YANGA KUWAKOSA ABDUL, MSUVA MECHI NA MTIBWA LEO, AJENDA ZA MKUTANO HIZI HAPA!


Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
YANGA SCA inashuka dimbani leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kumenyana na Mtibwa Sugar ya Morogoro katika mchezo wa kirafiki.
Yanga inatarajiwa kuwakosa nyota wake watatu, ambao ni beki Juma Abdul anayesumbuliwa na Malaria na mawinga Geoffrey Mwashiuya na Simon Msuva wanaosumbuliwa na maumivu ya goti kila mmoja.
Mchezo utafanyika baada ya kumalizika kwa Mkutano Mkuu wa dharula wa klabu ulioitishwa na Mwenyekiti, Yussuf Manji utakaoanza Saa 3:00 asubuhi ya leo.
Juma Abdul (kulia) akiwa na Amissi Tambwe juzi nje ya Uwanja wa mazoezi
Ajenda katika Mkutano huo zinatarajiwa kuwa 1. Mwenendo wa Timu, 2. Mahusiano kati ya Yanga na TFF, 3. Katiba ya Yanga, 4. Mapato na Matumizi ya Klabu, 5. Shukrani kwa Wajumbe waliomaliza muda wao, 6. Kuishukuru Serikali kwa ushirikiano wanaonyesha kwenye mashindano klabu inayoshiriki, 7.Maendeleo ya klabu na 8. Mengineyo.
Na mchezo wa leo ni sehemu ya maandalizi ya mchezo wa Kundi A Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Mouloudia Olympique Bejaia ya Algeria Jumamosi ijayo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Yanga itakuwa inasaka ushindi wa kwanza siku hiyo baada ya kucheza mechi zote nne za awali bila ushindi, ikifungwa tatu na kutoa sare moja.
Yanga ilifungwa 1-0 mara mbili, na Mouloudia Olympique Bejaia nchini Algeria na TP Mazembe Dar es Salaam kabla ya kutoa sare ya 1-1 na Medeama SC mjini hapa na baadaye kwenda kufungwa 3-1 na timu hiyo nchini Ghana katika mchezo wa marudiano.
Yanga itahitimisha mechi zake za Kundi A Kombe la Shirikisho kwa kumenyana na wenyeji TP Mazembe ya DRC mjini Lubumbashi Agosti 23, mwaka huu.
Mazembe inaongoza Kundi A kwa pointi zake 10 baada ya mechi nne, ikishinda tatu na kutoa sare moja, ikifuatiwa na Bejaia na Medeama, ambazo kila moja ina pointi tano za sare tatu na ushindi mmoja, wakati Yanga inashika mkia kwa pointi yake moja.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI