RAIS DKT. MAGUFULI AWAAPISHA WAKUU WA MIKOA WATATU IKULU JIJINI DAR ES SALAAM.



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha Dkt. Binilith Satano Mahenge kuwa mkuu wa mkoa wa Ruvuma Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha Dkt. Charles Mlingwa kuwa mkuu wa mkoa wa Mara Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha Zainab Telack kuwa mkuu wa mkoa wa Shinyanga Ikulu jijini Dar es Salaam.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Wakuu wapya wa Wilaya mara baada ya kuwaapisha wakuu wapya watatu wa Mkoa Ikulu jijini Dar es Salaam. Wengine katika picha ni Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan watatu kutoka kushoto, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa watatu kutoka kulia na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi wakwanza kushoto. 


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na Wakuu wa mikoa pamoja na Wakuu wa Wilaya wateule mara baada ya kumaliza kuwaapisha wakuu wa mikoa ya Shinyanga, Mara na Ruvuma Ikulu jijini Dar es Salaam.
. Baadhi ya Wakuu wa Wilaya wateule wakila kiapo cha uadilifu Ikulu jijini Dar es Salaam. PICHA NA IKULU.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 29 Juni, 2016 amewaapisha wakuu wa Mikoa watatu aliowateua Jumapili iliyopita tarehe 26 Juni, 2016.

Wakuu wa Mikoa walioapishwa leo Ikulu Jijini Dar es salaam ni Dkt. Binilith Satano Mahenge ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Dkt. Charles Ogesa Mlingwa ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Mara na Bi. Zainab Rajab Telack ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.

Hafla ya kuapishwa kwa wakuu hao wa Mikoa imehudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama na wakuu wa wilaya wateule ambao waliteuliwa na Rais Magufuli Jumapili iliyopita tarehe 26 Juni, 2016.

Aidha, miongoni mwa wakuu wa wilaya 139 walioteuliwa, Rais Dkt. John Pombe Magufuli amefanya mabadiliko madogo katika wilaya tatu ambapo ametengua uteuzi wa Mkuu wa Wilaya ya Rombo Mteule Mhe. Fatma Hassan Toufiq na badala yake amemteua Bi. Agness Elias Hokororo kuwa Mkuu wa Wilaya hiyo, ametengua uteuzi wa Mkuu wa wilaya ya Serengeti Mteule Bw. Emile Yotham Ntakamulenga na badala yake amemteua Bw. Nurdin Hassan Babu kuwa Mkuu wa Wilaya hiyo na ametengua uteuzi wa Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mteule Bw. Fikiri Avias Said na badala yake amemteua Bw. Miraji Mtaturu kuwa Mkuu wa wilaya hiyo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewataka wakuu wa wilaya wateule kwenda kuchapa kazi na kutatua kero za wananchi katika wilaya zao huku wakizingatia kufanya kazi kwa uadilifu na uaminifu.

Rais Magufuli pia amewataka kusimamia ukusanyaji mapato ya serikali na matumizi ya fedha na rasilimali nyingine za umma, kuhakikisha wananchi wapo salama na pia kuhakikisha wananchi wanafanya kazi za uzalishaji mali.

"Katika kazi hizi wapo watakaowakejeli, katika kazi hizi wapo watakaowadhihaki, nyinyi kavumilieni na mmuweke Mungu mbele na mkawaweke watanzania mbele, mkafanye kazi kadiri Mungu atakavyokuwa amewaongoza.

"Nataka kuwahakikishia tunawaunga mkono kwa nguvu zote, mkafanye kazi bila uwoga wowote, katembeeni kifua mbele, kwa sababu tumewaamini wala msiwe na wasiwasi, ukifanya kitu kizuri kwa dhamira yako iliyo njema kitazaa matunda mazuri, ukifanya kitu kwa unafiki hakitafanikiwa" Amesema Rais Magufuli

Katika hafla hiyo, wakuu wa mikoa walioapishwa na wakuu wa wilaya wateule wamekula kiapo cha ahadi ya uadilifu kwa viongozi wa umma, zoezi ambalo limeongozwa na Kamishna wa Maadili Jaji Mstaafu Salome Kaganda.

Katika hatua nyingine, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amekutana na kufanya Mazungumzo na mwenyekiti mwenza wa taasisi ya Bill and Melinda Gates ya Marekani Bi. Melinda Gates ambapo Rais Magufuli amemuhakikishia mwenyekiti mwenza huyo kuwa serikali ya awamu ya tano itaendeleza na kuimarisha zaidi uhusiano wake na taasisi hiyo ambayo imekuwa ikishirikiana na Tanzania katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Afya, Uongozi na Kilimo.

Kwa upande wake Bi. Melinda Gate amempongeza Rais Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya katika kukabiliana na rushwa na kuongeza ukusanyaji wa mapato ya serikali, na pia kwa nia yake thabiti ya kuinua sekta ya kilimo inayotegemewa na idadi kubwa ya watanzania na ameahidi kuwa taasisi ya Bill and Melinda Gates itaendelea kushirikiana na Serikali ya awamu ya tano katika kuongeza tija ya uzalishaji wa mazao ya kilimo.


Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
29 Juni, 2016 .

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*