VAT YA UTALII NI VITA YA MADALALI DHIDI YA WAZALENDO.


indexNdugu zangu,
Katika kuliangalia kwa karibu hili la nchi yetu kuweka tozo ya asilimia 18 kwa baadhi ya huduma za kitalii naiona vita ya kimaslahi iliyoibuka kati ya madalali wa utalii na Serikali inayoweka msimamo unaoungwa mkono na wazalendo wa nchi hii.
Ni vita ya kupigania maslahi ya wengi dhidi ya wachache.
Haya ni mapambano muhimu katika wakati tulio nao ambapo wenye kupigania maslahi ya kiudalali wameshafanikiwa kusambaza hofu kuwa watalii wanaikimbia nchi yetu na kwamba tunaelekea kushindwa.
Kenya inayozungumzwa kuondoa kodi hiyo ni hatua ya hila na kizandiki katika ushindani na inachangiwa pia na pigo wanalolipata kutoka na ugaidi wa el shabaab  na hofu yenye kuambatana nayo hususan watalii. Inasikitisha sana na hatuna budi kuwa na mshikamano na jirani zetu wa Kenya katika vita vyao dhidi ya ugaidi.
Hata hivyo, hilo haliondoi ukweli kuwa kwenye sekta ya utalii Kenya ni washindani wetu.
Kama nchi hatuwezi kubadilisha maamuzi yetu tuliojiridhisha kuwa ni sahihi kwa vile tu Kenya wameamua vingine. Hizo ni dalili za kuyumba na kutojiamini kama taifa.
Naamini, Tanzania kama nchi bado inavutia watu wengi wa dunia kuja kuitembelea kutokana na vivutio tulivyo navyo na ambavyo vingine hata mtalii aimalize Kenya yote hawezi kuviona kama si kuzunguka dunia na mwisho kuambiwa, viko Tanzania tu.
Naamini pia, kama mtalii alishaamua kutembelea Tanzania tangu Januari mwaka huu, hawezi kufuta safari yake kwa sababu ya VAT ya asilimia 18. Vinginevyo, hakuwa na dhati ya kufunga safari ya kuja Tanzania.
Isipokuwa, naamini mtalii anaweza kufuta  safari yake aliyoipanga tangu Januari kwa tishio la usalama wake, hata kama ungemuahidi kumuondolea  VAT na kumkaribisha airport na glasi ya bure ya juisi ya ukwaju. Hili ni tatizo kwa wengine, sisi hatuna kwa sasa na linachangia kutuuza kiutalii.
Ni rai yangu kwa Serikali, kuwa isikubali kusogea hata hatua moja kutoka msimamo wa sasa. Tuko kwenye vita na tumezidiwa na wapinzani wetu, kwa kiasi fulani kwenye propaganda.
Vinginevyo, hata kama itachukua muda, lakini haya ni mapambano sahihi na ya haki kwetu, na uwezo wa kushinda tunao.
Maggid.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA