4x4

SIMBA YAANZA VIZURI YAIBAMIZA NDANDA 3-1


Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
SIMBA SC imeanza Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwa kishindo kufuatia ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Ndanda FC ya Mtwara jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Japokuwa hakufunga hata bao moja, lakini beki wa kulia Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ ndiye anastahili sifa zaidi kwa ushindi mnono wa Simba leo, kutokana na kuseti mabao yote. 
Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Emmanuel Mwandembwa wa Arusha, hadi mapumziko timu hizo zilikuwa zimefungana bao 1-1.
Simba SC walitangulia kwa bao la mshambuliaji kutoka Burundi, Laaudit Mavugo dakika ya 20 aliyemalizia mpira wa adhabu wa Tshabalala.
Frederick Blagnon (kushoto) akikimbia baada ya kuifungia Simba bao la pili. Kulia ni mshambuliaji aliyefunga bao la kwanza, Laudit Mavugo


Mavugo akiwa ameinuliwa na Tshabalala baada ya kufunga bao la kwanza. Mwingine ni mfungaji wa bao la tatu, Shizza Kichya

Mshambuliaji anayeinukia vizuri nchini, Omary Mponda akaisawazishia Ndanda FC dakika ya 37 kwa kichwa akimalizia krosi ya Nahodha Kiggi Makassy.
Mabadiliko yaliyofanywa na kocha Mcameroon wa Simba, Joseph Marius Omog kipindi cha pili akiwatoa Jamal Mnyate na Ibrahim Hajib na kuwaingiza Mwinyi Kazimoto na Frederick Blagnon  yaliiongezea uhai Simba na kuvuna mabao zaidi.
Mshambuliaji kutoka Ivory Coast, Blagnon alianza kuifungia Simba SC bao la pili dakika ya 73 kwa kichwa akimalizia kona ya Tshabalala.
Shiza Kichuya akimtoka Nahodha wa Ndanda FC, Kiggi Makassy
Nyota wa mchezo wa leo, Tshabalala akimtoka bekin wa Ndanda, Paul Ngalema 

Beki wa kulia wa Simba, Hamad Juma akimtoka kiungo wa Ndanda FC, Salum Telela

Nyota wa mchezo wa leo, Tshabalala akaseti bao la tatu baada ya kupiga kona iliyotemwa na kipa Jackson Chove na winga Shizza Ramadhani Kichuya akasukumia nyavuni kuipa Simba SC ushindi wa 3-1.
Kwa ujumla Simba SC imecheza leo na ilistahili ushindi huo, wakati Ndanda walionyesha upinzani kwa wenyeji kipindi cha kwanza pekee. 
Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Vincent Angban, Hamad Juma, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Novaty Lufunga, Method Mwanjali, Jonas Mkude, Shizza Kichuya/Mohamed Ibrahim dk84, Muzamil Yassin, Laudit Mavugo, Ibrahim Hajib/Frederick Blagnon dk62 na Jamal Mnyate/Mwinyi Kazimoto dk69. 
Ndanda FC; Jackson Chove, Azizi Sibo/Bakari Mtama dk65, Paul Ngalema, Kiggi Makasi, Hemed Khoja, Salvatory Ntebe, Forahim Isihaka, Bryson Raphael, Salum Telela, Omary Mponda na Shija Mkina/Nassor kapama dk65.
Post a Comment