MGOSI MENEJA MPYA SIMBA, MWALYANZI ATOLEWA KWA MKOPO AFRICAN LYON

Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
MSHAMBULIAJI mkongwe, Mussa Hassan Mgosi amestaafu rasmi soka na sasa anakuwa Meneja wa timu ya Simba SC.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Simba SC, Hajji Sunday Manara amesema kwamba Mgosi ataagwa rasmi katika mchezo wa kirafiki dhidi ya URA ya Uganda Jumapili Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Na Manara amesema kwamba aliyekuwa Meneja wa timu, Abbas Suleiman Ally anakuwa Mratibu wa timu kuanzia leo na Nahodha mpya ni Jonas Gerald Mkude.
Aidha, Manara amesema kiungo Peter Mwalyanzi aliyesajiliwa msimu uliopita kutoka Mbeya City, ametolewa kwa mkopo African Lyon iliyopanda Ligi Kuu msimu huu.
Mussa Hassan Mgosi ataagwa Jumapili kabla ya kustaafu na kuwa Meneja wa timu
“Kulingana na usajili uliofanyika msimu huu, timu sasa itakuwa na viungo wengi na ushindani wa namba utakuwa mkubwa, hivyo tumeona Mwalyanzi tumpeleke African Lyon kwa mkopo akapate nafasi ya kutunza kipaji chake,”.
“Kama atafanikiwa kukuza kiwango na mwalimu akajiridhisha, basi atarejeshwa huko mbele ya safari,”alisema.
Kikosi cha Simba SC kinaingia kambini leo Ndege Beach Hotel, Mbweni kujiandaa na mchezo wa kirafiki dhidi ya URA Jumapili Uwanja wa Tafa.
Na mashabiki wa Simba SC watapata fursa ya kukishuhudia kikosi chao kwa mara ya pili wiki hii, kitakapomenyana na URA.
URA wanatarajiwa kuwasili leo na kesho watacheza mechi ya kwanza ya kujipima nguvu dhidi ya Azam FC Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Mapema Jumatatu, Simba SC iliitandika mabao 4-0 AFC Leopard ya Kenya katika mchezo wa kwanza rasmi wa kirafiki chini ya kocha Mcameroon, Joseph Marius Omog.  
Katika mchezo huo uliokwenda sambamba na sherehe za miaka 80 ya Simba, mshambuliaji chipukizi wa kimataifa wa Tanzania, Ibrahim Hajib Migomba aliendelea kumvutia kocha Omog baada ya kufunga mabao mawili, huku wachezaji wapya, Mrundi Laudit Mavugo na Shizza Kichuya wakifunga pia. 
Hadi mapumziko, Simba walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililofungwa na Hajib dakika ya 38 kwa shuti la umbali wa mita takriban 30 baada ya kupokea pasi ya kiungo Mkongo, Mussa Ndusha.
Hajib alimalizia vizuri krosi ya Kichuya kuifungia Simba SC bao la pili dakika ya 56, kabla ya Kichuya kufunga bao la tatu dakika ya 66, akimalizia krosi ya Mavugo.
Mavugo aliyeingia kipindi cha pili kumpokea Muivory Coast Frederick Blagnon, aliifungia Simba SC bao la nne dakika ya 82 akiunganisha krosi nzuri ya Kichuya.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DKT NCHIMBI ASHIRIKI MAZISHI YA ASKOFU.GACHUMA WA KANISA LA NLGCC

π™‚π˜Όπ™ˆπ™Šπ™‰π˜Ώπ™„ π™†π˜Όπ˜Ύπ™ƒπ™€π™•π˜Ό π™†π™„π˜½π™„π™‰π™‚π™’π˜Ό.