AZAM FC YAZINDUKA, YAILAZA 1-0 PRISONS CHAMAZI


Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, usiku wa jana imeiadabisha Tanzania Prisons kwa bao 1-0 katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) uliofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Mchezo huo ulikuwa ni wa mwisho kwa Azam FC mwaka huu kabla ya kuukaribisha mwaka mpya ‘2017’, bao hilo pekee limewekwa kimiani na nahodha John Bocco ‘Adebayor’, dakika ya 40 baada ya kupokea pasi safi ya Joseph Mahundi na kuwahadaa mabeki wa Prisons kisha kupiga shuti la kiufundi lililojaa kimiani.
Wachezaji wa Azam FC wakimpongeza Nahodha wao, John Bocco baada ya kufunga jana
Iddi Cheche (kushoto)  aliiongoza Azam jana kwenye mchezo wa jana

Azam FC iliingia kwenye mchezo huo ikiwa na sura mpya kwenye benchi la ufundi lililosimamiwa na makocha wa timu yake ya vijana, Idd Nassor 'Cheche' na Idd Abubakar na hii ni kufuatia kuwasitishia mikabata wakufunzi kutoka Hispania wakiongozwa na Kocha Mkuu, Zeben Hernandez.
Hiyo inamaanisha kuwa makocha hao wa muda wameanza kibarua chao vema kwa kujiandikia rekodi ya kuiongoza Azam FC kushinda mchezo wa ligi katika mechi yao ya kwanza wakiwa benchini.
Mabingwa hao wa Ngao ya Jamii waliuanza mchezo huo vema wakifanya mashambulizi kadhaa langoni mwa Prisons, lakini safu yao ya ulinzi ilikuwa imara kuondoa hatari zote wakiongozwa na Salum Kimenya.
Alikuwa ni Bocco aliyeihakikishia Azam FC bao la uongozi hadi dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamalizika.
Kipindi cha pili Azam FC iliongeza nguvu kwa kuwaingiza Shaaban Idd, Himid Mao na Samuel Afful, lakini jitihada za kusaka mabao zaidi zilishindikana kutokana na uimara wa safu ya ulinzi ya Prisons.
Kiungo Frank Domayo, alikaribia kuipatia bao la pili Azam FC dakika ya 50 akiwa anatazamana na kipa wa Prisons, lakini shuti aliloopiga lilitoka pembeni kidogo ya lango la wapinzani wao.
Dakika moja baadaye mshambuliaji wa Azam FC, Yahaya Mohammed, alifanya jitihada binafsi za kuwatoka mabeki wa Prisons lakini shuti alilopiga lilitoka nje ya lango la Prisons.
Prisons ilipata pigo dakika ya 69 baada ya kiungo wao mkabaji, Kazungu Mashauri, kuonyeshwa kadi nyekundu kufuatia kumfanyia madhambi ya makusudi winga wa Azam FC, Mahundi ambaye alishindwa kuendelea na mchezo huo na nafasi yake kuchukuliwa na nahodha msaidizi, Himid Mao.
Hadi dakika 90 zimalizika ubao wa matokeo ulikuwa ukisomeka vilevile na hivyo kufanya Azam FC kuondoka na pointi zote tatu zinazoifanya kufikisha jumla ya pointi 30 katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ikizidiwa pointi 14 na kinara Simba (44) na 10 kwa upande wa Yanga waliojikusanyia 40.
Huo ni ushindi wa kwanza wa Azam FC kwenye mechi za mzunguko wa pili wa ligi baada ya kuanza vibaya kwa kutoka sare mechi mbili mfululizo dhidi ya African Lyon (0-0) na Majimaji (1-1).
Azam FC kwa sasa inaelekea kwenye changamoto nyingine ya kushiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi, ambapo itaanza kufungua dimba Jumatatu ijayo kwa kucheza na Zimamoto saa 10.15 jioni ndani ya Uwanja wa Amaan, visiwani Zanzibar.
Kikosi cha Azam FC leo; Aishi Manula, Shomari Kapombe, Erasto Nyoni, Aggrey Morris, Yakubu Mohammed, Stephan Kingue, Salum Abubakar, Frank Domayo, Yahaya Mohammed/Shaaban dk 64, John Bocco/Samuel Afful dk90, Joseph Mahundi/Himid dk 71.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA