AZAM YASAJILI WASHAMBULIAJI WAWILI HATARI KUTOKA GHANA


Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
KLABU ya Azam FC imefanikiwa kuingia mikataba na washambuliaji nyota kutoka Ghana, Samuel Afful na Yahaya Mohammed.
Taarifa ya Azam FC imesema kwamba, wachezaji hao wamesaini mikataba mbele ya viongozi wakuu wa timu wakiwemo Ofisa Mtendaji Mkuu, Saad Kawemba, Meneja Mkuu, Abdul Mohamed, Kocha Mkuu Zeben Hernandez Rodriguez na wakala anayewasimamia wachezaji hao, Kingsley Atakorah, ambaye pia ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Adom Wonders Academy ya nchini Ghana.
Samuel Afful (kushoto) na Yahaya Mohammed (kulia) wakiwa na kocha Hernandez baada ya kusaini
Viongozi mbalimbali wa Azam FC wakiwashuhudia wachezaji hao wakisaini leo

Wakati Afful, 20, akisaini mkataba wa miaka mitatu, Mohammed aliyetua nchini leo mchana akitokea Ghana naye amesaini kandarasi ya miaka miwili tayari kabisa kuanza kuitumikia timu hiyo yenye maskani yake Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Afful ambaye mpaka sasa yumo katika vikosi vya timu za vijana za Ghana chini ya umri wa miaka 20 na 23, anajiunga Azam FC akitokea timu ya Sekondi Hasaacan ya Ghana, ambayo aliifungia mabao tisa timu hiyo msimu uliopita.
Moja ya rekodi yake ni kuifungia bao muhimu timu ya Taifa ya Ghana chini ya umri wa miaka 20 (U-20) mwaka jana dhidi ya Zambia kwenye ushindi wa mabao 2-1, lililoipa nafasi ya kushiriki fainali za Kombe la Dunia nchini New Zealand, baada ya kutinga nusu fainali ya Mataifa ya Afrika kwa Vijana (U-20) zilizofanyika Senegal mwaka jana.
Mohammed, 28, ambaye ni mshambuliaji mzoefu anayetokea Aduana Stars, alikuwa ni mfungaji bora namba mbili wa Ligi Kuu ya Ghana msimu uliopita akifunga mabao 15, pungufu ya mabao mawili na kinara Latif Blessing (Liberty Proffessional) aliyetupia 17.
"Azam FC tunaamini ya kuwa ujio wa nyota hao, utazidi kuipa nguvu timu yetu kuelekea kwenye michuano inayotukabili mbeleni, mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), Kombe la Kagame (CECAFA Kagame Cup) tukiwa kama mabingwa watetezi, Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) na Kombe la Shirkisho Afrika (CC) mwakani,"imesema taarifa ya Azam.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*