AJALI ZA VIFO ZAPUNGUA KWA ASILIMIA ISHIRINI NA NNE

JALI ZA VIFO ZAPUNGUA KWA ASILIMIA ISHIRINI NA NNE

Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha

Katika kipindi cha toka Januari mpaka Oktoba mwaka 2016 ajali za vifo zimepungua kwa asilimia ishirini na nne ukilinganisha na kipindi kama hicho mwaka 2015, ambapo kulikuwa na jumla ya ajali za vifo 74 tofauti na mwaka huu kumekuwa na ajali 56 ambapo ni sawa na upungufu ya ajali 18 ambazo ni 24% .

Akitoa takwimu hizo katika sherehe za uzinduzi ya wiki ya nenda kwa Usalama Barabarani zilizofanyika katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Mkuu wa kikosi cha Usalama Barabarani mkoani hapa Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Nuru Kacharia alisema kwamba katika ajali hizo 74 kwa mwaka 2015 jumla ya watu 97 walipoteza maisha na mwaka huu 2016 kwa kipindi kama hicho ajali hizo ni 56 ambazo zilisababisha vifo vya watu 68.
Askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani Koplo Athilio Choga akimuelezea mgeni rasmi mkuu wa wilaya ya Arusha Mh. Gabriel Daqarro (Mwenye suti) namna ya mpangalio wa mji unavyoweza kupanua barabara ili kuepukana na ajali.

Kacharia aliendelea kubainisha kwamba, mbali na upungufu wa ajali za vifo lakini kikosi hicho cha Usalama Barabarani kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wameweza pia kupunguza ajali za majeruhi kwa 5% ambapo mwaka 2015 kuanzia Januari hadi Oktoba ajali zilizosababisha majeruhi zilikuwa 763 tofauti na ajali zilizosababisha majeruhi 725 kwa kipindi kama hicho kwa mwaka huu wa 2016.

“Asilimia 75 ya ajalli za barabarani zinasababishwa na wanadamu kwa kutotii sheria za barabarani, madereva kuendesha vyombo vya usafiri wakiwa walevi, kuendesha kwa mwendokasi, watembea kwa miguu na waenda mikokoteni kutofuata sheria”. Alifafanua Mkuu huyo wa Usalama Barabarani.

Alisema mbali na makosa ya kibinadamu lakini pia, ubovu wa vyombo vya usafiri kama vile uchakavu wa magurudumu na kadhalika husababisha ajali kwa asilimia kumi na tano pamoja namiundo mbinu ya barabarainachangia kwa asilimia kumi.
Mkuu wa kikosi cha Usalama Barabarani mkoa wa Arusha (SSP) Nuru Kacharia akitoa takwimu juu ya hali ya usalama barabarani kwa wananchi wa Arusha wakati wa uzinduzi ya wiki ya nenda kwa usalama barabarani iliyofanyika jana katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.

Alisema kwamba kwa mwaka huu wa 2016 Kikosi cha Usalama Barabarani kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa vyuo vya udereva wameweza kutoa elimu kwa jumla ya wadereva 73,830 wa vyombo vya usafiri, huku vituo 2,149 vya pikipiki wanachama wake walipata elimu sahihi ya matumizi ya barabarani, na kuongeza kwamba jumla ya vipindi 624 vya redio sawa na dakika 18,720 zilitumika katika kuwaelimisha watumiaji wa barabara  kwa mwaka huu wa 2016.

Akizindua rasmi wiki ya nenda kwa Usalama Barabarani mkoani hapa, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha mara baada ya ukaguzi wa vibanda mbalimbali vilivyomo ndani ya uwanja huo, Mkuu wa wilaya ya Arusha Mh. Gabriel Daqarro alisema kwamba ajali za barabarani zimeendelea kugharimu maisha ya watu wengi hivyo kuathiri ustawi wa jamii pamoja na uchumi kwa ujumla.
Kamanda wa polisi Mkoa wa Arusha Naibu Kamishna (DCP) Charles kumbo akitoa shukrani kwa wadau wa kampuni mbalimbali wakiwemo na waandishi wa habari katika kufanikisha sherehe za wiki ya nenda kwa usalama barabarani.

Alisema kila mmoja wetu anapaswa kuchukua hatua ili kupunguza ajali na kuiagiza kamati na taasisi husika kuweka mikakati madhubuti kama vile kupendekeza marekebisho ya sheri za usalama barabarani, wakala wa barabara waweke alama za barabarani ili zitoe uelewa sahihi kwa watumiaji wa barabara na kuliomba Jeshi la Polisi washirikiane na wadau wengine liweze kutoa mafunzo ya mara kwa mara hasa kwa waendesha pikipiki ili ajali hizo ziweze kupungua.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Naibu Kamishna (DCP) Charles Mkumbo ambaye pia ni mlezi wa Kamati ya Usalama Barabarani alisema kwamba, kamati hiyo itatekeleza yote yaliyoagizwa na Mkuu wa Mkoa na kuwashukuru wadau wote pamoja na vyombo mbalimbali vya habari kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kikosi cha Usalama barabarani na kuahidi kuongeza jitihada za kila aina ili kuweza kupunguza ajali .

Katika sherehe hizo za uzinduzi zilizokuwa na kauli mbiu “Hatutaki ajali tunataka kuishi salama” Jeshi la Polisi liliwatunuku vyeti wadau mbalimbali pamoja na Mtangazaji wa kituo cha Televisheni cha  Star TV mkoani hapa Ramadhani Mvungi na Radio Triple “A” kwa kutoa mchango mkubwa katika uelimishaji wa jamii juu ya Usalama Barabarani mkoani hapa.
Askari wa Brass Bendi ya Polisi toka Chuo cha Polisi Moshi wakiwa wanatoa heshima jukwaani wakati wakipita mbele ya mgeni rasmi Mh. Gabriel Daqarro mkuu wa wilaya ya Arusha wakati wa uzinduzi ya wiki ya Nenda kwa usalama Barabarani mkoani hapa.
Mkuu wa wilaya ya Arusha Mh. Gabriel Daqarro (aliyekaa katikati mwenye suti) ambaye alimwakilisha Mkuu wa mkoa kwenye uzinduzi ya wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani mkoani Arusha akiwa katika picha ya pamoja na wadau mbalimbali.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

ALLY KAMWE AZIMIA KWA MKAPA.

RAIS SAMIA KUZINDUA MKUTANO MKUU WA 79 WA BARAZA LA MICHEZO YA MAJESHI DUNIANI

MIGINGO KISIWA KIDOGO ZAIDI AFRIKA KILICHOGOMBEWA NA UGANDA, KENYA