WATAALAM WA ARDHI WATAKIWA KUTOA SULUHISHO LA MIGOGORO YA ARDHI NCHINI.


 Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Ardhi Prof. Idrissa Mshoro akizungumza na Mtandao wa Wanataaluma wa Vyuo Vikuu Vinavyotoa Mafunzo yahusuyo Usimamizi wa Ardhi Kanda ya Afrika Mashariki leo jijini Dar es salaam.
 Washiriki wa Mtandao wa Wanataaluma wa Vyuo Vikuu Vinavyotoa Mafunzo yahusuyo Usimamizi wa Ardhi Kanda ya Afrika Mashariki  kutoka nchi 9 za Bara la Afrika wakifuatilia Mkutano wa mtandao huo leo jijini Dar es salaam.
 Washiriki wa Mtandao wa Wanataaluma wa Vyuo Vikuu Vinavyotoa Mafunzo yahusuyo Usimamizi wa Ardhi Kanda ya Afrika Mashariki  kutoka nchi 9 za Bara la Afrika wakifuatilia Mkutano wa mtandao huo leo jijini Dar es salaam.
 Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Ardhi Prof. Idrissa Mshoro akizungumza na waandishi wa Habari leo jijini Dar es salaam mara baada ya Ufunguzi wa Mkutano wa Wanataaluma ya Usimamizi wa Ardhi Kanda ya Afrika Mashariki .
 Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Mozes Kusiluka akiwaeleza waandishi wa Habari kuhusu mpango wa Serikali wa kupima na kurasimisha maeneo yasiyopimwa katika jiji la Dar es salaam leo.

Na. Aron Msigwa – Dar es salaam.
Serikali imewataka wataalam wa vyuo Vikuu vinavyotoa mafunzo ya Usimamizi wa Ardhi waitumie taaluma yao katika kutafuta suluhisho la migogoro ya Ardhi inayowakumba wananchi katika maeneo mbalimbali nchini.

Akizungumza kwa Niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi wakati wa Ufunguzi wa Mkutano wa Wanataaluma ya Usimamizi wa Ardhi Kanda ya Afrika Mashariki leo jijini Dar es salaam, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo (Sayansi) Prof. Simon Msanjila amesema kuwa wataalam hao wanalo jukumu la kufuatilia migogoro inayotokea nchini na kuhakikisha wanatoa ushauri wa kitaalam utakaotoa majibu ya utatuzi wa migogoro hiyo.

“Ninyi kama watalaam wa sekta ya Ardhi lazima mtoe majibu kwa nini migogoro ya ardhi inaendelea kutokea katika maeneo mbalimbali licha kuwepo kwa kanuni, Sheria na taratibu zinazosimamia sekta ya Ardhi nchini” Amesema Prof.Msanjila.

Ameeleza kuwa wao kama watalaam wa sekta hiyo wanatakiwa kwenda zaidi kwenye matatizo halisi na kuwawafikia wananchi wengi zaidi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili  kuondoa changamoto zao kuliko kucheza na vitabu na kuongea kwenye Ofisi.

 Amewataka wataalam hao hasa wale walioko nchini Tanzania kufika katika maeneo yenye migogoro ya Ardhi ikiwemo Morogoro na maeneo mengine ili kuangalia kwa nini wananchi wanaendelea na mapigano tunajua ipo migogoro ya Ardhi inayotokea katika mikoa ya Morogoro, Pwani na mikoa mingine.

Amesema kuwa kwa upande wa Serikali suala la ufumbuzi wa migogoro ya Ardhi linaendelea kupewa kipaumbele kwa kuhakikisha kuwa ardhi inaendelea kutolewa kwa kuzingatia sheria pia kushughulikia changamoto zote zinazokwamisha ustawi wa sekta ya ardhi hususan uondoaji kero zote zinazokwamisha matumizi bora ya ardhi kwa jamii.

Akifafanua kuhusu nafasi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi katika mkutano huo ameeleza kwamba kupitia mkutano huo wa kitaalam wa masuala ya Ardhi, Wizara hiyo inajifunza kuhusu  changamoto zitakazojitokeza na kuibuliwa ili ziwekwe kwenye mitaala kwa lengo la kuwaandaa watalaam watakaokuwa na uwezo wa kusuluhisha matatizo yote yanayojitokeza kwenye sekta hiyo.

Amesema kuwa Sekta ya Elimu kupitia mkutano huo itaboreshwa kwa kupata nyongeza ya utalaam kutoka kwa wataalam kutoka Vyuo vikuu vya nchi mbalimbali za Bara la Afrika waliohudhuria mkutano huo na kuongeza kuwa Chuo Kikuu Ardhi nchini Tanzania ambacho kimebobea kwenye masuala ya Ardhi kitapata taarifa zaidi katika uboreshaji wa mitaala na mafunzo ya Programu za Utawala wa Ardhi, Ugawaji wa Ardhi na Upimaji wa Ardhi”

Kwa Upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Ardhi Prof. Idrissa Mshoro akizungumza mara baada katika mkutano huo amesema kuwa wataalam wa Ardhi nchini Tanzania bado wana umuhimu mkubwa katika maendeleo ya sekta ya Ardhi na kufafanua kuwa wao kama chuo kinachozalisha watalaam wa Ardhi wanalo jukumu kuzalisha watalaam watakaofanya usimamizi thabiti wa Ardhi kukabiliana na changamoto zilizopo.

“Sisi nafasi yetu kama Chuo Kikuu Ardhi ni kujua ni namna gani tunavyoweza kuzalisha wataalam wa kutosha wenye weledi watakaoweza kukabiliana na changamoto mbalimbali zilizoko kwenye sekta ya Ardhi pia kuhakikisha wataalam tunaozalisha wanakidhi ubora na matarajio ya wananchi” Amesema Prof. Mshoro.

Amesema kuwa wanataaluma kutoka Tanzania watanufaika kutokana na mkutano huo kwa kuwa unawajumuisha watalaam wa Ardhi kutoka takribani nchi 9 watakaobadilishana uzoefu kuhusu changamoto mbalimbali za ardhi zinazojitokeza katika maeneo yao na namna wanavyozitatua.

Aidha, amesema kuwa Sekta ya Ardhi nchini Tanzania bado inakabiliwa na uhaba wa watalaam wa kutosha  ambao wangeweza kusimamia maamuzi katika masuala ya Ardhi ngazi za chini na kuongeza kuwa ili kupata maamuzi na taarifa sahihi za ardhi ni lazima suala la uwepo wa watalaam hao liendelee kupewa kipaumbele.

Kuhusu mchango wa watalaam hao katika utatuzi wa migogoro ya Ardhi amesema kuwa ipo haja ya watalaam waliopo kutumika ipasavyo kutatua migogoro inayojitokeza na kuwaletea manufaa wananchi ambao wanahitaji huduma za wataalam hao.

Amesema kuwa kwa upande wa Serikali tayari watalaam wa sekta husika wamejipanga kuhakikisha kuwa wanapata suluhisho la mgogoro inayojitokeza kupitia sheria zilizopo.

Mkutano huo unaohusisha Mtandao wa vyuo Vikuu ni wa nane  tangu kuanzishwa Mtandao wa EALAN mwaka 2009 ambapo kwa mwaka huu Chuo Kikuu Ardhi, Tanzania kimekuwa mwenyeji wa Mkutano huo kufuatia kuteuliwa kuwa kituo Maalum Cha Mafunzo ya Usimamizi wa Ardhi Barani Afrika.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*