SERIKALI MTANDAO KUPUNGUZA URASIMU NA KUONGEZA TIJA KATIKA TAIFA


Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Serikali Mtandao Dk. Bakari Jabiri akitoa ufafanuzi kwa Waziri Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Angellah Kairuki (kulia) kuhusu kituo cha ufuatiliaji mifumo ya mawasiliano Serikalini, Ofisi za Wakala ya Serikali Mtandao (e-GA) jijini Dar es salaam.

Na Aron Msigwa – MAELEZO.

Matumizi ya Teknolojia ya Habari na mawasiliano (TEHAMA) katika uendeshaji wa shughuli za serikali ( e-Government) katika miaka ya hivi karibuni yameendelea kukua kwa kasi na kupata nguvu katika nchi mbalimbali duniani kutokana na mchango wake katika kufanikisha utoaji wa taarifa na huduma kwa wananchi kwa haraka na gharama nafuu.

TEHAMA imegusa maisha ya kila siku ya wananchi na kurahisisha mawasiliano muhimu katika shughuli zao kiuchumi, kiutamaduni, kisiasa na kijamii. Aidha, TEHAMA imekuwa mkombozi katika kurahisisha na kuimarisha sekta ya biashara na fedha.

Ripoti ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 2014 kuhusu matumizi ya Mtandao katika shughuli za Serikali ( 2014 UN e- Government Survey) kwa nchi 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa inaonesha kuwa matumizi ya TEHAMA kwenye shughuli za Serikali duniani kote yamefanikiwa sana kuwasogeza wananchi karibu na Serikali.

Matumizi hayo yameongeza uwazi, uwajibikaji,ufanisi na matokeo makubwa yanayozingatia muda katika nyanja mbalimbali zinazogusa maisha ya kila siku ya wananchi. Miongoni mwa nchi zinazofanya vizuri zaidi duniani katika matumizi hayo ni Jamhuri ya Korea ambayo imetajwa kuwa nchi ya kwanza ikifuatiwa na Australia na Singapore.

Nchi nyingine zinazofuatia ni Ufaransa, Japan, Marekani, Uingereza, New Zealand, Finland,Uholanzi, Uruguay, Ireland, Australia, Canada, Norway,Sweden, Iceland, Urusi,India,China, Ujerumani, Israel, Denmark, Luxemburg,Italia, Ubelgiji, Hispania, Chile,Bahrain, Estonia na Austria.

Kwa mujibu wa Ripoti hiyo Tanzania ni miongoni mwa nchi za Bara la Afrika zilizo katika kundi la kati katika matumizi ya Serikali Mtandao. Nchi nyingine za Afrika ambazo ziko kwenye kundi hilo ni Tunisia, Mauritius, Misri, Seychelles, Rwanda, Kenya, Uganda, Afrika Kusini, Botswana, Namibia, Nigeria, Angola, Zimbabwe, Ghana, Swaziland, Gabon, Algeria, Cape Verde na Cameroon.

Kama tunavyojua Tanzania sio kisiwa, haiwezi kujitenga na mabadiliko haya. Aidha, ni ukweli usiopingika kuwa matumizi ya mtandao katika shughuli za Serikali yameokoa muda wa watu kufuatilia huduma na taarifa kutoka eneo moja hadi jingine, yamepunguza gharama na usumbufu waliokuwa wakiupata wananchi wakati wa kulipia huduma na tozo mbalimbali za Serikali, utafutaji wa taarifa za huduma, matangazo ya serikali na nafasi za ajira ambazo sasa zinapatikana kwa njia ya mtandao.

Jukumu na mamlaka ya kuratibu na kusimamia utekelezaji wa Serikali Mtandao nchini liko chini ya Wakala ya Serikali Mtandao (e-Government Agency) iliyoanzishwa Aprili, 2012 chini Sheria ya Wakala za Serikali Na. 30 ya mwaka 1977.

Wakala hiyo pamoja na mambo mengine ilianzishwa kwa lengo la kuboresha uwezo wa taasisi za umma kutekeleza jitihada za Serikali Mtandao, kuboresha upatikanaji wa huduma hiyo kwa umma, kuboresha mifumo shirikishi ya TEHAMA, kusimamia uzingatiaji wa viwango pamoja na kutoa ushauri wa kitaalam na msaada wa kiufundi na huduma.

Mtendaji Mkuu wa Wakala hiyo Dkt. Jabiri Bakari anaifafanua dhana ya Serikali Mtandao kuwa ni matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika taasisi za umma kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma na taarifa kwa umma, kwa haraka na kwa gharama nafuu.

Anasema utekelezaji Serikali Mtandao umegawanyika katika maeneo makuu manne ambayo ni kati ya Serikali na watumishi wake, Serikali na Sekta ya Biashara, Serikali na Wananchi pia ni kati ya Taasisi moja na Taasisi nyingine za Serikali.

Dkt. Jabiri anaeleza kuwa lengo la kuanzishwa kwa Serikali mtandao nchini Tanzania ni kuimarisha utawala bora, kuongeza tija na ufanisi katika uendeshaji wa taasisi za umma na kuhakikisha kunakuwa na mawasiliano ya haraka yenye uhakika na salama ndani ya serikali na taasisi zake.

Aidha, Serikali mtandao inapanua wigo wa upatikanaji wa taarifa muhimu katika kila ngazi ya Serikali, kuimarisha usalama wa serikali na raia wake pamoja na kuongeza uwezo wa Serikali kupambana na majanga kwa kutumia teknolojia.

Anabainisha kwamba serikali mtandao inafanya kazi kama ilivyo Serikali ya kawaida kwa maana ya mfumo (system) ambao ndani yake una mifumo midogo midogo kwa maana ya taasisi mbalimbali, wakala, mashirika na halmashauri ambazo zote hutengeneza mfumo mkubwa mmoja wenye lengo la kuwahudumia wananchi.

Jambo linaloitofautisha Serikali mtandao na Serikali ya kawaida ni suala la matumizi ya muda mchache katika kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi.Kupitia serikali mtandao mwananchi hujaza fomu kwa njia ya mtandao kisha mifumo ya TEHAMA iliyowekwa huwasiliana na kubadilishana taarifa na kutoa huduma stahiki kwa mwananchi.

Utendaji wa serikali unaotumia mfumo wa mafaili/majalada ya kawaida (files system) hutumia muda mwingi kushughulikia jambo moja, mwananchi anapoomba huduma anatakiwa kwenda kuchukua fomu kwenye ofisi ya Serikali na kuijaza kisha kuiwasilisha moja kwa moja kwenye taasisi husika.

Mfano, mwananchi anapoomba Hati ya kusafiria kutoka Serikalini, analazimika kwenda Idara ya Uhamiaji na kujaza fomu za maombi ya huduma. Hatua ya kujaza na kurejesha fomu hizo haichukui muda mrefu isipokuwa pale tu inapoanza hatua ya uhakiki na utambuzi wa taarifa zilizowasilishwa na mwananchi ili ziweze kufanyiwa kazi na taasisi husika.

Ni ukweli usiopingika kuwa zoezi la uhakiki wa taarifa za mwanachi anayeomba Hati ya kusafiria au leseni ya udereva au kitambulisho cha Taifa kwa njia ya kawaida bila kutumia mtandao huchukua muda mrefu kwa kuwa suala la uhakiki wa taarifa zikiwemo za mwenendo wa makosa mbalimbali, kuzaliwa na mambo mengine hufanywa na taasisi zaidi ya 4 au 5 wakati kupitia TEHAMA jambo hilo lingeweza kufanywa ndani ya siku moja.

Dkt. Jabiri anasema ili Serikali mtandao iweze fanya kazi yake ipasavyo hapa nchini lazima kuwe na miundombinu ndani au nje ya taasisi pia uwepo wa mifumo Tumizi ( Application Systems) inayoshughulikia masuala mbalimbali, uwepo wa wafanyakazi uwepo wa Sera, miongozo na taratibu za kusimamia TEHAMA kuwezesha utoaji wa huduma mtandao (e - Services).

Dkt. Jabiri anasisitiza kuwa Tanzania iko kwenye hatua ya kwanza na ya pili kwa kuwa taasisi za Serikali zipatazo 200 zina miundombinu na tovuti zenye taarifa za awali za kumsaidia mtu kujua huduma inayotolewa na taasisi husika ili aweze kuchukua hatua ya kupata huduma.

Katika hilo Wakala ya Serikali mtandao imefanikiwa kusanifu Tovuti Kuu ya Takwimu Huria (Open Data Portal) ambayo ina taarifa mbalimbali za sekta tatu zilizopewa kipaumbele Maji, Elimu na Afya.

Pia serikali ilianzisha Tovuti ya Ajira (Ajira Portal) kwa lengo la kuwapatia wananchi taarifa za ajira serikalini, Tovuti Kuu ya Serikali,Tovuti Rasmi ya Wananchi ambayo inamwezesha mwananchi kuwasilisha maswali na hoja ambazo hujibiwa na Serikali pamoja na uanzishaji mfumo wa Barua Serikalini (GMS) ambao sasa unatumiwa na taasisi 117 za Serikali na Balozi za Tanzania ambao umejikita katika kuimarisha mawasiliano kwa njia ya barua pepe na kuongeza usalama wa ubadilishanaji taarifa.

Mtendaji huyo anaeleza kuwa katika awamu ya kwanza taasisi 75 za serikali na Wizara zote za Serikali kupitia mkongo wa taifa, pia Wakala imeziunganisha Taasisi 72 zilizounganishwa kwa simu zinazotumia itifaki ya Intaneti kwenye mkongo wa taifa ili kurahisisha mawasiliano na kupunguza gharama.

Aidha, anaeleza kuwa suala la baadhi ya Taasisi za serikali kukawia kuunganishwa kwenye mtandao huo linatokana na mapungufu yaliyokuwa kwenye miongozo na taratibu zinazosimamia shughuli zaTEHAMA ikiwemo uanzishaji wa tovuti, jambo ambalo Wakala hiyo inalisimamia sasa kwa kuzitaka taasisi zote za Serikali ziwe na tovuti zenye mfumo unaofanana.

Anasisitiza kuwa licha ya mabadiliko ya kiutendaji yanayotokea kwenye taasisi za Serikali, Wakala ya Serikali mtandao imekuwa makini kuhakikisha hakuna mfumo unaoinuka dhidi ya mfumo mwingine lengo likiwa kumhakikishia mwananchi huduma katika eneo moja kwa muda mfupi.

Meneja Habari,Elimu na Mawasiliano wa Wakala ya Serikali Mtandao Bi. Suzan Mshakangoto anasema kuwa katika kuimarisha matumizi ya Serikali Mtandao nchini matumizi ya mitandao isiyo rasmi katika shughuli za serikali kwa sasa hayana nafasi.

Anasisitiza kwamba mkakati uliopo ni kuhakikisha mawasiliano na matumizi ya barua pepe nje ya mfumo wa serikali kwenye ofisi za umma yanafungwa kabisa ili dhana ya Serikali mtandao ichukue nafasi yake.

"Mpaka sasa tumetoa mafunzo ya usimamizi na ujenzi wa mtandao wa Mawasiliano serikalini na usalama wa Mtandao kwa kwa taasisi za umma149 wakiwemo maofisa TEHAMA 226, mafunzo ya vituo vya uendeshaji wa vituo vya Data kwa taasisi za umma 91 na mafisa TEHAMA 162 pamoja na mafunzo ya usimamizi wa mfumo wa Barua Pepe Serikalini kwa taasisi 157" Anaeleza Bi.Suzan.

Aidha, anaeleza kuwa mpaka sasa taasisi 200 za umma zina tovuti ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa na huduma kwa wananchi. Changamoto iliyopo ni Tovuti nyingi kukosa taarifa zilizohuishwa pia kuunganisha maeneo ambayo bado hayajafikiwa hasa Halmashauri na vijiji ili kuwezesha taarifa mbalimbali kupatikana kwa wakati.

Anafafanua kuwa hatua ya mifumo ya serikali kuchelewa kufanya kazi pamoja katika kubadilishana taarifa linatokana na kwamba awali hakukuwa na mfumo uliowezesha jambo hilo kufanyika kutokana na mapungufu yaliyojitokeza kwenye Sera, miongozo na taratibu zinazosimamia masuala ya TEHAMA nchini lakini sasa kuna mwongozo uliotolewa kuhakikisha mifumo ya taasisi za Serikali inawasiliana na kufanya kazi pamoja ili kuondoa mapungufu yaliyokuwepo.

Kwa mujibu wa Bi. Mshakangoto, taasisi zaidi ya 72 za serikali zikiwemo Wizara zote, Wakala, Bunge na Mahakama zimeunganishwa huku halmashauri zilizounganishwa kwenye mkongo wa taifa zikifikia 77. Aidha kazi ya kuzifikia halmashauri zilizobaki inaendelea ili kuwezesha mawasiliano ya serikali kupita kwenye mkongo wa taifa.

Pia katika kuhakikisha kuwa huduma za Serikali zinamfikia mwananchi kupitia simu za mkononi umeanzishwa mfumo shirikishi unaowarahisishia wananchi kupata huduma za Serikali popote walipo. Mfumo huu uliobeba huduma mbalimbali zinazotolewa na taasisi za umma unapatikana kupitia namba maalumu ya kutolea huduma *152*00#, unaokoa muda wa kufuata huduma kwenye ofisi husika, unaondoa urasimu na kupunguza mianya ya rushwa.

Matumizi ya serikali mtandao yataongeza ufanisi na tija katika Taifa kwani upotevu wa muda na umbali vitapunguzwa kwa kiwango kikubwa kama si kuondolewa kabisa. Hivyo watumishi wa serikali na wananchi kwa ujumla tuitumie hii mifumo kwa ajili ya kuharakisha maendeleo.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DKT NCHIMBI ASHIRIKI MAZISHI YA ASKOFU.GACHUMA WA KANISA LA NLGCC

π™‚π˜Όπ™ˆπ™Šπ™‰π˜Ώπ™„ π™†π˜Όπ˜Ύπ™ƒπ™€π™•π˜Ό π™†π™„π˜½π™„π™‰π™‚π™’π˜Ό.