WAZIRI MAHIGA AKUTANA NA MABALOZI


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akisalimiana na Balozi Mteule wa Yemen nchini Mhe.Fikri Taleb Abubaker Al Sakaf mara baada ya kuwasili Wizarani kuwasilisha Nakala za Hati za Utambulisho 
Mhe. Waziri Balozi Dkt. Augustine Mahiga akionesha Hati za Utambulisho za Balozi Mteule wa Yemeni nchi Tanzania Mhe.Fikri Taleb Abubaker Al Sakaf mara baada ya kukabidhiwa 
aziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akisalimiana na Balozi Mteule wa Saudi Arabia nchini Tanzania Mhe. Mohammed Bin Mansoor Al Malyk alipowasili Wizarani Jijini Dar es Salaam kukabidhi Hati za Utambulisho 
Balozi Mteule wa Saudi Arabia nchini Tanzania Mhe. Mohammed Bin Mansoor Al Malyk akikabidhi Hati za Utambulisho kwa Mhe. Waziri Balozi Dkt. Augustine Mahiga Wizarani Jijini Dar es Salaam 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akiwa katika mazungumzo na Balozi wa Malawi nchini Tanzania Mhe. Hawa Ndolowe alipomtembelea Wizarani Jijini Dar es Salaam .
Mzungumzo yakiendelea, Kushoto ni Balozi Msaidizi wa Malawi nchini Tanzania Bw.Sai Kaphale na Kulia ni maafisa kutoka Wizarani wakifuatilia mazungumzo yalikuwa yakiendelea. 
Wakiwa katika picha ya pamoja 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akimsikiliza Balozi wa Japan nchini Tanzania Mhe.Masaharu Yoshida alipomtembelea kwa mazungumzo yaliyofanyika Wizarani Jijini Dar es Salaam 
Mazungumzo yakiendelea. Kushoto ni Maafisa kutoka Ubalozi wa Japan nchini Tanzania na kulia ni Maafisa kutoka Wizarani wakifuatilia mazungumzo yaliyokuwa yakiendelea .



JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI

Simu: 255-22-2114615, 211906-12
Barua pepe: nje@nje.go.tz
Barua pepe: gcu@nje.go.tz
Tovuti : www.foreign.go.tz

Nukushi: 255-22-2116600

              

 

            20 KIVUKONI FRONT,
            P.O. BOX 9000,
                  11466 DAR ES SALAAM, 
                                    Tanzania.
 


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushrikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (Mb), amepokea Nakala za Hati za Utambulisho za Waheshimiwa Mabalozi Wateule wa Nchi za Yemen na Saudi Arabia na baadaye kufanya mazungumzo na Waheshimiwa Mabalozi wa  Malawi na Japan leo ofisini kwake.

Wakati wa mazungumzo na Balozi Mteule wa Saudi Arabia, Mhe. Mohammed Mansour Al-Malik viongozi hao walisisitiza umuhimu wa Tanzania na Saudi Arabia kuimarisha uhusiano na ushirikiano hususan katika nyanja za biashara na uchumi. Dkt. Mahiga  alimweleza Balozi Mteule kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli alifurahishwa na ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia, Mhe. Adel Al Jubair  aliyoifanya nchini mwezi Machi 2016.  

Wakati wa ziara hiyo, Rais Magufuli aliomba Serikali ya Saudi Arabia kupitia Mfuko wa Serikali (Saudi Fund) kufadhili ukamilishwaji wa miradi mbalimbali ya barabara hapa nchini. Ombi hilo liliafikiwa na ujumbe kutoka Saudi Arabia ulifanya ziara nchini hivi karibuni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.

Rais Magufuli pia alitumia fursa hiyo kumualika Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo  kutembelea Hifadhi za Taifa zilizopo hapa nchini. Mhe. Waziri alikubali isipokuwa alisema atakuja wakati mwingine na mwanae wa kiume ambaye anapenda sana kuona paka wakubwa akimaanisha wanyama wakubwa kama simba, chui, tembo na faru.

Kwa upande wake, Balozi Mteule wa Saudi Arabia aliahidi kusimamia utekelezaji wa yote yaliyoafikiwa wakati wa ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi yake na masuala mengine yenye maslahi ya pande zote mbili.

Wakati wa mazungumzo na Balozi Mteule wa Yemen, Mhe.  Fikri Taleb Abubaker Al-Sakaf, wawili hao walisisitiza umuhimu wa kuimarisha uhusiano kati ya nchi hizi mbili. Waziri Mahiga alitumia fursa hiyo pia kuwaalika wafanyabiashara wakubwa kutoka Yemen kuja kuwekeza Tanzania. Alisema kuna wafanyabiashara wengi wenye asili ya Yemen wamefanikiwa kibiashara hapa nchini. 

Aliongeza kuwa historia inaonesha kwamba watu kutoka Yemen ndio walikuwa wa kwanza kufanya biashara za maduka ya bidhaa muhimu nchini ambao walikuwa na utaratibu wa kukopesha bidhaa na kulipa baadaye. Alisema watu hao kutoka Yemen pia ndio walikuwa na utaratibu wa kupeleka bidhaa hadi vijijini na kukopesha wateja wao ambao leo unatumiwa na wafanyabiashara wa Tanzania kwa jina maarufu wamachinga. 

Kwa upande wake, Balozi Mteule wa Yemen aliahidi kuwa atafanya kila awezalo kushawishi makampuni makubwa kutoka Yemen kuja kuwekeza nchini. Alisema kama watu wa Yemen walikuwa wanafanya biashara ndogo ndogo huko nyuma hapa nchini, kuna haja sasa ya kupanua wigo na kuingia katika biashara kubwa.

Wakati wa mazungumzo na Balozi wa Malawi, Mhe. Hawa Ndilowe, wawili hao walisisitiza pia umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya nchi hizi mbili. Aidha, Mhe. Ndilowe alimweleza Waziri Mahiga kuwa Malawi imejipanga kuandaa mkutano wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Malawi (JPC) mwezi Desemba 2016. Alieleza mara ya mwisho kufanyika mkutano huo ilikuwa mwaka 2003 nchini Tanzania, hivyo kuna umuhimu wa kuitisha mkutano huo ili kutoa fursa kwa wadau kujadili masuala mbalimbali ya ushirikiano pamoja na kutafuta mbinu za kukabiliana na changamoto zinazotukabili.

Waziri Mahiga alikaribisha uamuzi huo kwa furaha kwa kusema kuwa wakati wa mkutano huo itakuwa fursa nzuri ya kufafanua masuala mbalimbali ambayo yamefanyiwa mabadikiko na Serikali ya Awamu ya Tano, hususan katika sekta ya usafirishaji katika Bandari ya Dar es Salaam, mifuno ya ulipaji kodi, uhamiaji na biashara za mipakani.

Aliendelea kueleza kuwa Tanzania na Malawi zinatakiwa kushirikiana katika masuala ya ulinzi na usalama, hususan katika kukabiliana na mauaji ya watu wenye ualbino ambayo yameikumba nchi zao.

Katika mazungumzo yake na Balozi wa Japan hapa nchini, Mhe. Masaharu Yoshida, Waziri Mahiga alipongeza ushirikiano uliopo kati ya nchi hizi mbili ambao umejikita katika kuimarisha sekta mbalimbali ikiwemo miundombinu hapa nchini kwa ajili ya maendeleo. 

Aidha, akitoa maoni yake kuhusu Mkutano wa Sita wa Kimataifa kuhusu Ushirikiano wa Maendeleo kati ya Japan na Afrika (TICAD VI)  uliofanyika kwa  mara ya kwanza Afrika, Jijini Nairobi mwezi Agosti, 2016, Waziri Mahiga alisema mikutano hiyo ni jukwaa muhimu linalotoa fursa kwa nchi za Afrika na Japan kujadili maendeleo

Pia alipongeza agenda zilizojadiliwa kwenye mkutano wa TICAD VI ikiwemo kuhamasisha mageuzi ya kiuchumi kupitia uendelezaji wa viwanda; Kuboresha sekta ya Afya kwa maisha bora na kusaidia jitihada za kudumisha amani na utulivu katika jamii kwa ajili ya maendeleo ya Afrika.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 17 Novemba, 2016.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI

KOCHA WA AL.AHLY ASEMA YANGA NI TIMU BORA NA NGUMU