4x4

SAMATTA APIKA BAO GENK YAUA 2-0 UGENINI MECHI YA MWISHO ULAYA


Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta mchana huu amecheza kwa dakika zote 90 na kuisaidia KRC Genk kushinda 2-0 ugenini katika mchezo wa Kundi F Europa League dhidi ya wenyeji Sassuolo Uwanja wa Mapei, Citta del Tricolore mjini Reggio nell'Emilia, Italia. 
Kwa matokeo hayo, Genk inamaliza kileleni mwa Kundi F baada ya kujikusanyia pointi 12 kutokana na mechi sita, ikishinda nne na kufungwa mbili.
Imeungana na Athletic Bilbao ya Hispania iliyomaliza nafasi ya pili kwa pointi zake 10 kufuzu hatua ya 32 Bora ya michuano hiyo.
Mbwana Samatta mchana huu amecheza kwa dakika zote 90 na kuisaidia KRC Genk kushinda 2-0 dhidi ya Sassuolo  

Katika mchezo huo, Samatta aliseti bao la kwanza lililofungwa na kiungo Mbelgiji, Bryan Heynen dakika ya 58 wakati bao la pili lilifungwa na mshambuliaji Mbelgiji, Leandro Trossard dakika ya 80, akimalizia pasi ya mshambuliaji Mgiriki, Nikolaos Karelis.
Huo unakuwa mchezo wa 38 kwa Samatta tangu ajiunge na Genk Januari mwaka huu kutoka TP Mazembe ya DRC, 18 msimu uliopita na 18 msimu huu, akifunga mabao 10, matano msimu huu na matano msimu uliopita.
Katika mechi hizo, ni 19 tu ndiyo alianza, 10 msimu uliopita na nane msimu huu, wakati 17 alitokea benchi nane msimu uliopita na 14 msimu huu – na mechi 10 hakumaliza akitolewa, sita msimu uliopita na nne msimu huu.
Kikosi cha US Sassuolo Calcio kilikuwa: Pegolo, Antei, Missiroli/Pellegrini dk45, Matri, Acerbi, Lirola, Mazzitelli, Cannavaro, Caputo, Ragusa/Ricci dk45 na Adjapong.
KRC Genk : Jackers, Walsh, Brabec, Dewaest, Castagne, Ndidi, Heynen/Kumordzi dk88, Samatta, Bailey/Buffel dk81, Trossard na Karelis/Sabak dk92.
Post a Comment