MAGHEMBE AIOMBA JUMUIYA YA KIMATAIFA KUUNGA MKONO MAPAMBANO DHIDI YA MAJANGILI


Waziri wa Maliasili Prof. Jumanne Maghembe (wa tatu kulia) akipokea
ndege maalum aina ya drones kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Kimataifa wa Mfuko wa
Uhifadhi Wanyamapori na Mazingira Duniani (WWF) Dkt. Marco Lambertini (wa tatu
kushoto) kwa ajili ya kusaidia doria za kiitelijensia za kupambana na ujangili
katika pori la akiba la Selous. Wengine
katika picha ni kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa WWF – Tanzania, Amani Ngusaru, Meneja
wa Pori hilo la Akiba  Selous,  Mabula Misungwi, Mwenyekiti wa bodi ya
WWF – Ujerumani, Dkt. Valentin Von Moscow, Mkurugenzi Mtendaji WWF – Ujerumani,
Ebenhard Brandes na Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Kuzuwia Ujangili, Faustine
Ilobi Masalu.
 
Waziri wa Maliasili na Utalii Prof. Jumanne Maghembe (wa tatu kushoto), Viongozi
wa Mfuko wa Uhifadhi Wanyamapori na Mazingira Duniani (WWF) na Viongozi wengine
wa Wizara wakipokea maelekezo kutoka kwa Mtaalam wa uendeshaji wa ndege maalum
aina ya drones na jinsi zinavyofanya kazi, Parmena Elisa, ndege hizo zilitolewa na Mfuko
wa WWF kusaidia doria za kiitelijensia za kupambana na ujangili katika pori la
akiba la Selous jana tarehe 1 Julai, 2016 Matambwe Selous.
Waziri wa Maliasili Prof. Jumanne Maghembe akizungumza katika hafla ya
makabidhiano ya ndege maalum aina ya drones zilizotolewa na Mfuko wa WWF kusaidia
doria za kiitelijensia za kupambana na ujangili katika pori la akiba la Selous. Wengine katika picha ni Mkurugenzi
Mkuu wa Kimataifa wa Mfuko wa Uhifadhi Wanyamapori na Mazingira Duniani (WWF)
Dkt. Marco Lambertini (katikati) na Mkurugenzi Mtendaji WWF – Ujerumani,
Ebenhard Brandes (kushoto).
 
Mkurugenzi Mkuu wa Kimataifa wa Mfuko wa Uhifadhi Wanyamapori na
Mazingira Duniani (WWF) Dkt. Marco Lambertini (wa pili kushoto) akimkabidhi, Namsifu
Johannes Marwa (Mhifadhi Wanyamapori), Tuzo ya WWF ya Mhifadhi Bora kwa mchango
wake alioutoa katika kupambana na ujangili katika pori la akiba la Selous. Wanaoshuhudia
ni Waziri wa Maliasili, Prof. Jumanne Maghembe (wa tatu kushoto), Mkurugenzi
Mtendaji WWF – Ujerumani, Ebenhard Brandes na Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya
Kuzuwia Ujangili Wizara ya Maliasili, Faustine Ilobi Masalu (wa nne kushoto),
tuzo hiyo ilitolewa Matambwe Selous tarehe 1 Julai, 2016.
 
Picha ya pamoja.

………………………………………………………………………………………..
 
WAZIRI wa Maliasili na Utalii Prof.
Jumanne Maghembe ameiomba Jumuiya  ya Kimataifa kuunga mkono juhudi za
Serikali katika kupiga vita ujangili kwa vitendo katika kuimarisha uhifadhi
nchini.
Prof. Maghembe alisema hayo jana, Matambwe Selous, katika hafla fupi
ya makabidhiano ya ndege maalum 8 zilizotolewa Mfuko wa Uhifadhi Wanyamapori na
Mazingira Duniani (WWF) kwa Wizara ya Maliasili na Utalii.
Ndege hizo ndogo aina ya drones ambazo hazitumii rubani na huongozwa na mitambo
maalum zitatumika katika pori la akiba la Selous kwa ajili ya kuimarisha ulinzi
wa Wanyamapori kwa kukusanya taarifa za kiitelijensia zitakazosaidia kukamatwa
majangili. Ndege hizo zina thamani ya dola za kimarekani 80,000 sawa na zaidi
ya Tsh  milioni  172.
“Msaada huu umekuja wakati muafaka ambapo Pori la Akiba la Selous linahitaji teknolojia
za kisasa katika kuimarisha mapambano dhidi ya ujangili ndani na kuzunguka
hifadhi hii” alisema Prof. Maghembe.
Alieleza kuwa changamoto kubwa inayoikabidili hifadhi ya Selous ni ujangili ambao kwa
kiasi kikubwa umesababisha idadi ya Wanyamapori hususani tembo kupungua kwa kasi
kubwa ukilinganisha na miaka ya nyuma.
 
Alisema kuwa takwimu zinaonesha kuwa mwaka 1986 idadi ya tembo katika pori hilo ilikuwa
50,000, idadi ambayo iliongezeka mwaka 2003 na kufikia 70,000 baada ya
Serikali ya Ujerumani kusaidia kuanzishwa kwa Mpango wa Kuendeleza Selous
(Selous Conservation Program) na Serikali ya Tanzania kukubali aslimia 50 ya
makusanyo yanayotokana na utalii yabaki kuendeleza uhifadhi katika pori hilo.
 
Alisema kuwa baada ya mradi huo kuisha na mfumo wa “retention” kuondolewa na Serikali
hali ilibadilika na kuwa mbaya zaidi ambapo kati ya mwaka 2008 na 2011 vitendo
vya ujangili viliongezeka maradufu, sensa ya mwaka 2013 ilionesha idadi ya
tembo hao kupungua hadi kufikia 13,000.
Prof. Maghembe aliongeza kuwa pamoja na hayo Serikali imejipanga kuhakikisha
Wanyamapori wanalindwa usiku na mchana na kwamba wale wote wanaojihusisha na
vitendo vya ujangili watakamatwa na kufikishwa mahamani ili sheria ichukue
mkondo wake.
“Hatutawavumilia hawa watu wamalize wanyamapori wetu wote tulionao, tunawafuatilia usiku na
mchana na lazima tutawakamata” alisisitiza Prof. Maghembe
Aliongeza kuwa Serikali kwa kushirikiana na washirika wa uhifadhi imechukua hatua za
makusudi za kukabiliana na tatizo hilo ikiwemo kuanzishwa kwa mpango wa Kitaifa
wa Kukabiliana na Ujangili na Biashara Haramu ya Wanyamapori, mpango ambao
umekuwa na matokeo mazuri baada ya kuungwa mkono na washirika hao kwa kusaidia
fedha, vifaa na misaada mbalimbali ya kiufundi.
Aliongeza kuwa sehemu ya mpango wa Serikali wa kukabiliana tatizo hilo ni kuanzishwa kwa
Jeshi Usu (Paramilitary) ambapo maeneo yote ya hifadhi nchini yatalindwa
kijeshi. 
 
Prof. Maghembe ameeleza kuwa pamoja na mambo mengine ili kukomesha ujangili ni lazima
mataifa yaliyoendelea ambayo ndiko yaliko masoko makubwa ya meno ya tembo na
bidhaa zake kusitisha kabisa uingizwaji wa meno hayo katika nchi zao ili
kukomesha biashara hii haramu.
 
“Kuna nchi ambazo tayari zimechukua hatua ya kukataza kabisa uingizwaji wa meno ya
tembo nchini mwao, mfano Marekani, tunaiomba sana jumuiya ya kimataifa wakiwemo
marafiki zetu China na nchi nyingine wakatae kabisa uingizwaji wa meno haya
nchini mwao, hii itasaidia sana kukomesha biashara hii haramu” Alisema.
 
Katika hatua nyingine Prof. Maghembe aliwataka wafugaji walioingiza mifugo katika
maeneo yote ya hifadhi nchini waondoe mifugo yao kwa hiari kabla ya
kushinikizwa kufanya hivyo na Serikali kwa mujibu wa sheria.
 
Sheria ya Wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009 Ibara ya 18 (2) inasema “Si ruhusa mtu yeyote
kuingia na kulisha mifugo ndani ya Mapori ya Akiba, Mapori Tengefu na Ardhioevu”
 
Prof. Maghembe alisema kuwa “mtandao wa ujangili unaanzia na watu wanaoingiza mifugo
ndani ya hifadhi, hivyo ni lazima sheria zifuatwe  na waondoke mara moja,
watakaokaidi sheria itafuata mkondo wake na mifugo itakayokamatwa itataifishwa
na Serikali kwa mujibu wa sheria za nchi, sheria hizi hazina tofauti na sheria
zinazokataza watu wasijenge mabondeni au kwenye hifadhi za barabara”  
 
Awali akitoa taarifa, Meneja wa Pori hilo la Akiba la Selous  Mabula Misungwi alieleza baadhi ya changamoto kuu zinazoikabili hifadhi hiyo kuwa ni pamoja na ujangili, miundombinu mibovu ya barabara kwa ajili ya doria na vifaa ikiwemo magari ya doria na nyumba za watumishi.
 
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Kimataifa
wa Mfuko wa Uhifadhi Wanyamapori na Mazingira Duniani (WWF) Dkt. Marco
Lambertini alisema kuwa ili kuimarisha Uhifadhi nchini ni lazima wananchi
waishi karibu na maeneo hayo na pia washirikishwe juu ya umuhimu wake ili wasaidie
kuyalinda kwa faida yao na taifa kwa ujumla.
(Na Hamza Temba – Wizara ya Maliasili na Utalii # www.wizarayamaliasilinautalii.blogspot.com)

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DKT NCHIMBI ASHIRIKI MAZISHI YA ASKOFU.GACHUMA WA KANISA LA NLGCC

π™‚π˜Όπ™ˆπ™Šπ™‰π˜Ώπ™„ π™†π˜Όπ˜Ύπ™ƒπ™€π™•π˜Ό π™†π™„π˜½π™„π™‰π™‚π™’π˜Ό.