MKANDARASI APEWA WIKI MBILI KURUDISHA VIFAA NA KUENDELEA NA UJENZI SUMBAWANGA



Mkandarasi Jianx-Geo Engineering Group Corporation kutoka China anayejenga sehemu ya barabara ya Sumbawanga Mjini-Chala-Kanazi kwa kiwango cha lami amepewa wiki mbili kurejesha vifaa vya ujenzi katika eneo la kazi ili kuongeza kasi ya ujenzi wa barabara hiyo ambao umeonekana kusuasua kutokana na ukosefu wa vifaa vya kutosha.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, wakati alipokagua mradi wa ujenzi wa barabara ya Sumbawanga-Namanyere-Mpanda Mkoani Rukwa.

Waziri Prof. Mbarawa amesema barabara hiyo imegawanywa katika sehemu mbili ambazo ni Sumbawanga Mjini-Chala-Kanazi KM 75 na Kanazi-Kizi-Kibaoni KM 76.6 ili kuhakikisha barabara hiyo inakamilika kwa wakati na viwango kulingana na mkataba.

“Hakikisheni baada ya wiki mbili vifaa vinakuwepo katika eneo la kazi na mnatekeleza wajibu wenu kukamilisha barabara hii kwa wakati tuliokubaliana ili ianze kutumiwa na wananchi”, amesema Prof. Mbarawa.

Waziri Prof. Mbarawa ameongeza kuwa wananchi wanamatarajio makubwa na barabara hiyo kwa muda mrefu hivyo Mkandarasi ahakikishe kazi ya ujenzi katika kipande kilichobaki kwa kiwango cha lami inamalizika ifikapo mwezi Julai mwakani ili kuharakisha shughuli za kimaendeleo mkoani hapo.

Aidha, amemtaka mkandarasi huyo kukamilisha mzani wa kupima uzito wa magari katika kijiji cha Kanondo KM 5 kutoka Sumbawanga mjini ifikapo mwezi Agosti mwaka huu kwa lengo la kudhibiti uzito wa magari yanayofanya shughuli za kusafirisha mizigo na abiria katika barabara hiyo.

Kwa upande wake Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Rukwa, Eng. Masuka Mkina amemuhakikishia Waziri Mbarawa kuwa ujenzi wa barabara zote utazingatia viwango na utakamilika kwa wakati.

"Nikuhakikishie kuwa tutasimamia na kuzingatia viwango vilivyowekwa katika mradi wa ujenzi huu ili wananchi wanufaike na kuongeza uchumi wa mkoa ",amesema Eng. Mhina.

Ujenzi wa barabara ya Sumbawanga-Namanyere-Mpanda kwa kiwango cha lami unagharamiwa na Serikali ya Tanzania kwa jumla ya kiasi cha Shilingi bilioni 150.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akitoa maelekezo kwa Mkandarasi anayejenga barabara ya Sumbawanga Mjini-Chala- Kanazi yenye urefu wa KM 75 alipokagua ujenzi wa barabara hiyo.
Mkandarasi anayejenga barabara ya Kanazi-Kizi-Kibaoni yenye urefu wa KM 76.6 akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa wakati alipokagua ujenzi huo. Katikati ni Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) Mkoa wa Rukwa Eng. Masuka Mkina.
Mbunge wa Jimbo la Nkasi kaskazini Mhe. Ally Kessy (mwenye kofia) akieleza jambo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa wakati alipokagua miundombinu ya Bandari ya Kipili, Mkoa wa Rukwa.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (Kulia) akitoa maelekezo kwa Meneja wa kiwanja cha ndege cha Rukwa Bw. Sandali Kaisi (kushoto) kuhusu uboreshwaji wa kiwanja hicho wakati alipotembelea kiwanja hicho.
Meneja wa kiwanja cha ndege cha Rukwa Bw. Sandali Kaisi (wa kwanza kushoto) akitoa maelezo ya hali ya miundombinu kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (kulia kwake) wakati Waziri alipokagua kiwanja hicho.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (wa pili Kulia) akitoa maelekezo kwa Meneja wa kiwanja cha ndege cha Rukwa Bw. Sandali Kaisi (wa kwanza kushoto) wakati alipokagua kiwanja hicho.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akitoa maelekezo kwa Afisa Uendeshaji wa Bandari ya Kipili Bw. Hamis Msellem wakati alipokagua miundombinu ya bandari hiyo wilaya ya Nkasi, Mkoani Rukwa. Kulia kwake ni Mbunge wa Jimbo la Nkasi kaskazini Mhe. Ally Kessy.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akifafanua jambo kwa Mbunge wa Jimbo la Nkasi Kaskazini Mhe. Ally Kessy wakati alipokagua miundombinu ya bandari hiyo, Mkoani Rukwa.
Mbunge wa Jimbo la Nkasi kaskazini Mhe. Ally Kessy akiteta jambo na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa wakati alipotembelea Jimboni kwake.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI