KUZINGATIA TARATIBU ZA NCHI HIYO KATIKA MAOMBI YA VIZA.


indexNa Benedict Liwenga, MAELEZO, Dodoma.
 
WATANZANIA ambao wanapenda kutembelea nchi ya Uingereza wametakiwa kuzingatia taratibu zilizowekwa na nchi hiyo katika maombi ya viza ikiwemo kuomba viza mapema, kuwasilisha nyaraka zote muhimu pamoja na taarifa sahihi ili kuepuka usumbufu usio wa lazima.
 
Ushauri huo umetolewa leo Bungeni Dodoma na Naibu Waziri, Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mhe. William Ole Nasha ambaye alijibu swali kwa niaba ya Waziri mwenye dhamana katika Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga lililotaka kujua ni sababu zipi zinazoifanya Serikali ya Tanzania iridhike na utaratibu unaoleta usumbufu kwa Watanzania wanaotaka kusafiri kwenda Uingereza kutafuta viza kupitia Kenya na Afrika Kusini.
Mhe. Ole Nasha ameeleza kuwa, hapo awali huduma za viza zilikuwa zikitolewa na Ubalozi wa Uingereza nchini, Ubalozi huo ulihamisha shughuli za utoaji wa viza kutoka hapa nchini kwenda nchini Kenya tarehe 1 Desemba, 2008 na kuanzia tarehe 18 Agosti, 2014 huduma hizo zimehamishiwa nchini Afrika Kusini na siyo Kenya tena.
Alifafanua kuwa, kwa mujibu wa Serikali ya Uingereza uamuzi huo ni wa kisera ba umefikiwa ili kuleta ufanisi katika utendaji kazi wa Idara ya Viza na Masuala ya Uhamiaji ya Uingereza.
“Mchakato wa utoaji viza za Uingereza unafanyika Kikanda, kwa mantiki hiyo maombi yote ya viza kutoka nchi zote za Afrika Mashariki na Kati yanafanyiwa kazi katika Ubalozi wa Uingereza nchini Afrika Kusini”, alisema Ole Nasha.
Aidha, Waombaji wa viza hapa nchini wanatakiwa kuwasilisha maombi yao pamoja na nyaraka zinazohitajika katika Kituo cha Kuombea Viza (Visa Application Centre) kilichopo Viva Tower, Dar es Salaam.
“Kituo hicho ndicho chenye jukumu la kusafirisha maombi hayo kwenda Afrika Kusini na kurejesha nyaraka husika kwa waombaji nchini, Mwombaji halazimiki kufuata huduma hiyo nchini Afrika Kusini”, alisema Mhe. Ole Nasha.
Amefafanua kuwa, Ubalozi wa Uingereza Nairobi unashughulikia maombi machache ya viza (restricted number of applications) kwa Viongozi wa Serikali na watendaji wengine wenye pasi za Kidiplomasia hasa katika hali ya dharura ambapo maombi hayo yanapaswa kupelekwa moja kwa moja Ubalozi wa Uingereza Nairobi na waombaji wenyewe au kupitia Ubalozi wa Tanzania Nairobi.
“Napenda kuwakumbusha Waheshimiwa Wabunge pamoja na Watanzania wenzangu kwamba. Zoezi la utoaji viza lina utaratibu Wake na moja ya taratibu hizo ni kwamba nchi inayotoa Viza Ina Uluru wa kuamua ni wapi itatolea viza hizo, kwa mantiki hiyo hata Serikali yetu ya Tanzania ku pitia Balozi zake zilizopo nje inazo taratibu zake za kutoa viza kwa wageni wote wanaotembelea Tanzania, ni vema Watanzania ambro wangependa kutembelea nchi ya Uingereza wakazingatia taratibu zilizowekwa na nchi hiyo katika maombi ya viza”, alisisitiza Ole Nasha.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

ALLY KAMWE AZIMIA KWA MKAPA.

RAIS SAMIA KUZINDUA MKUTANO MKUU WA 79 WA BARAZA LA MICHEZO YA MAJESHI DUNIANI

MIGINGO KISIWA KIDOGO ZAIDI AFRIKA KILICHOGOMBEWA NA UGANDA, KENYA