KAMA MANJI ATAONDOKA ANGALAU HESHIMA TU YA KUMUAGA, SI KEJELI NA MAJINGAMBO



Na Saleh Ally, Dubai
NIKIWA nje ya nyumbani Tanzania kutekeleza majukumu kadhaa ya SALEHJEMBE,  nimesikia Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji, yuko katika hatua za mwisho kuachia ngazi.

Baadaye nikaanza kupata taarifa mbalimbali kuhusiana na Manji kwamba ameamua kujiondoa uenyekiti wa Yanga kwa kuwa amechoshwa na hali ya kusakamwa na kila anachofanya kuonekana ni kibaya.

Chanzo kingine kikanieleza kwamba Manji anaweza kuondoka kwa kuwa kuna baadhi ya viongozi wa Serikali ya Tanzania, wamekuwa wakifanya kampeni za kuhakikisha anang’oka Yanga.

Chanzo kikuu kinaelezwa kuwa ni suala la kutaka kuwekeza Yanga na yeye alitumia neno kukodisha ambalo lilizua mjadala mkubwa saa chache tu baada ya kulieleza hilo.

Juhudi za kumpata licha ya kwamba niko nje ya nchi zilikuwa kubwa, mwisho nilifanikiwa na kumuuliza uhakika wa kile kilichokuwa kinaendelea.

Lakini Manji alionekana kutotaka kulizungumzia suala hilo zaidi ya kunieleza hivi: “Ndugu yangu ningependa uniache, mimi pia ni binadamu. Wakati mwingine napenda kupumzika.

“Haiwezekani mimi nikawa mbaya kwa kila kitu, muda wangu, fedha na mambo mengi nafanya kwa ajili ya Yanga. Lakini watu wananipiga vita sana, hadi inafikia nakata tamaa.”

Nilipotaka kupata uhakika kwamba kwa kauli yake hiyo maana yake ameishajitoa Yanga au kuachia ngazi nafasi ya mwenyekiti, jibu lake likawa hivi: “Naomba uniache ndugu yangu, nimechoka, nataka kupumzika.”

Halafu baada ya hapo alipotea hewani, kwa kuwa niko mbali na nyumbani, ikawa vigumu kumpata kwa mara nyingine na kuzungumza naye. Lakini nikawa na maswali mengi sana baada ya kuanza kuona wadau wakichangia kwenye mitandao ya kijamii.

Wengi walionekana kushangazwa na wakasema kama ni kweli, basi Manji anapaswa kufikiria upya uamuzi wake huo. Kwamba ni wachache sana wanaompiga vita na Wanayanga wengi wanathamini mchango wake, jambo ambalo si siri hata kidogo.

Lakini wale wanaoonyesha kufurahia, wazo langu likaenda moja kwa moja huenda ni Wanayanga wasiopenda maendeleo au wale wenye tabia ya kutokubali mazuri ya wengine au inawezekana pia ni marafiki wa wapinzani wa Manji.

Tena wengi wamekuwa wakimuunga mkono katibu wa baraza la wazee la yanga, Ibrahim Akilimali eti ni shujaa mkubwa kwa maneno yake ya kejeli kwa Manji.

Lakini jana, nasikia Akilimali kawa muungwana na kuona alichofanya si sahihi hata kidogo. Sijui sasa hao waliokuwa wakimshabikia nao kama wataomba radhi au watakaa kimya tu.

Wapo ambao Manji akiwa madarakani wana hofu, huenda walishindwa kuivuruga Yanga kwa urahisi au hawakufurahishwa na uimara wa Yanga, hivyo wangependa kuona kisiki au kigingi kwao kinaondoka au kuondolewa.

Lakini nani asiyejua kwamba Manji amefanya mengi makubwa kwa mamilioni ya fedha ambayo hata hao wanaofurahia wangeambiwa watoe robo tu wasingeweza? Kwani Yanga ina matajiri wangapi ambao Manji amewakuta? Kweli ni wengi sana, sasa vipi mbona hawatoi?

Hadi anaingia Manji, Yanga imekuwa ikisuasua. Lakini amekwenda taratibu anafanya mambo yakibadilika hadi kufikia Yanga ambayo inaogopwa na sasa kwa miaka minne ndiyo timu yenye mafanikio zaidi Tanzania, tena mfululizo.

Hivyo hauwezi kusema Manji ni adui mkubwa hivyo wa Yanga, tena anayepaswa kuonekana kuondoka kwake ni nafuu kwa Yanga na watu wanapaswa wamsukume kwa maneno ya jazba na hasira, utafikiri alizuia riziki zao na wakashindwa kuendesha familia zao labda kwa kudhibiti mianya fulani. Au aliwabana rafiki zao wakashindwa kufaidika, nao wakayumba kimaisha.

Kwa kuwa sina uhakika, niseme hivi. Kama Manji atakuwa ameweka msimamo wa kuondoka, Wanayanga nao wakaafiki, basi vizuri kuagana naye vizuri kwa kuwa kuna kesho.
Jazba au maneno ya kashfa hayawezi kuwa msaada hata chembe. Pia hata kama alifikia uamuzi huo, hakuna haja ya kuanzisha malumbano. Naye ni binadamu na ana maamuzi yake.

Simba wameonyesha mfano mzuri hivi karibuni, mchezaji wao mkongwe Mussa Hassan Mgosi amestaafu. Badala ya kusukumwa kwa maneno na matusi, amepewa heshima ya kuagwa tena uwanjani.

Inawezekana Manji asipate nafasi ya kuagwa uwanjani na sisemi aagwe uwanjani, lakini nakumbushia jambo la kuachana vizuri, kwa njia sahihi kuliko kuanzisha malumbano.


Wale wenye furaha kama kweli Manji atakuwa ameondoka Yanga, nao wanapaswa kupunguza furaha yao ambayo inaweza kupandwa na mihemko inayoweza kusababisha malumbano baina yao na wanachama wanaotambua au kuthamini mchango wa Manji.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI