WANAOPOKEA
RUSHWA KUFUKUZWA KWENYE MIZANI
Serikali imesema itachuku
hatua kali ikiwemo kumfukiza kazi na
kumfikisha mahakamani mfanyakazi wa
Mizani atakayebainika anajihusisha na vitendo vya kupokea rushwa ili kuruhusu
magari kupita bila kupimwa uzito.
Kauli hiyo imetolewa
na Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi),
Eng. Joseph Nyamhanga wakati alipokagua huduma za upimaji uzito wa Magari
katika Mzani wa Njuki Mkoani Singida.
Amesema hadi sasa kuna
baadhi ya wafanyakazi wa Mizani wameachishwa kazi kutokana na kujihusisha na
vitendo vya kupokea rushwa kutoka kwa madereva wa magari ya Mizigo na abiria.
“Hatutasita kuchukua
hatua kwa mfanyakazi yeyote atakayejihusisha na vitendo vya rushwa, hatua kali
tutachukua dhidi yake ikiwemmo kumfikisha mahakamani”. Amesema Eng. Nyamhanga.
Badala yake Eng.
Nyamhanga amewataka wafanyakazi wote wa Mizani nchini kufanya kazi kwa uadilifu
kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za uendeshaji wa Mizani ili kuweza
kuleta ufanisi katika vituo vya kazi.
Pia amewataka madereva
wa magari na abiria nchini kushirikiana na Wizara hiyo kwa kutoa taarifa za
Wafanyakazi wa Mizani wanaowaomba rushwa ili kuweza kuondoa kero hiyo kwa wananchi
wanaotumia hudum za Mizani nchini.
Vilelevile amewaasa madereva
wa magari ya mizigo kutozidisha uzito wa mizigo kwenye magari ili kuepusha
uharibifu wa barabara ambazo hujengwa kwa kutumia kodi za wananchi.
“Madereva mnawajibu wa
kulinda barabara hizi kwa kutozidisha uzito wa mizigo kwenye magari yenu ili
kuziwezesha barabara zetu zidumu kwa muda mrefu”. Amesisitiza Eng. Nyamhanga.
Aidha, Eng. Nyamhanga
amesema Wafanyabiashara na madereva wa magari makubwa ya mizigo yaendayo nje ya
nchi kuchangamkia fursa ya kuwapo kwa stika maalum za magari hayo kwani
kutapunguza idadi ya vizuizi vya upimaji
wa uzito na hivyo kuharakisha safari zao.
Naye Msimizi wa Mzani
wa Njuki Mnanka Chile amewaomba madereva wa magari kuzingatia sheria na kanuni
za alama za barabarabi na kuwa makini pindi wanapokaribia seheme za Mizani ya kupimia
uzito wa Magari.
Katibu Mkuu Eng. Josph
Nyamhanga yupo katika ziara ya kukagua Miradi ya Ujenzi wa barabara kwa kiwango
cha lami, Vivuko na huduma za Mizani katika Mikoa ya Dodoma, Manyara Singida na
Mara.
Imetolewa na kitenga
cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.