CAF YAPITISHA USAJILI WA YANGA, KESSY NAYE APETA


Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
KWA mara nyingine, Shirikisho la Afrika (CAF) limepitisha usajili wa beki mpya wa Yanga, Hassan Kessy aliyesajiliwa kutoka kwa mahasimu Simba SC.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya Habari usiku wa kuamkia leo, CAF imetoa orodha ya wachezaji wote waliopitishwa katika usajili mdogo wa hatua ya makundi ya michuano ya Afrika – Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho.
Na katika Kombe la Shirikisho wachezaji wote wapya watano wa Yanga wamepitishwa na kupewa leseni za kucheza mechi za Kundi A, zinazoelekea ukingoni.
Hao ni Obrey Chola Chirwa, Juma Hassan Mahadhi, Benno David Kakolanya, Hassan Khamis Ramadhan ‘Kessy’ na Vicent Andrew Chikupe.
Hassan Kessy anasubiri busara za Simba kuanza kuichezea Yanga
Hata hivyo, kutokana na kosa walilofanya Yanga SC kuanza kumsajili Kessy kabla ya hajamaliza Mkataba wake na Simba, sasa watalazimika kuzungumza na klabu yake hiyo ya zamani ili wamridhie kucheza.
Na kwa sababu Yanga imeshindwa kujishusha kwa Simba, Kessy ameendelea kubaki nje huku hatua ya makundi ikielekea ukingoni na timu hiyo ina nafasi finyu ya kusonga mbele.  
Yanga kesho watawakaribisha Mouloudia Olympique Bejaia katika mchezo wa marudiano Kundi A Kombe la Shirikisho Afrika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Yanga itaingia katika mchezo wa kesho ikitoka kucheza mechi tano bila kushinda ikilazimishwa sare ya 0-0 na Mtibwa Sugar ya Morogoro katika mchezo wa kirafiki, ikifungwa 1-0 mara mbili, na Mouloudia Olympique Bejaia nchini Algeria na TP Mazembe Dar es Salaam kabla ya kutoa sare ya 1-1 na Medeama SC mjini hapa na baadaye kwenda kufungwa 3-1 na timu hiyo nchini Ghana katika mchezo wa marudiano.
Makocha wa Yanga, Mholanzi Hans van der Pluijm (kulia) na Msaidizi wake, Juma Mwambusi (kushoto) wakiwa na winga Simon Msuva
Wachezaji wa Yanga wakiwa mazoezini jana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam

Mara ya mwisho Yanga kushinda ilikuwa ni kwenye Fainali ya Kombe la TFF, ilipoibugiza Azam FC 3-1 Uwanja wa Taifa. 
Yanga itahitimisha mechi zake za Kundi A Kombe la Shirikisho kwa kumenyana na wenyeji TP Mazembe ya DRC mjini Lubumbashi Agosti 23, mwaka huu.
Mazembe inaongoza Kundi A kwa pointi zake 10 baada ya mechi nne, ikishinda tatu na kutoa sare moja, ikifuatiwa na Bejaia na Medeama, ambazo kila moja ina pointi tano za sare tatu na ushindi mmoja, wakati Yanga inashika mkia kwa pointi yake moja. 

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*