MUSEVENI ANALIPENDA UA LA BOGA( WINNIE), ANALICHUKIA BOGA ( BESIGYE)...!


Ndugu zangu,
Mvuto kwenye kisa cha Yoweri , Winnie na Kiiza unatokana na ukweli, kuwa Yoweri Museveni hakuitarajia adhabu ya yeye ' kulisaliti' pendo la Winnie kwake iwe kwa Winnie kutembea na Kizza Besigye, rafiki wa zamani wa Yoweri Museveni.
Juzi tuliona jinsi Winnie alivyoingia kwenye maisha ya Museveni.
Kiukweli, Museveni wa sasa bado anaonyesha kumpenda Winnie, lakini, anamchukia Besigye, mume wa Winnie.
Ni Winnie aliyeacha kazi yake yenye maslahi makubwa , Uganda Airlines, mwaka ule wa 1981 na kujiunga na NRA akishawishiwa na Museveni.
Winnie na Museveni ujanani wamekulia nyumba moja kwenye familia ya Boniface Byanyima, baba wa Winnie. Ni wazazi wa Winnie waliomtunza Museveni ikiwamo kumlipia ada ya shule yake. Hivyo, Winnie na Museveni wamefahamiana kwa miaka mingi.
Msituni, kwenye mapambano ya NRA dhidi ya Obote na baadae akina Tito Okello, Winnie ndiye alikuwa kando ya Museveni. Ni takribani miaka mitano. Wakawa wapenzi. Na mtoto wamepata.
Bila shaka, Winnie alitarajia safari yao, yeye na Museveni, ya kutoka msituni na kuingia Kampala mwaka 1986 ingemfikisha pia kwenye Ikulu ya Entebbe akiwa mke wa Rais.
La hasha, Yoweri Museveni akafanya mipango ya kumrudisha Janet, mke wake wa ndoa aliyekuwa akiishi Gothernburg, Sweden na akitunzwa na Serikali ya Sweden.
Machungu ya kuachwa na Museveni na kumwona Janet akichukua nafasi yake yalipelekea Winnie kubaki mpweke.
Hata hivyo, Museveni hakumtupa mpenzi wake wa zamani, alihakikisha anampa nafasi ya kwenda kutumikia Ubalozini, Paris. Huko Winnie aliwahi hata kukaimu nafasi ya Balozi.
Ikafika siku Winnie akapokea simu kutoka kwa Kiiza Besigye aliyekwenda ziara ya kikazi Marekani na alitaka kurudi Uganda kwa kupitia Paris.
Wakati huo huo, kamanda mwenzao tangu enzi wakiwa msituni Major Victor Bwana, alipelekwa Paris kupatiwa matibabu baada ya kupata ajali mbaya Uganda.
Winnie aliachwa akihangaika na mgonjwa huyo ikiwamo kutafuta fedha za kulipa gharama za hospitali kule Ufaransa. Winnie hata pamoja na kumpigia simu Museveni mara kwa mara, lakini hakupata msaada uliohitajika.
Ujio wa Kanali Kiiza Besigye Paris ulimfanya Winnie asimulie yote. Kiiza alionekana kuguswa sana na mateso ya mpiganaji mwenzao, Major Victor Bwana, na akahidi, akirudi Kampala, atahangaikia kupata ufumbuzi.
Kwa mujibu ya maelezo ya Winnie Byanyima, tangu hapo, alimwona Kiiza Besigye kuwa ni mtu anayejali, mtu mkweli na mtiifu. Maana, aliporudi Kampala, Kiiza alianza kulifanyia kazi suala la mpiganaji mwenzao Major Bwana. Kiiza Besigye alianza kwa kuwatunza watoto walioachwa Uganda wa mpiganaji mwenzao Bwana.
Winnie Byanyima anasema;
" Kiiza alikuwa mtu pekee aliyemkumbuka Major Bwana. Iligusa moyo wangu kumwona mtu akiwa mkweli na mtiifu. Hivi ndiyo Besigye alivyoushinda moyo wangu. Unaushinda moyo wangu kwa mambo ya kikanuni. Unapaswa uongee na moyo wangu. Ndivyo alivyofanya Besigye." ( Source:Kizza Besigye and Uganda’s Unfinished Revolution © Daniel Kalinaki 2014.)
Kinachomsumbua Museveni leo ni ukweli, mpinzani wake, Kiiza Besigye ndiye aliye na mpenzi wake wa zamani, Winnie Byanyima.
Winnie anamjua vilivyo Museveni, na Museveni analijua hilo. Kwanba Winnie anajua nguvu na udhaifu wa Museveni. Yumkini Museveni alimtelekeza Winnie kwa ' Sababu za kiitifaki'. Lakini, Museveni ameshindwa kuficha kuwa bado ana mapenzi kwa Winnie, na kuwa anamheshimu Winnie kwa uwezo na ujasiri wake mkubwa. Museveni anajua pia, kuwa Winnie, kutokana na uwezo wa kiakili na sifa nyingine za kiuongozi, ni mwanamke aliyechangia kumfikisha Museveni Ikulu ya Entebbe.
Winnie, aliyekaa akitibu majeraha ya mahaba kwa miaka mitano baada ya 1986 kutupwa kando na baadae kukutana na Besigye miaka ya 90 mwanzoni, alikerwa na anaendelea kukerwa na tabia ya Museveni kumwandama mume wake wa sasa, Kiiza Besigye.
Yaweza kabisa kusemwa, Museveni wa leo hawezi kumfanya lolote baya Besigye kwa sababu ya Winnie, mzazi mwenzake. Winnie, mwenye uwezo wa kumkemea Museveni hadharani na asiogope kufanywa chochote na Museveni.
Na ajabu ya Winnie, Museveni na Besigye ni kuwa, pamoja na Winnie kuwa upande wa upinzani, Museveni amemtunuku Winnie nishani kadhaa za kitaifa, lakini, Besigye hajawahi kutunukiwa na Museveni hata nishani moja ya makaratasi!
Ndio maana ya kusema, kuwa Museveni analipenda ua la boga, lakini analichukia boga!
Maggid.
0

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

HIVI NDIVYO BIASHARA YA NGONO NAMNA INAVYOTIKISA MOROGORO: SEHEMU YA PILI.

WAPENZI WANASANA WAKIFANYA MAPENZI GESTI

LICHA YA UZURI WAKE MWANADADA ELIZABETH MICHAEL a.k.a LULU SI MALI KITU MBELE YA RAY, AMKWEPA KUOGOPA AIBU.

ANGALIA PICHA NDEGE KUBWA YA ABIRIA DUNIANI ILIYOANZA SAFARI NDEFU ZAIDI!

MATOKEO YA DARASA LA SABA YATANGAZWA

ZIARA YA KATIBU MKUU WA CCM NDUGU KINANA NDANI YA CHAKE CHAKE,MKOA WA KUSINI PEMBA LEO.

IJUE HISTORIA YA UHASIMU WA KOREA KASKAZINI NA MAREKANI

NCHI YA URUSI NDIYO NCHI INAYOONGOZA KWA KUWA NA UBORA WA ELIMU NA VYUO DUNIANI.

TFF YATANGAZA MAJINA YA WACHEZAJI 30 WATAKAOWANIA TUZO YA MCHEZAJI BORA MSIMU HUU