Nimeonja raha na karaha ya spidi ndogo ya mabasi ya mikoani

Na Richard Mwaikenda,Mbarali

Nimeonja chungu ya spidi ndogo ya mabasi na hatimaye raha ya usalama wa maisha yangu nilipoanza safari kutoka Stendi Kuu ya Ubungo, Dar es Salaam kwenda Mbarali, mkoani Mbeya.

 Lengo langu la safari ni kwenda Rujewa,wilayani Mbarali, Mbeya kuripoti tukio kubwa hapa nchini na duniani la Kupatwa kwa Jua leo Septemba Mosi.

Kama kawaida niliamka mapema saa 10 alfajiri nyumbani kwangu kivule, Ukonga, tayari kuwahi daladala ya kuniwahisha Stendi ya Ubungo, ili nipande mabasi ya kwenda Mbeya.

Nilipoteremka Kituo cha Riverside Ubungo mara nikavamiwa na wapiga debe wa mabasi huku kila mmoja akinishawishi kupanda basi lake, lakini nikaepukana na bughudha  zao kwa kuwaambia waniache ninayo tiketi, ingawa sikuwa nayo.

Usipojiamini na kuwa na msimamo, wapiga debe na makondakta wa mabasi ya mikoani, watakusumbua kwa kukusukasuka yaani kwa lugha rahisi watakugombea kama mpira wa kona ili mradi kila mmoja akitaka usafiri na basi lake.

Watu hao wasivyo na staha wengine wanadiriki hata kunyang'anya mizigo ya abiria ili wawafuate kwenda kupanda gari lao hata kama hutaki.

Lakini mimi niliepukana  na adha  hiyo nikapanda bodaboda hadi stendi ya Ubungo ambayo ipo umbali wa takribani kilomita moja hivi, ambapo kabla ya kudakwa tena na wapiga debe nikatumia mbinu ileile kwamba wasipoteze muda kwani nina tiketi tayari.

Baada ya muda nikiwa nimesogelea vibanda vya kukatia tiketi majira ya saa 11:50 asubuhi, nikamkubalia dada mmoja mpigadebe ambaye alinijia kwa unyenyekevu na kunishawishi kwenda kukata tiketi katika basi la Majinjah Special lililokuwa linakwenda Mbeya.

Nikakatiwa tiketi ya kuteremkia Igawa njia panda ya kwenda Rujewa, wilayani Mbarali ambako jua linapatwa na mwezi.

Nikapanda basi hilo na kuanza safari majira ya saa 12:30, lakini ikawa vigumu basi hilo kutoka haraka Ubungo kutokana na msongamano mkubwa wa mabasi ambayo kila dereva alikuwa akigombea kuwahi kutoka.' Ilituchukua zaidi ya dakika 15 kuingia Barabara Kuu ya Morogoro.

Baada ya basi kuingia barabarani nikashangaa mabasi hayo kuruhusiwa kupita kwenye njia ya mabasi ya mwendo kasi hadi mataa ya Ubungo ambapo walikuwepo matrafiki lakini bila kuwachukulia hatua.Nikajiaminisha kwamba watakuwa wameruhusiwa.

Karaha ya mwendo mdogo wa mabasi hayo ilianzia Ubungo ambapo nikajua kuwa huenda madereva wanafanya hivyo kutokana na kuwepo foleni ya magari.

Lakini cha ajabu ni kwamba madereva wengi wa mabasi walikuwa  wanatii sheria bila shurti kwani walionekana wakiendesha kuanzia spidi ya Kilomita kati ya 30, 50 hadi 80 kwa saa.

Walikuwa wakipunguza mwendo kulingana na maelekezo ya spidi zilizopo kwenye alama za barabarani ambapo miji midogo na ya kati ilikuwa km 30-50 kwa saa na pasipo na mji Km 80 kwa saa. Mabasi tuliyoongozana nayo ni New Force, FM Safari Highclass, Kidinio na Rungwe Express.

Mimi siku zote nikisafiri  kwenda mikoani kwa basi kupitia Morogoro ilikuwa tunatumia masaa matatu kutoka Dar es Salaam, lakini juzi mabasi hayo yaliyoondoka Ubungo saa 12:30 yalifika  Mji Kasoro Bahari saa 4:30 hivyo kuwa nyuma ya lisaa limoja.

Pia, kwa mwendo huo wa spidi ndogo ulinifanya niamini kwamba hivi sasa elimu ya usalama barabarani imewafikia vizuri madereva na wananchi kwa ujumla, kwani ndani ya basi hakuna hata abiria mmoja aliyesikika akipiga kelele kwamba tunachelewa kutokana na mwendo huo, kama ilivyozoeleka siku za nyuma.

Siku za nyuma mabasi yalikuwa yanatumia masaa 6 hadi 7 kutoka Dar es Salaam kwenda Iringa Mjini, lakini cha ajabu  jana mabasi yaliyotoka Dar es Salaam saa 12:30 yalipita njia panda ya Iringa Mjini majira ya saa 9:15 alasiri hivyo kutumia masaa 9 badala ya muda huo.

Pia, nilishuhudia jinsi askari wa usalama barabarani  walivyokuwa wamejipanga katika baadhi ya vituo na miji tangu tulipokuwa tunatoka Dar es Salaam hadi Iringa huku wakionekana kudhibiti muda wa mabasi hayo kuondoka na kufika katika miji mbalimbali, lakini vile vile kuangalia na makosa mengine.

Vile vile nilifurahishwa na kitendo cha mabasi hayo kusimama maeneo muafaka hasa katika baadhi ya hoteli kuwapa fursa abiria kwenda maliwatoni kujisaidia, si kama ilivyozoeleka siku za nyuma ambapo yalikuwa yanasimama popote na kuwaruhusu abiria kwenda kuchimba dawa vichakani.

Lakini nilibaini kwamba pamoja na yote hayo, inapaswa Trafiki kuwapa uelewa zaidi abiria wa kufunga mikanda, vile vile makondakta kila mara  basi linapoanza safari wawe wanawakumbusha abiria kufanya hivyo. Ikibidi Trafiki wawe wanaingia kwenye basi kukagua hilo.

Wakati tunakaribia kuingia  Mji wa Mbuyuni mpakani mwa mikoa ya Morogoro na Iringa,Trafiki aliliposimamisha basi, nilishuhudia akiwasihi abiria wasishuke kwenda kuchimba dawa vichakani kwa kuwaeleza kuwa hairuhusiwi ama sivyo basi litapigwa faini na abiria wenyewe kkuendana na sheria zilivyo sasa.

Pamoja na mwanzo kutofurahishwa na mwendo mdogo wa mabasi hayo, lakini kadri tulivyokuwa tunasonga mbele nilianza kufarijika na mwendo huo kwani ulituhakikishia safari yetu kuwa salama na kwa kiasi kikubwa kuondoa hofu ya uwezekano wa kupata ajali.

Madereva Wakiendelea kutii sheria za usalama barabarani, basi kuna uwezekano mkubwa wa kuepukana na ajali, hivyo kuokoa maisha ya watu waliokuwa wanakufa katika ajali hizo na wengine kujeruhiwa na kupata vilema vya kudumu.
0

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

HIVI NDIVYO BIASHARA YA NGONO NAMNA INAVYOTIKISA MOROGORO: SEHEMU YA PILI.

ANGALIA PICHA NDEGE KUBWA YA ABIRIA DUNIANI ILIYOANZA SAFARI NDEFU ZAIDI!

WAPENZI WANASANA WAKIFANYA MAPENZI GESTI

IJUE HISTORIA YA UHASIMU WA KOREA KASKAZINI NA MAREKANI

LICHA YA UZURI WAKE MWANADADA ELIZABETH MICHAEL a.k.a LULU SI MALI KITU MBELE YA RAY, AMKWEPA KUOGOPA AIBU.

KWA HERI KAMANDA WETU ABBAS KANDORO

DC MJEMA AONJA ADHA YA MAFURIKO AKIKAGUA ATHARI ZA MAFURIKO ILALA

YANGA SC WAANZA KAZI AFRIKA LEO…WANAKIPIGA NA U.S.M. ALGER SAA 4:00 USIKU ALGERIA

NCHI YA URUSI NDIYO NCHI INAYOONGOZA KWA KUWA NA UBORA WA ELIMU NA VYUO DUNIANI.