MWIJAGE:KUPITISHA ENEO LA MKIU KUWA LA VIWANDA


imagesNa Mwamvua Mwinyi,Mkuranga
WAZIRI wa viwanda ,biashara na uwekezaji Charles Mwijage amesema atahakikisha anakaa na bodi yake ya EPZA ili kupitisha eneo la Mkiu jimbo la Mkuranga kuwa eneo la viwanda.
Amesema eneo hilo ambalo lina ukubwa wa hekari 600 litawezesha kuongeza viwanda vingi vitakavyozalisha bidhaa mbalimbali na kuongeza pato la taifa.
Akielezea mikakati ya wizara hiyo jana,kwa viongozi wa wilaya ya Mkuranga ,mkoa wa Pwani na wananchi wa kijiji cha Mkiu ,alisema yeye ni mwenyekiti wa bodi ya EPZA hivyo kwa mamlaka aliyonayo eneo hilo tayari litengwe kwa ajili ya viwanda .
Alisema wakati wowote kuanzia sasa atakaa na bodi hiyo na  ataweka saini kuthibitisha hilo na hatua ya upimaji iweze kuanza.
Mwijage alieleza kuwa ataendelea kusimamia ujenzi wa viwanda kwa wingi na maeneo ya uwekezaji ili kuinua sekta hiyo nchini.
Katika hatua nyingine alisema haitaji kuona kuna mapungufu katika utekelezaji wa majukumu yake ya kazi hivyo atahakikisha mamlaka inayoshughulikia masuala ya gesi anaisimamia.
Aidha alisema wilaya ya Mkuranga ni wilaya ya viwanda kwani kunatarajia pia kujengwa kiwanda cha nguo wilayani Mkuranga kiwanda ambacho kitaweza kuzalisha km za nguo Mil .240 kwa mwaka.
Mwijage alisema ujenzi wa kiwanda hicho utasaidia watannzania kuachana na uvaaji wa nguo za mitumba na kuvaa nguo zinazotengenezwa kwenye viwanda vinavyojengwa hapa nchini.
Alieleza haiwezekani kujenga viwanda vingi vinavyozalisha nguo ndani ya nchi itasaidia kwa kiasi kikubwa kuvaa nguo za mitumba.
Awali mbunge wa jimbo la Mkuranga,Mohammed Ulega aliomba eneo hilo liwe la viwanda kwani tayari imetengwa hekari 600 ambalo limeunganisha maeneo ya Njopeka,Mkiu na Lukanga.
Alisema eneo hilo lina sifa ya uwepo wa gesi ambayo itasaidia kutumika katika viwanda mbalimbali vitakavyojengwa jimboni hapo.
“Serikali ina nia nzuri ya kukuza sekta ya uwekezaji lakini kwa tabia ya urasimu iliyopo kwenye baadhi ya mamlaka ,na utaratibu wa nenda rudi nenda rudi kwa wawekezaji itafikia hatua wawekezaji hawa watakata tamaa”alisema Ulega.
Ulega alisema wilaya imeshapokea viwanda vidogo vidogo na wananchi wanapenda uwekezaji lakini anaomba kuwepo kwa kazi zenye staha na heshima sio bora kazi.
Alisema wanashirikiana na wawekezaji na kuwaheshimu lakini kuna kila sababu na wao kuthamini kazi wanazozitoa kwa wananchi wanaowapatia kazi hizo.
Ulega alisema sio kama hawataki viwanda na sio kama wanashtaki lakini ni bora ziwe kazi zenye tija kwa manufaa ya jamii.
Mkuu wa mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo,alisema ni kipindi kirefu walipigania eneo hilo liwe la viwanda.
Alimshukuru waziri Mwijage kwa ushirikiano wake kwa kushughulikia masuala mbalimbali wanayoyafikisha ofisini kwake .
Mhandisi Ndikilo alimuomba waziri huyo kuendeleza ushirikiano huo ili kukuza sekta ya viwanda na uwekezaji mkoani Pwani.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI