WADAU WA SANAA NCHINI WAHAMASISHWA KUDHAMINI NA KUFADHILI MASHINDANO YA UREMBO BILA UBAGUZI.


S1Miss Dar Indian Ocean aliyemaliza muda wake, Camilla John (katikati) akimvisha skafu Mshindi wa Mashindano ya Miss Tanzania Indian Ocean 2016 Jackline Kimambo (kushoto) mara baada ya kuibuka mshindi katika mashindano hayo yaliyofanyika 30 Julai, 2016 katika Ukumbi wa MRC Ulioko Mikocheni jijini Dar es Salaam.
S2Miss Tanzania Indian Ocean 2016 Jackline Kimambo (aliyekaa katikati) akiwa katika picha ya pamoja na warembo wenzie ambaye ni Mshindi wa pili na wa tatu mara baada ya kumalizika kwa mashindano hayo yaliyofanyika 30 Julai, 2016 katika Ukumbi wa MRC Ulioko Mikocheni jijini Dar es Salaam.
S3Kaimu Mkuregenzi Idara ya Maendeleo ya Sanaa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw. Francis Songoro (kulia) akimpongeza Miss Tanzania Indian Ocean 2016 Jackline Kimambo kwa kuibuka mshindi wa mashindano hayo baada ya kumalizika kwa mashindano hayo yaliyofanyika 30 Julai, 2016 katika Ukumbi wa MRC Ulioko Mikocheni jijini Dar es Salaam.
S4Miss Tanzania Indian Ocean 2016 Jackline Kimambo akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya washiriki baada ya kumalizika kwa mashindano hayo yaliyofanyika 30 Julai, 2016 katika Ukumbi wa MRC Ulioko Mikocheni jijini Dar es Salaam.
……………………………………………………………………………………………..
Na. Benedict Liwenga-WHUSM.
Wadau wanaojishughulisha na masuala ya Sanaa nchini wamehamishwa kujitokeza kwa wingi katika kusaidia maendeleo ya Sanaa kwa kudhamini na kufadhili mashindano ya urembo bila kubagua.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Sanaa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw. Francis Songoro wakati alipokuwa akiwasilisha hotuba ya Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Anastazia Wambura ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi katika Mashindano ya Miss Tanzania Indian Ocean 2016 yaliyofanyika katika Ukumbi wa MRC uliopo Mikocheni jijini hapa.
Akiwasilisha hotuba hiyo, Songoro amesema kwamba kazi inayofanywa na wadau wa sanaa ni hatua ya utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Utamaduni ambayo inasisitiza jamii na wakuzaji sanaa kuendeleza ubunifu katika kazi za kiutamaduni.
Ameeleza kuwa, Serikali kupitia Wizara yake inathamini na kuunga mkono juhudi zinazofanywa na wadau hao hasa katika kukuza na kuviendeleza vipaji vya vijana nchini, hivyo amewapongeza wadau hao kwa moyo wao wa kujitoa na kuwataka kuendeleza kwa vitendo Sera ya Taifa ya Utamaduni ya mwaka 1997 katika Sura ya 9 kifungu cha 9:5:8 ambacho kinasisitiza na kuhimiza watu binafsi pamoja na Mashirika kuwekeza rasilimali katika sekta ya utamaduni.
‘’Maonyesho haya ni ishara tosha kuwa sanaa ni kazi, ajira, biashara na burudani, hivyo kipekee nawapongeza sana’’, alisema Songoro.
Aliongeza kuwa, Warembo ambao wameshiriki katika mashindano hayo wanautangaza utalii wa ndani na nje ya nchi na kwa kufanya hivyo wanaiwakilisha vyema Tanzania Duniani katika mashindano ya Miss World na pia kukuza uchumi wa nchi.
Aidha, amewataka warembo ambao hawakubahatika kuibuka washindi katika mashindano hayo kutokata tamaa, bali waitumie fursa hiyo hususani ya elimu waliyoipata wakiwa kambini kwa kuisadia jamii inayowazunguka na kuwa wanawake wa mfano wa kuigwa katika kujitambua na kujiamini.
‘’Mtambue kwamba, siyo wote mtakaoibuka washindi na kuendelea mbele katika mashindano haya, niwaombe wale ambao hamtashinda msivunjike moyo, bali mkaitumie elimu mliyoipata na yale ambayo mmejifunza mkiwa kambini kwa kuisaidia jamii inayowazunguka na muwe wanawake wa mfano wa kuigwa’’, alisema Songoro.
Katika mashindano hayo, Mshindi wa Kwanza aliyeibuka na kunyakua taji hilo ni Jackline Kimambo ambaye alipatikana kati ya tano bora  na kuvikwa taji la Miss Tanzania Indian Ocean 2016 na Mshindi wa pili ni Regina Ndimbo huku wengine waliobaki kwenye tano bora wamepata fursa ya kuingia katika mashindano ya Miss Kinondoni.
Shindano hilo lilihusisha jumla ya washiriki wapatao 20 ambapo mmoja kati yao ndiyo aliyeibuka mshindi na lilidhaminiwa na wadau mbalimbali wakiwemo Mikocheni Resort Centre, Mlimani TV, Channel Ten, Darling, Helmic, Tanzania Breast Cancer Foundation, Magic FM, Jozi Lounge, Kiss Printers pamoja na NTS.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*