WAZIRI MKUU AELEZA MIKAKATI YA SERIKALI KUIPANGA DODOMA ISIWE KAMA DAR ES SALAAM


Waziri Mkuu Majaliwa Akisalimiana 
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imeunda timu ya wataalamu ambao watatoa ushauri juu ya suala zima la kuhamishia makao makuu Dodoma.Ametoa kauli hiyo jana mchana (Jumamosi, Oktoba 1, 2016) wakati akizungumza na watumishi wa Serikali wa mkoa wa Dodoma, wazee wa mkoa huo, wafanyabiashara pamoja na viongozi mbalimbali kwenye ukumbi wa mikutano wa Dodoma (Dodoma Convention Centre).
“Tumeunda timu ya watu 10 ambao ni wataalamu waliobobea kwenye masuala ya ujenzi wa miji mikuu, hawa wana uzoefu wa kuangalia makao Makuu ya nchi yanafananaje. Watakuja Dodoma, wapitie master plan na kisha watapita kwenye maeneo kadhaa ya mji ili waone hali halisi ikoje ndipo watupe maoni yao,” amesema.
“Tunataka tusirudie kosa la Jiji la Dar es Salaam la kulazimika kubomoa makazi ya watu kila inapolazimu kufanya uboreshaji wa miundombinu. Hawa watu watatuambia wapi tunatakiwa tuweke njia nne au sita za magari, wapi tuweke bustani au wapi tujenge nyumba za ghorofa moja, mbili, tatu au zaidi,” ameongeza.
Akifafanua kuhusu miundombinu, Waziri Mkuu amesema timu hiyo pia itatakiwa kutoa ushauri juu ya wapi ijengwe njia ya malori tu au mahali gani zinahitajika kujengwa barabara za juu (flyovers) ili kuepusha msongamano katikati ya mji wa Dodoma.
Bila kutaja majina ya wajumbe wa timu hiyo, Waziri Mkuu amesema timu hiyo itaongezewa wataalamu kutoka China na Malaysia ambao nchi zao tayari zina uzoefu wa kuhamisha makao makuu ya nchi zao zaidi ya mara moja.
Alitumia fursa hiyo kuwaeleza watumishi juu ya uwepo wa Tume ya Kuboresha Maslahi ya Wafanyakazi ambayo imekuwa ikifanya kazi tangu mwaka jana. “Kuna vikao vimekuwa vinafanyika tangu mwaka jana baina ya Serikali na viongozi wa vyama vya wafanyakazi kwa lengo la kujadili uboreshaji wa maslahi ya wafanyakazi, na jambo hili linaendelea vizuri,” amesema.
Kuhusu madeni ya watumishi wa umma, Waziri Mkuu amewasihi watumishi wawe na imani na Serikali yao kuhusu madeni hayo na kwamba ikimaliza uhakiki unaofanyika hivi sasa, kila mwenye stahili zake atalipwa.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameutaka uongozi wa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) ihakikishe inakamilisha upimaji wa viwanja 100,000 kama ilivyojipangia ili watumishi hao pamoja na wananchi waweze kupatiwa viwanja haraka iwezekanavyo.
“Nimearifiwa kuwa mna mpango wa kupima viwanja 100,000 kwa ajili ya kuwapatia wananchi na watumishi. Kamilisheni utaratibu huo haraka ili watumishi wapewe viwanja na waweze kujenga nyumba zao za kuishi,” amesema huku akishangiliwa.
Natambua kuwa mmekubaliana kuanzisha utaratibu wa kuingiza viwanja kwenye mfumo wa kompyuta ili kuepuka double allocation. Harakisheni zoezi hilo ili kama itawezekana, kabla ya Novemba kazi hiyo iwe tayari na watu wapatiwe viwanja chini ya mfumo huo mpya,” amesisitiza.
Kuhusu huduma za kijamii kama elimu, umeme, maji na masoko, Waziri Mkuu amewahakikishia watumishi hao kwamba Serikali imeangalia kila eneo na kuzingatia mapendekezo yaliyotolewa ili kuboresha utoaji wa huduma hizo. Amewataka watumishi hao wabadilike na wawe tayari kuwapokea watumishi wenzao watakaowasili kwa awamu kuanzia mwezi huu.


IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI