Mbowe apingwa kila kona,Ni kuhusu kubeza juhudi za Serikali Kagera


*Wasomi wamshukia, wamtaka aache siasa

WADAU mbalimbali wamempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuwa muwazi kwa wananchi wake wakati wanapohitaji misaada mbalimbali wakati wa majanga.

Wametoa kauli hiyo leo jijini Dar es salaam wakati wa mahojiano na mwandishi wa habari hizi kueleza kauli ya hivi karibuni ya Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe ambaye amekaririwa akidai kuwa kauli za Rais mkoani Kagera ni za hatari.

Wamesema kuwa baadhi ya Watanzania wamezoea kupewa ahadi ambazo kwa wakati mwingine ni vigumu kutekelezeka na sasa watu kama Mbowe bado wako kwenye mtazamo huo.

Wameongeza kuwa Rais Magufuli amekuwa siku zote mkweli, jambo ambalo baadhi ya watu wasiopenda ukweli wanapotosha kauli zake kwa kutaka kuwachonganisha wananchi na Rais wao ambaye amekusudia kuwaletea wananchi maendeleo.

Rais Magufuli akiwa Kagera hivi karibuni alisisitizia msimamo ambao si mpya, umekuwa msimamo wake na wa Serikali tangu yalipotokea maafa ya tetemeko la ardhi mkoani humo kwamba Serikali itasaidia lakini haitaweza kumjengea nyumba kila mtu.“Baadhi ya wanasiasa na viongozi wamekuwa wakitoa kauli zenye kupotosha na kubeza hotuba ya Rais Magufuli mkoani Kagera jambo ambalo sio zuri na sio ukomavu wa kiasa” walisema.

Mhadhiri Mwandamizi Chuo Kikuu cvha Dar es Salaam, Dkt Bashiru Ally amesema kuwa katika mfumo wa siasa huru kuna kutofautiana mitazamo kati ya wananchi ,Serikali na viongozi wa siasa lakini ni wazi kuwa Rais alisimama katika msimamo wa Serikali yake na uwezo wa kutekeleza ahadi zake.

Alisema kuwa Rais Magufuli alikuwa na maana nzuri ya kukabiliana na majanga nchini inategemea uwezo wa nchi na mshikamano wa wananchi na huo ni ukweli ambao wengi hawakupenda kuusikia.

Dkt. Bashiru Ally alisema kuwa kwa janga la Kagera kulikuwepo mshikamano wa Serikali katika ngazi zote, wananchi na wadau mbalimbali walishiriki kwa namna moja ama nyingine kukabiliana na janga hilo.

“Wito wangu ni kuwataka wanasisa kujifunza kutokana na majanga badala ya kutoa kauli tatanishi na zenye kubomoa mshikamano wa wananchi, bali wanatakiwa kukosoa bila kubeza, kupotosha kwa namna ni ya kungwana,” alisema Dkt Bashiru

Kwa upande wake Dkt. Benson Bana kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam amesema kuwa watu wanatafsiri vibaya maneno ya Mhe. Rais aliyoyaongea Mkoani Kagera hivi juzi.

“Mheshimiwa ameongea ukweli kwa sababu ni sahihi kuwasaidia watu wengi kwa pamoja kuliko kumsaidia mtu mmoja mmoja,” alisema.

Aliongeza kuwa hakuna haja ya kuwa na wasiwasi juu ya lugha za Mhe. Rais kwani lugha zake hazina ubabaishaji ni za kweli na ziko moja kwa moja, hao wanaomuongelea vibaya ni wale wenye lengo la upinzani tu na sio maendeleo ya Taifa.

Ameongeza kuwa kwa upande wake pamoja na wananchi wenye mapenzi ya kweli wamemuelewa Mhe. Rais na ndio maana walikuwa wakimpigia makofi wakati akiongea kule Kagera.

”Mimi nilikuwepo mkoani Kagera na hotuba za mheshimiwa zote nilizisikiliza kwa makini ndio maana nasema wanye nia mbaya na Rais ndio wanaoongea mabaya juu yake kwani mbona alivyoongelea suala la kupunguza umeme hawakusema chochote?” alihoji Dkt. Bana.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Chama cha United Democratic Party (UDP) John cheyo amewataka Watanzania kutotegemea serikali kwa kila kitu pindi wanapopatwa na majanga.

Alisema kuwa lengo la Mheshimiwa Rais Magufuli ni kutaka Watanzania kujenga utamaduni wa kujitegemea pindi wanapofikwa na majanga mbalimbali na ndio maana alitaka kujua juhudi zao kabla ya kuomba msaada wa Serikali.

Profesa Haji Semboja alisema kuwa kauli ya Rais ilikuwa ni kuwahimiza watu wa Kagera ambao anajua wana uwezo wa mambo mengi ya kulima mazao mbalimbali kama vile mazao ya chakula na biashara ikiwemo ndizi na kahawa ambayo yanaweza kuwapatia chakula cha kutosha wananchi wa mkoa huo.

Naye Kaimu Mkuu wa Chuo cha Diplomasia nchini Dkt. Bernad Achiula amesema kuwa baadhi ya wananchi wamepokea hotuba ya Rais John Magufuli kwa mtazamo tofauti, lakini ni dhahiri hakuna nchi yeyote duniani ambayo inahudumia kila mwananchi katika majanga ya kiasili yanayotokea.

“Wajibu wa Serikali katika nchi yeyote ni kujenga na kuboresha miundombinu mbalimbali iliyotokea ikiwemo barabara, hospitali, shule, malazi ya muda kwa waadhirika, madawa, miundombinu ya umeme, maji kwa waathirika hatua inayolenga kuwapa pole waathirika hao.

Alisema kuwa hatua hizo zinalenga kutoa huduma kwa wananchi wengi kuliko kutoa msaada kwa mtu mmoja mmoja. Alisema wanaotaka kumlaumu Rais basi wangemlaumu kama angekuwa Serikali yake haijatoa huduma hizo muhimu.

Alipoulizwa kuhusu kauli hizo za Mbowe, Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO ambaye pia ndiye Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi alisema lugha ya Rais na Serikali kwa ujumla kuhusu maafa ya Kagera na mengine yaliyotokea nchini haijawahi kubadilika wala kutetereka.

“Rais na Serikali yake kwa ujumla wamekuwa wazi katika hili na itaendelea kuwa wazi kwamba kama Taifa hatuna raslimali za kumsaidia kila mwathirika wa tetemeko la Kagera kwa kumfanyia kila kitu.

Serikali ilitibu majeruhi wote bure, ilisaidia kifuta machozi kwa familia zote zilizopoteza ndugu zao, ilisaidia waathirika kupata huduma za kibinadamu kama dawa, ushauri wa kisaikolojia, vyakula na mavazi na maturubai kwa makazi ya muda na inaendelea kujenga miundombinu kama shule, zahanati na barabara,” alisema.

Dkt Abbas akasisitiza: “Mbowe atafute tu ajenda nyingine. Nilikwenda Kagera na kukaa kwa wiki mbili baada ya tetemeko kutokea ambapo nilibahatika kuzungumza na waathirika mijini na vijijini; hakuna kati yao popote aliyekuwa anasema Serikali itamjengea nyumba au kumsaidia kila kitu. Kwa hiyo ujumbe wa Rais ulieleweka tangu mwanzo na hata sasa.”

Ameongeza kuwa Serikali imesaidia kaya maskini kwa kuwapatia sajuri na mabati kwa ajili ya ujenzi wa nyumba.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

NI SIMBA PEKEE ILIYOFUNGWA ROBO FAINALI

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

DK NCHIMBI AMTEMBELEA MZEE YUSUF MAKAMBA*

AZIZ KI AAHIDI KILA ATAKAYEIFUNGA MAMELODI

DKT NCHIMBI AWAAHIDI MAKUBWA WANANCHI WA KWELA, RUKWA

DKT NCHIMBI ASHIRIKI MAZISHI YA ASKOFU.GACHUMA WA KANISA LA NLGCC

π™‚π˜Όπ™ˆπ™Šπ™‰π˜Ώπ™„ π™†π˜Όπ˜Ύπ™ƒπ™€π™•π˜Ό π™†π™„π˜½π™„π™‰π™‚π™’π˜Ό.