SERIKALI YAFAFANUA KUHUSU NDEGE NDOGO ZINAZOENDESHWA NA RUBANI MMOJA.



Na Benedict Liwenga, MAELEZO, Dodoma.

SERIKALI imesema kuwa, hakuna kiwango kinachobainisha wazi kuwa ndege yenye uwezo wa kubeba abiria kumi au zaidi ni sharti iendeshwe na marubani wawili.

Kauli hiyo imetolewa leo Bungeni mjini Dodoma na Naibu Waziri. Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Eng. Edwin Ngonyani wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Tambwe, Mhe. Khalifa Issa aliyetaka kujua kuhusu Sheria za nchi na za Kimataifa zisemavyo kuhusu ndege za namna hiyo kurushwa na rubani mmoja.

Eng. Ngonyani amesema kwamba, taratibu zinazoongoza fani ya kuendesha ndege nchini huongozwa na miongozo inayokubalika Kimataifa na ambayo imeridhiwa hapa nchini na Bunge.

Amefafanua kuwa, Katika taratibu hizo, kuna matakwa ya kisheria na kiufundi ambayo yakifuatwa yanawezesha kuwa na uwezekano mdogo sana wa kukumbwa na athari ya kiafya na kushindwa kumudu kuendesha ndege.

Ameeleza kuwa, Marubani hupimwa afya zao na madaktari bingwa kila muda maalum kulingana na umri kama ilivyoainishwa katika Kanuni ya 140 mpaka 177 ya The Civil Aviation (Personnel Licensing) Regulations, 2012.

"Serikali inaruhusu ndege kuendeshwa na rubani mmoja kwa kuzingatia taratibu hizo, Aidha, Kanuni 32(5) inasema kwamba ndege iliyoandikishwa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuruka kwa shughuli za kibiashara yenye uzito unaozidi kilo 5,700 itakuwa na marubani wasiopungua wawili", alisema Eng. Ngonyani.

Pia amefafanua kuwa, shughuli za Usalama wa Anga nchini zinaongozwa na Sheria Namba 80 "Cvil Aviation Act. 80" na Kanuni zilizotengenezwa chini yake, ambapo urushaji wa ndege yenye abiria tisa au zaidi unaongozwa na Kanuni ziitwazo "The Civil Aviation (Operation of Aircraft) Regulations, 2012" ambapo ndege inayotimiza vigezo vilivyowekwa kwenye vifungu (2), (3) na (4) vya Kanuni ya 32 kuwa na uzito wa chini ya kilo 5,700 inaruhusu kuendeshwa na rubani mmoja.

Ameongeza kuwa, katika viwango vinavyotolewa na Shirika la Kimataiaf la Usafiri wa Anga (ICAO) kwenye kiambatanisho namba 19, chini ya Mkataba wa Kimataifa wa Usafiri wa Anga (Chicago Convention) hakuna kiwango chochote kinachobainisha wazi kuwa ndege yenye uwezo wa kubeba abiria 10 au zaidi ni sharti iendeshwe na marubani wawili.

"Pia hakuna hata mapendekezo ya kiutekelezaji kwenye suala hilo, na hata katika Kiambatanisho cha 6 chenye sehemu tatu kianchohusiana na uendeshaji wa ndege ambacho ndicho kinachozungumzia idadi ya marubani katika uendeshaji wa ndege hakina katazo hilo", alisisitiza Eng. Ngonyani.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DKT NCHIMBI ASHIRIKI MAZISHI YA ASKOFU.GACHUMA WA KANISA LA NLGCC

π™‚π˜Όπ™ˆπ™Šπ™‰π˜Ώπ™„ π™†π˜Όπ˜Ύπ™ƒπ™€π™•π˜Ό π™†π™„π˜½π™„π™‰π™‚π™’π˜Ό.