Ndege iliyobeba wachezaji wa timu ya soka ya Brazil yaanguka Colombia



Mabaki ya ndegeImage copyrightTELEANTIOQUIA VIA TWITTER
Image captionNdege hiyo ilianguka eneo lenye milima mingi ikielekea Medellin
Ndege iliyokuwa imewabeba watu 81, wakiwemo wachezaji na maafisa wa moja ya klabu kubwa za soka nchini Brazil, imeanguka ikikaribia mji wa Medellin nchini Colombia na kuua watu 76.
Polisi wamesema watu watano walinusurika lakini watu wengine wote waliangamia.
Ndege hiyo ya kukodishwa ilikuwa safarini kutoka Brazil ikipitia Bolivia na ilikuwa imewabeba wachezaji na maafisa wa timu ya Chapecoense.
Klabu hiyo ilikuwa imepangiwa kucheza mechi ya fainali ya Copa Sudamericana, dhidi ya timu ya Atletico Nacional ya mji wa Medellin.
Mechi ya awamu ya kwanza ya kombe hilo, la pili kwa umuhimu Amerika Kusini, ilikuwa imepangiwa kuchezwa Jumatano lakini sasa imesitishwa.
Timu hiyo inayotoka mji wa Chapeco, kusini mwa Brazil, ilipandishwa kucheza ligi ya daraja ya kwanza nchini Brazil mwaka 2014 na ilifika fainali ya kombe hilo la Sudamericana kwa kulaza San Lorenzo ya Argentina.
Mechi hiyo ilikuwa inatazamwa kama kubwa zaidi katika historia ya klabu hiyo ndogo.
Shirikisho la Soka la Amerika Kusini (Conmebol) limesema kwamba limesitisha shughuli zake zote kwa sasa.
Taarifa zinasema ndege hiyo muundo wa British Aerospace 146 ambayo imekuwa ikitumiwa na shirika la ndege la Lamia la Bolivia ilikuwa na abiria 72 na wahudumu tisa.
Maafisa wa klabu hiyo ya Chapecoense wametoa taarifa wakisema: "Tunamuomba Mungu awe na wachezaji, maafisa, wanahabari na wageni wengine watu ambao walikuwa wameandamana na ujumbe wetu."
Wamesema hawatatoa taarifa nyingine hadi ibainike kiwango kamili cha mkasa huo.
Taarifa zinasema watu wawili kutoka kwa timu hiyo - Alan Ruschel na Danilo - huenda wamenusurika.
Telemundo Deportes wameandika kwenye Twitter kwamba Ruschel ameathiriwa na mshtuko lakini ana fahamu na anazungumza. Aidha, ameomba aruhusiwe kukaa na pete yake ya harusi na awaombe jamaa zake.
Timu hiyo ilipangiwa kucheza mechi ya awamu ya kwanza ya fainali ya Copa SudamericanaImage copyrightAFP
Image captionTimu hiyo ilipangiwa kucheza mechi ya awamu ya kwanza ya fainali ya Copa Sudamericana
Ndege hiyo ilianguka eneo la milimani nje kidogo mwa mji wa Medellin majira ya saa sita usiku saa za huko (saa mbili asubuhi Afrika Mashariki).
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa maafisa wa uwanja wa ndege, marubani walisema ndege hiyo ilikuwa imepata matatizo katika mfumo wake wa umeme.
Meya wa mji ulio karibu wa La Ceja amethibitisha kwamba mchezaji mmoja wa miaka 25 ni miongoni mwa manusura.
Ramani
Meya wa Medellin Mayor Federico Gutierrez amesema ajali hiyo ni "janga kubwa".
Maafisa wa uwanja wa ndege wa Jose Maria Cordova de Rionegro uliopo Medellin, wamesema juhudi zote zinafanywa kuwaokoa manusura.
Hali mbaya ya hewa inazuia maafisa kufikia eneo la mkasa kwa urahisi.
Hakukutokea moto baada ya ndege hiyo kuanguka, jambo ambalo linaibua matumaini ya kupatikana kwa manusura.
Eneo la ajaliImage copyrightMI ORIENTE
Image captionMaafisa wa uokoaji wanaweza tu kufika eneo la ajali kwa barabara

Klabu ya Chapecoense
  • Ilianzishwa 1973.
  • Ikapandishwa kucheza ligi ya daraja ya kwanza Brazilian, Serie A, mara ya kwanza 2014. Imo nambari tisa ligini kwa sasa.
  • Walikuwa wanaelekea kucheza fainali ya Copa Sudamericana, mshindi hufuzu kucheza Copa Libertadores, shindano kubwa la klabu Amerika Kusini.
  • Jiji lao la nyumbani ni Chapeco katika jimbo la Santa Catarina, Brazil


Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*