TACAIDS YAWATAKA WADAU WA MAPAMBANO DHIDI YA UKIMWI



Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS Dkt. Leonard Maboko akizungumza na wadau mbalimbali walio katika Mapambano dhidi ya Ukimwi leo jijini Dar es salaam. Mkurugenzi huyo amekutana na wadau hao kwa mara ya kwanza kuzungumza nao kuhusu mikakati mbalimbali ya kudhibiti Ukimwi.

Wadau kutoka mashirika na taasisi mbalimbali zinazojihusisha na mapambano dhidi ya Ukimwi wakifuatilia kwa makini hotuba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS Dkt. Leonard Maboko alipokuwa akizungumzanao leo jijini Dar es salaam.

Na. Aron Msigwa –  Dar es salaam.

Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS) imewataka baadhi ya wadau, mashirika na taasisi zilizo katika mapambano dhidi Ukimwi kuzingatia malengo ya awali ya kuanzishwa kwa taasisi hizo  na kuepuka kujiingiza katika shughuli za uanaharakati ambazo ni kinyume cha sheria.

Akizungumza katika kikao chake cha kwanza na wadau mbalimbali walio katika mapambano dhidi ya Ukimwi leo jijini Dar es salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS Dkt. Leonard Maboko amesema kuwa baadhi ya wadau, mashirika na taasisi zimekuwa zikifanya shughuli nje ya malengo ya awali ya kuanzishwa hali inayosababisha mgongano katika jamii.

"Zipo baadhi ya taasisi zinazofanya shughuli nje ya malengo, tunatambua Serikali haijakataa jitihada za makundi mbalimbali ya kupambana na UKIMWI, sisi kama TACAIDS tutaendelea kuungana na Serikali kuhakikisha kuwa zile taasisi zilizo kwenye mapambano zinasimamia malengo ya kuanzishwa kwake na si vinginevyo"  Amesisitiza Dkt. Maboko.

Amewataka wadau na mashirika hayo kuendelea kujikita na kuongeza nguvu katika utoaji wa elimu ,uhamasishaji wa wananchi kupima kwa hiari VVU kwa lengo la kujua hali zao  ili waweze kujikinga na maambukizi  mapya ya  ugonjwa huo.

Pia amewata wadau hao kuangalia namna bora ya kuwafikia, kuwaelimisha na kuwafuatilia wananchi walio katika makundi maalum kwenye mazingira hatarishi pia kuongeza shughuli za utafiti zitakazoisaidia nchi kufikia lengo la maabukizi sifuri.

Amesema hali ya uelewa wa wananchi juu ugonjwa wa Ukimwi imefikia asilimia 90 kwa kuwa watanzania sasa wanauelewa kuhusu ugonjwa huo na hali zao . Aidha, wengi wana uelewa iwapo wamepata maambukizi au la kutokana na kuongezeka kwa kampeni za uhamasishaji na elimu ya kujikinga na maambukizi.

Kwa upende wake Mkurugenzi wa Chama cha Uzazi na Malezi Bora Tanzania (UMATI), Lulu Ng’wanakilala amesema Taasisi zinazosajiliwa kutoa huduma za kuzuia na kupunguza maambukizi dhidi ya Ukimwi nchini Tanzania na kuanza kujiingiza kwenye shughuli za uanaharakati zinakwamisha na kupunguza juhudi za Serikali na wadau wengine wenye mapenzi mema walio kwenye mapambano dhidi ya Ukimwi.

‘Sisi kama wadau wa hizi taasisi tunaongea lugha moja, NGOs zinazosajiliwa kutoa huduma na kuanza kufanya uanaharakati kupitia masuala ya Ukimwi zinakwenda kinyume cha maelengo,sisi tupo kwa lengo moja kuhakikisha maambukizi yanafikia sifuri kwa kuhakikisha wote wanaotakiwa kupata huduma wanafikiwa na huduma zetu hasa makundi yanayochangia kwa kiasi kikubwa maambukizi ya Ukimwi’ Amesisitiza.

Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa Baraza la Watu Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi Tanzania (NACOFA) Bw. Deogratius Peter, akizungumzia hatua ya baadhi ya taasisi kuenenda kinyume na malengo ya kuanzishwa kwake amesema

‘Serikali imeshatoa Sera na miongozo mbalimbali inayosimamia shughuli za utoaji wa huduma za mapambano dhidhi ya Ukimwi kwa taasisi, makundi na wadau mbalimbali,  Sisi pamoja na Serikali tunakubali na kuheshimu juhudi za makundi haya katika mapambano dhidi ya Ukimwi, suala la uanaharakati halikubaliki maadili lazima yazingatiwe katika utoaji wa huduma zetu tufuate sheria za nchi ile kuepusha migongano isiyo ya lazima’ Amesisitiza.

Ameongeza kuwa taasisi zote zilizo katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi lazima zikajikite katifa tafiti pia kuyafuatilia makundi yote yaliyo katika mazingira hatarishi ambayo yanachangia  kwa kiwango kikubwa kueneza maambukizi ya VVU.


       

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI