na maadili katika kusimamia mchakato wa utoaji wa mkataba na leseni za utafutaji mafuta na gesi.

Mapendekezo
i) Ninapendekeza Wizara ya Nishati na Madini kuweka sera itakayosimamia tathmini za mara kwa mara za mchakato mzima wa utoaji wa mikataba na leseni za mafuta na gesi ili kutambua fursa za kuongeza thamani ya fedha na kubaini ukiukwaji na manunuzi ya udanganyifu.
ii) Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania linapaswa kuwa na mkakati wa manunuzi katika shughuli ya mafuta na gesi ikiwa ni pamoja na kutekeleza kikamilifu Mfumo wa Usimamizi wa Vihatarishi.

6.2.8.3 Uendelezaji wa Rasilimali-Watu katika Sekta ya Mafuta na Gesi
Ukaguzi ulibaini yafuatayo;
i) Mipango na mikakati ya uendelezaji rasilimali-watu iliyowekwa na wizara ya nishati na madini haijitoshelezi na si endelevu.
ii) Tathmini ya fani zinazohitajika katika sekta ya mafuta na gesi iliyofanywa na Wizara ya Nishati na Madini haikuzingatia fani muhimu zinazohitajika katika shughuli nzima ya mafuta na gesi asilia kama vile wahandisi waendeshaji mitambo.
iii) Mipango na mikakati ya uendelezaji wa rasilimali-watu katika Sekta ya mafuta na gesi haikutekelezwa kama ilivyopangwa.
iv) Wizara ya Nishati na Madini haina mpango wa ufuatiliaji, tathmini, na utoaji taarifa za utendaji wa uendelezaji rasilimali-watu katika Sekta ya Mafuta na Gesi asilia nchini.

Hitimisho la ukaguzi
Ukaguzi ulihitimisha kwamba mipango na mikakati ya uendelezaji rasilimali-watu haiwezeshi upatikanaji endelevu wa rasilimali-watu katika sekta ya mafuta na gesi asilia nchini hivyo kupelekea Wizara kushindwa kufikia malengo ya kutoa fursa za ajira na pia kuboresha uwezo wa kiufundi na kitaalamu.

Pendekezo
Ninapendekeza Wizara ya Nishati na Madini kwa ushirikiano na wadau itathmini kwa kina fani zinazohitajika ambazo zitasadifu mahitaji halisi ya uendelezaji wa rasilimaliwatu katika Taasisi za Serikali na Sekta kwa ujumla. Hii ni pamoja na kuandaa na kutekeleza mipango na mikakati madhubuti ya uendelezaji wa rasilimaliwatu itakayohusisha fani zote zinazohitajika katika kila hatua ya uzalishaji wa mafuta na gesi asilia nchini.

6.2.8.4 Usimamizi wa Uzingatiaji na Utekelezaji wa Sera, Sheria na Kanuni za Mazingira katika Shughuli za Utafutaji wa Petroli
Ukaguzi ulibaini yafuatayo;
i) Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira halijatengeneza mpango kazi wa ukaguzi unaozingatia vihatarishi utakaotumika kufanya kaguzi katika shughuli ya utafutaji petrol nchini;

ii) Kwa kipindi cha ukaguzi huu, Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa  Mazingira lilifanya kaguzi kwenye miradi 3 tukati ya miradi 71 iliyosajiliwa ili kuangalia iwapo makampuni ya utafutaji wa petroli yanafuata matakwa ya sheria za mazingira;

iii) Baraza kutowasilishataarifa za utendaji kwa Ofisi ya Makamu wa Rais – Idara ya Mazingira za hali ya utekelezaji wa mfumo wa udhibiti wa mazingira katika shughuli nzima ya utafutaji mafuta nchini;

iv) Ushirikishaji duni kati ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira, Ofisi ya Makamu wa Rais, Wizara ya Nishati na Madini, na Serikali za Mitaa;

v) Upungufu katika kupeana taarifa zinazohusu mazingira na kutokuwepo kwa muundo unaoeleweka wa kupeana taarifa baina yao.

Hitimisho la ukaguzi
Ukaguzi ulihitimisha kwamba Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira halijaweza kusimamia ipasavyo ufuatiliaji na utekelezaji wa sheria ya mazingira katika miundombinu ya utafutaji wa petroli, japokuwa ndio wakala anayehusika katika kusimamia utekelezaji wa sheria ya mazingira hapa nchini.


Pendekezo
Ninapendekeza kuanzishwa kwa mifumo ya kuhakikisha kaguzi za mazingira zinafanyika mara kwa mara na kwa muda muafaka kuliko kusubiri mpaka yatokee malalamiko. Aidha, ripoti ya jumla ya hali ya mazingira kwenye Sekta ya petroli nchini iwe inaandaliwa kila mwaka ili iwezeshe kufanyika kwa tathmini.


Mwisho
Ndugu wanahabari, huu ni muhtasari tu wa yaliyomo katika ripoti zilizowasilishwa leo Bungeni. Ni matumaini yangu kuwa, mtazisoma ipasavyo taarifa hizi ili muweze kupata maelezo ya kina yatakayowawezesha kupeleka ujumbe ulio sahihi kwa Umma wa watanzania. Aidha, pale ambapo mtahitaji kupata ufafanuzi Ofisi yangu itakuwa tayari kutoa ushirikiano.

Nakala ya ripoti hizo mtapewa na pia zinapatikana kwenye tovuti ya Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi (www.nao.go.tz).

Nawashukuru kwa kunisikiliza.Prof. Mussa Juma Assad
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali,
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
0

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

HIVI NDIVYO BIASHARA YA NGONO NAMNA INAVYOTIKISA MOROGORO: SEHEMU YA PILI.

DC MJEMA AONJA ADHA YA MAFURIKO AKIKAGUA ATHARI ZA MAFURIKO ILALA

DC MKURANGA AZINDUA MRADI WA MASHAMBA MJI YA NAMAINGO MSOLWA

ANGALIA PICHA NDEGE KUBWA YA ABIRIA DUNIANI ILIYOANZA SAFARI NDEFU ZAIDI!

TGGA WAMUAGA BOSS WA GIRL GUIDES AFRIKA KWA HAFLA KABAMBE

WAPENZI WANASANA WAKIFANYA MAPENZI GESTI

IJUE HISTORIA YA UHASIMU WA KOREA KASKAZINI NA MAREKANI

Wasafi TV kuanza kurusha matangazo yake leo (+video)

WAGGGS AFRIKA WAIPONGEZA TGGA KWA KUONGOZA AFRIKA KUSAJILI GIRL GUIDES WENGI