SIMBA BINGWA LIGI YA VIJANA U-20, WAIUA AZAM KWA MATUTA CHAMAZI


Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
SIMBA SC imefanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi ya Vijana chini ya umri wa miaka 20 Tanzania Bara, baada ya kuifunga Azam FC kwa penalti 5-3 kufuatia sare ya 2-2 ndani ya dakika 120.
Katika mchezo huo ulifanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), timu zote zilionyesha kandanda safi.
Simba walikuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 14 mfungaji Moses Kitandu aliyemalizia pasi ya George Emmanuel, lakini Shaaban Iddi akaisawazishia Azam dakika ya 28.
Rais wa TFF, Jamal Malinzi (kushoto), akimkabidhi Kombe la ubingwa wa Ligi ya U-20 Nahodha wa Simba, Moses Kitundu
Makamu wa Rais wa TFF, Wallace Karia akiwavalisha Medali wachezaji wa Simba
Wachezaji wa Simba wakicheza mduara baada ya ushindi wao

Wachezaji wa Simba wakifurahia na Kombe lao leo Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam

Said Mohammed akaifungia Azam FC bao lililoelekea kuwa la ushindi dakika ya 57, kabla ya Said Hamisi kuisawazishia Simba dakika ya 83.
Katika dakika 30 za nyongeza baada ya 90 kukamilika kwa sare ya 2-2 si Simba ya kocha Nico Kiondo wala Azam ya kocha Iddi Nassor ‘Cheche’ iliyofanikiwa kuongeza bao. 
Waliofunga penalti za Simba ni Calvin Faru, Said Hamisi, Mokiwa Perus, Vincent Costa na Moses Kitandu, wakati za Azam zilifungwa na Abbas Kapombe, Rajab Mohammed na Adolph Bitegeko huku ya Said Mohammed ikipanguliwa na kipa Ally Salum.
Michuano hiyo ya kwanza ya Ligi ya Vijana kufanyika nchini, ilidhaminiwa na Azam TV na ilishirikisha timu 16 zikianzia hatua ya makundi katika vituo vya Bukoba mkoani Kagera na Chamazi, Dar es Salaam.
Michuano hii inaacha kumbukumbu ya kuhuzunisha kufuatia kifo cha mchezaji wa Mbao FC, Ismail Mrisho Khalfan wakati timu yake ikimenyana na Mwadui FC.
Ismail alifariki dunia jioni ya Desemba 4 mjini Bukoba baada ya kuanguka uwanjani dakika ya 74 Uwanja wa Kaitaba, Bukoba dakika chache baada ya kuifungia bao timu yae katika ushindi wa 2-0 na akazikwa nyumbani kwao Mwanza siku iliyofuata.
Alianguka baada ya kugongana na mchezaji wa Mwadui na baada ya kupatiwa huduma ya kwanza na kuonekana hali yake si ya kawaida, alikimbizwa hospitali ya mkoa wa Kagera kwa matibabu zaidi, ambako umauti ulimfika.
Alifariki akiwa ana umri wa miaka 19 na akiwa ametoka tu kufanya mtihani wa kidato cha Nne katika shule ya sekondari ya Mwanza, maarufu 'Mwanza Seco'.
Katika Nusu Fainali, Simba iliitoa Stand United kwa penalti pia, 8-7 baada ya sare ya 1-1 wakati Azam iliitoa Mtibwa Sugar kwa penalti nayo, 4-2 kufuatia sare ya bila kufungana ndani ya dakika 120.
Kikosi cha Simba leo kilikuwa; Ally Salum, Kelvin Faru, Joseph Anthony, Freddy Anthony, Vincent Costa, Mokiwa Perus, Hussein Hamisi, George Emmanuel/Said Hamisi dk29, Moses Kitandu, Dadi Mbarouk/Ally Abdallah dk18 na Rashid Juma/Mohammed Kijiko dk40.
Azam FC; Metacha Mnata, Said Mohammed, Abdul Omary/Omary Wayne dk46, Abbas Kapombe, Godfrey Mpembwe, Adolph Bitegeko, Ramadhani Mohammed/Charles Ndahaze dk51, Stanslaus Rwakatare, Shaaban Iddi, Abdallah Masoud/Joseph Prosper dk49 na Rajab Mohamed. 

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

HATUTOPAKI BASI DHIDI YA YANGA-MOKWENA

“PEMBA SALUTI KWENU” DK. NCHIMBI*

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA