WAJANJA WAANZA KUJIMEGEA UWANJA WA NDEGE WA ZAMANI MBEYA



Muonekano wa Ofisi za Uwanja wa  ndege wa Zamani wa Mbeya unaodaiwa kuvamiwa

Mwenyekiti wa Mtaa wa Airport,  Enock Mwampagama akifafanua jambo  kwa waandishi wa habari(hawapo pichani) kuhusu uvamizi wa Uwanja wa ndege

Baadhi ya Waandishi wa habari wakipata maelezo kutoka kwa Mwenyekiti wa Mtaa wa Airport

Baadhi ya Waandishi wakiangalia mawe (bikons) zilizowekwa katika mashamba ambayo wananchi wamepimiwa ndani ya Uwanja wa Ndege

Moja ya Jiwe likionesha kiwanja kilichopimwa

Wanafunzi wa Shule ya Msingi Pambogo wakicheza kwenye uwanja wa Ndege ambapo wanalia kukosa eneo la kuchezea licha ya watu kugawana maeneo

Njia ya kurukia ndege ambayo sasa imegeuka uwanja wa kujifunzia kuendeshea magari
 
MUDA mfupi kupita baada ya Serikali kujenga na kuzindua Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Songwe uliopo Wilaya ya Mbeya Mkoani Hapa, Baadhi ya Wananchi wameanza kujipimia na kugawana uliokuwa Uwanja wa ndege wa zamani uliopo Iyela jijini Mbeya kwa matumizi binafsi.
 
 
Idadi ya viwanja vinavyodaiwa kuuzwa ni kati ya 60 hadi 70 ambapo jopo la wanahabari wa Chama Cha Waandishi wa Habari za Utalii na Uwekezaji Tanzania  (TAJATI) walitembelea na kukuta mawe yaliyopimwa kwa ajili ya kuwagawia wananchi.
 
 
Imeelezwa kuwa viwanja hivyo vyenye thamani ya kuanzia sh mil 20 hadi sh mil 50 kila kimoja vimegawiwa kwa wananchi huku ikielezwa kuwa mmoja wa wakazi wa eneo hilo aliyefahamika kwa jina la Mwanguku kuwa ndiye anayemiliki eneo hilo kabla ya kuanzishwa kwa uwanja huo zaidi ya miaka 50 iliyopita.
 
 
Uwanja huo wenye urefu unaokadiriwa km 2.7 uliopo Iyela jijini Mbeya umedaiwa kuuzwa kwa wananchi wa eneo hilo huku kukiwa na madai kuwa baadhi ya Watumishi wa Halmsahauri ya Jiji la Mbeya wanahusika na uuzwaji wa eneo la uwanja huo.
 
 
 
Akizungumza na waandishi wa habari kutoka TAJATI, Mwenyekiti wa Mtaa wa Airport,  Enock Mwampagama alikiri kuona uwanja huo umevamiwa huku kukiwa na baadhi ya viwanja vilivyopimwa na baadhi ya watu wakiendelea kulima eneo hilo.
 
 
Naye Mwenyekiti wa mtaa wa Pambogo ambako uwanja huo umepakana na mtaa huo Esia Edward, alisema  mara baada ya kuona eneo hilo linavamiwa alitoa taarifa ya uvamizi huo serikalini ambako hakupata mrejesho juu ya uvamizi huo.
 
Mwenyekiti wa mtaa wa Block T Adrian Majembe, alisema ameona uvamizi mkubwa ukiendelea eneo hilo na kuwa hata hivyo yeye kama Mwenyekiti wa mtaa unaopakana na uwanja huo hakushirikishwa kwa lolote na kuwa amesikia eneo hilo la viwanja lilikuwa ni la familia ya mtu aliyetambulika kwa jina la Mwanguku ambaye inadaiwa eneo hilo ni mali ya familia hiyo.
 
 
Alisema wakazi wa eneo hilo walidai kuwa eneo hilo wamegaiwa na Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi alipokuja Jijini Mbeya.
 
 
Alisema hata yeye alisikia watu wakisema wananchi wamegawiwa viwanja na wameruhusiwa kujenga eneo hilo na Waziri Lukuvi, Majembe ambaye aliwahi kuwa  Meya wa Manispaa ya Mbeya kati ya mwaka 1994-2000.
 
 
Kwa upande wake Ofisa Mtendaji wa Kata ya Iyela Henry Shipela alisema mara alipopata taarifa za uvamizi wa eneo hilo alifuatilia na kukuta watu wakiwa wanalima na kuwa baada ya kuulizia baadhi ya watu akaambiwa kuwa ni familia ya watumishi wa uwanja wa ndege na kuwa hata hivyo atafuatilia kujua sababu zaidi juu ya uvamizi wa uwanja huo.
 
 
Akizungumzia suala la uvamizi wa uwanja huo Meneja wa Uwanja wa Kimataifa wa Songwe, Hamis Amir, alisema amesikia suala la uvamizi wa uwanja ndege wa Iyela ambao ulikuwa ukitumika awali kabla ya kuanzishwa kwa uwanja wa Songwe mwaka 2012 lakini hata hivyo hajui vyema mipaka ya uwanja huo.
 
 
Mmoja wa maofisa wa Halmashauri ya Jiji anayeelezwa alihusika katika upimaji huo aliyetambulika kwa jina la Ben Mponzi alisema kuwa uwanja huo ulipimwa na Ofisa Mpima Ardhi wa Jiji la Mbeya Athuman Maugo ambaye naye alidai kuwa eneo hilo lilipimwa kwa idhini ya serikali na si Halmashauri ya Jiji la Mbeya.
 
 
Kwa upande wake  Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya Dkt Samwel Lazaro, alisema  Halmashauri ya Jiji la Mbeya haihusiki na jambo lolote kuhusu uwanja wa ndege wa Airport.
 
 
Awali Katibu Tawala Mkoa wa Mbeya, Mariam Mtunguja alisema Serikali ya Mkoa imeandika barua serikali kuu ili kuomba kibali cha kubadili matumizi ya uwanja huo ikiwa ni kutumia katika sekta ya uwekezaji.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*