MAJAJI WANAOSHIRIKI KATIKA MAFUNZO YA KUBADILISHANA UZOEFU


Na Mary Gwera, Mahakama ya Tanzania.

Katika muendelezo wa mafunzo ya kubadilishana uzoefu juu ya uendeshaji wa mashauri ya jinai, Majaji wanaoshiriki katika mafunzo haya wapatiwa somo  juu ya Sheria ya Utakatishaji Fedha ‘Money Laundering.’ 

Akitoa somo hilo mapema jana, katika Ukumbi wa Hazina mjini Dodoma, Bw. Robert Kassim, ambaye ni Mwanasheria- Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu ‘Financial Intelligency Unit’ (FIU) - Wizara ya Fedha na Mipango alisema elimu juu ya Sheria hii kwa Wahe. Majaji inalenga katika kuendelea kuwajengea uelewa zaidi kutokana na kesi za aina hiyo kuletwa Mahakamani.
Mwanasheria, Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu, Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Robert Kassim akitoa somo juu ya elimu ya Utakatishaji Fedha kwa kundi la Wahe. Majaji wanaoshiriki katika mafunzo ya kuubadilishana uzoefu juu ya uendeshaji wa mashauri ya jinai yanayoendelea katika Ukumbi wa Hazina uliopo mkoani Dodoma.

“Kitengo cha Utakatishaji Fedha kinaendelea kutoa elimu kwa makundi mbalimbali ikiwa ni pamoja na Wapelelezi, Waendesha Mashitaka, Mabenki na Sekta nyingine ili wote kwa pamoja tuwe na uelewa wa pamoja dhidi ya vitendo hivi haramu ambavyo huchangia katika kurudisha maendeleo ya nchi nyuma,” Alisema Bw. Kassim.

Alisisitiza kuwa suala la Utakatishaji Fedha lina madhara mengi kwa Taifa, akitaja kuwa ni pamoja na kurudisha nyuma ushindani wa kiuchumi, kushusha hadhi na utengamano wa Taasisi za kifedha na mifumo yake, pia kufifisha uwekezaji wa mitaji ya kimataifa.
Waheshimiwa Majaji wakimsikiliza mtoa mada ya Utakatishaji Fedha.

Kwa upande wake, Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu-Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Mhe. Rehema Mkuye alisema kuwa somo hilo ni muhimu sana kulielewa zaidi, akifafanua kuwa kati ya mashauri ambayo Divisheni yake itashughulika nayo ni pamoja na Mashauri ya Utakatishaji fedha na uhujumu uchumi.

“ Somo juu ya Sheria hii ni muhimu, mafunzo kama haya ni vyema yakaendelea kutolewa zaidi na zaidi hata kwa makundi mengine kama Wapelelezi na watu tunaoshirikiana nao katika uendeshaji wa kesi ili kujenga uelewa wa pamoja na hatimaye kurahisisha usikilizaji wa mashauri ya namna hii,” alisisitiza Mhe. Mkuye.
Sehemu ya Majaji, wanaoshiriki katika mafunzo.

Naye, Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu, Kanda ya Tanga, Mhe. Iman Aboud, alisema kuwa kwa kuwa Mashauri ya Utakatishaji Fedha ni miongoni mwa Mashauri yenye maslahi kwa jamii ni vyema yakashughulikiwa kwa haraka kutokana na mvuto wake kwa jamii ‘public interest.’

“Miongoni mwa kesi ambazo jamii inapenda zishughulikiwe kwa haraka ni pamoja na kesi za Utakatishaji Fedha, hivyo uelewa zaidi juu ya Sheria hii ya Utakatishaji wa Fedha ni muhimu sana,” alisema Jaji Aboud.

Katika hatua nyingine, Jaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi alisema kuwa ujengaji wa uelewa wa pamoja kuhusu sheria yenyewe pamoja na mikataba ya Kimataifa na Kikanda ambayo Tanzania imeridhia na ni Mwanachama.
Jaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi akitoa mada katika mafunzo ya Majaji.

“Uelewa huu kwa sasa ni muhimu zaidi kuendana na mabadiliko ya kiuchumi na kijamii ambayo Tanzania inakabiliana nayo, ambapo idadi ya makosa ya kutakatisha fedha pamoja na makosa mengine yanayohusisha ubadhilifu wa mali yameongezeka ukilinganisha na kipindi cha nyuma, hali hii inailazimu Mahakama kuwa na uelewa wa kutosha wa namna ya kusikiliza na kutoa maamuzi wa kesi hizo na kwa wakati,” alisisitiza, Mhe. Jaji, Feleshi.

Mafunzo haya ya siku tano yaliyoanza tarehe 13.12 na kutarajiwa kumalizika Jumamosi tarehe 17. 12. 2016 yanalenga katika kubadilishana uzoefu juu ya uendeshaji wa Mashauri ya jinai, taratibu na changamoto mbalimbali zinazowakabili na hatimaye kuja na mikakati ya pamoja ya jinsi ya kukabiliana nazo.

Aidha kwa mafunzo haya mahsusi chini ya ufadhili wa pamoja kati ya Mahakama na Serikali ya Uingereza chini ya program ya STACA yalitanguliwa na mafunzo kwa Mahakimu 173 yaliyofanyika kuanzia tarehe 14 Novemba – 2 Desemba, 2016.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI