WIZARA YA MALIASILI NA UTALII YAOKOA WAFUGAJI 50 WALIOKUWA WAKIPITISHA MIFUGO YAO NDANI YA PORI LA AKIBA LA SELOUS


Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Askari wa Wanyamapori wa Pori la Akiba la Selous, Kanda ya Kaskazini Mashariki Kingupira imewaokoa wafugaji 50 waliokuwa wakiwapitisha jumla ya ng’ombe 1780, kondoo 200 na punda 6 baada ya kutelekezwa kwa muda wa siku tano na mtu mmoja aliyetajwa kwa jina la Mzigua aliyewarubuni kwa kuwaonyesha njia za mkato ndani ya Pori hilo wao bila kujua na kuamua kuwakimbia. 

Bw. Lisasi Cherehani ambaye ni mmoja wa wafugaji hao alisema ‘’tulimpa Mzigua kiasi cha zaidi ya shilingi 5,000,000 kutoka kwa wafugaji kama malipo ya kutufikisha eneo la Ilonga mkoani Morogoro tukitokea vijiji vya Ndundunyekanza, Kipungila na Chumbi vilivyopo wilayani Rufiji mkoani Pwani kwa makubaliano kuwa atatupitisha njia fupi ya mkato tutakayotembea kwa muda wa siku tano tu, hatukujua anatutupitisha ndani ya pori hili. ‘’

Baada ya kutelekezwa, wafugaji hao ambao walikuwa katika hali mbaya waliomba msaada kwa ndugu zao ambao waliwasiliana na Uongozi wa Pori la Akiba la Selous ambao kwa haraka walifanya jitihada za kuokoa maisha yao ikiwa ni kuwapa huduma ya kwanza, maji, uji pamoja na kuwakimbiza hospitalini kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Maj. Gen. Gaudence Milanzi aliwatembelea wafugaji hao jana kwa ajili ya kuwapa pole na kuwapelekea chakula yakiwemo maji pamoja na unga.

Aidha, Milanzi aliagiza Wafugaji hao waachiwe huku akitoa wito kwa wananchi kuacha kupita maeneo ya Hifadhi kwa vile ni kosa kisheria na wale wote watakaobainika watachukuliwa hatua za kisheria na kuahidi kuwa mtu huyo aliyewa danganya kwa kuwapitisha ndani ya Hifadhi hiyo ni lazima akamatwe kwa udi na uvumba.

‘’Sisi kama Serikali kitu cha kwanza ni ubinadamu tumewahudumia na hivyo natoa tamko la kuwaachia wafugaji wote waliopotea ndani ya Pori hili kwa vile mateso waliyoyapata na mali waliyoipoteza ni kubwa sana baada ya kudanganywa kwa na kupitishwa ndani ya Pori la Akiba la Selous.’’ Alisema Milanzi

Mmoja wa wafugaji aliyekuwa katika msafara huo na aliyekuwa akiwasiliana kwa njia ya simu , Bw. Lisesi Cherehani akielezea namna walivyotelekezwa katika pori hilo, alisema kuwa walianza safari hiyo siku ya jumatano ambapo walikuwa wakitembea usiku na mchana kwa muda w siku tano bila kujua wanapitishwa ndani ya Hifadhi hiyo ndipo wakaanza kushikwa na kiu kwa vile maji waliyokuwa nayo yaliwaishia na kila walipokuwa wakijaribu kumuuliza aliyewapitisha njia hiyo alikuwa akiwambia baada muda mfupi watakutana na maji hata hivyo waliendelea na safari bila mafanikio ndipo walipoanza kuanguka na baadhi ya wafugaji walianza kunywa mikojo yao pamoja na damu za kondoo kwa ajili ya kuokoa maisha yao.

Aliongeza kuwa, wasingekuwa Askari wanyamapori ambao walikuja kuwapa msaada wa kibinadamu kwa kuwapatia maji pamoja na kuwanyesha uji wangeweza kufa wote.‘’Nawashukuru sana askari wanyamapori kwa kutuhudumia bila wao leo hii msingemkuta mtu yeyote hapa tungekuwa tayari tumeshakufa.’’ Alisema Bw. Cherehani.

Mfugaji mwingine, Mbaga Mahila aliwashukuru sana Askari wanyampori kwa utu waliouonesha tokea mwanzo walipowaokoa hadi hapo walipofikia na kuitaka jamii ibadilishe mtazamo wa kuwaona askari wanyamapori kama watu katili jambo ambalo halina ukweli wowote.

Pia, Masanje Hambe aliiomba Serikali iwasamehe kwa kuwa wametambaua kosa la kuingia ndani ya Pori la Akiba la Selous kinyume cha sheria lakini hata hivyo hawakujua kuwa wanapitishwa ndani ya hifadhi hiyo.

Awali, Mkuu wa Kanda ya Mashariki Kingupira, Bw. Paschal Mrina alisema wamepata taarifa za wafugaji hao kutoka kwa Wasamaria wema na Uongozi wa wilaya ya Rufiji kuwa kuna wafugaji wamepotelea ndani ya hifadhi hiyo na kwa bahati nzuri kulikuwa na mfugaji mmoja aliyekuwa na simu ndipo wakaanza kuwasiliana naye na kuunda kikosi maalum cha doria kwa ajili ya kuwaokoa.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Kanda hiyo alisema wamefanikiwa kuwaokoa wafugaji wote na ilionekana mizoga saba na wengine ambao hawakuonekana taratibu za kuanza kutafuta zimeandaliwa

Alielezea njia walizotumia kuokoa wafugaji hao ni kuwa waliunda vikosi vitatu vya doria ambapo kikosi cha kwanza kilifanya doria kwa njia za miguu, kikosi cha pili kilfanya doria kwa njia za magari na kikosi cha tatu kilifanya doria kwa kutumia ndege kwa ajili ya kubaini walipo.

Kwa upande wake, Katibu wa Chama cha Wafugaji, Bw. Magembe Makoye alitumia fursa hiyo kuiomba Serikali kuacha kuwafukuza wafugaji katika maeneo waliyopo badala yake wawatafutie maeneo mbadala ili kuthibiti matukio kama hayo ambayo yamepelekea hasara na mateso makubwa kwa wafugaji.

Pori la Akiba la Selous lina ukubwa wa kilomita za mraba 50,000 na limegawanywa katika kanda nane huku Kanda ya Mashariki Kipungira ikiwa moja kati ya kanda kubwa yenye kilomita za mraba 7,650, Shughuli zinazofanyika katika Pori hilo ni Utalii wa picha na pamoja na uwindaji  .
   Baadhi wa Wafugaji wakiwa wanakunywa maji na juisi walizopelekewa kama msaada baada ya kuokolewa na Askari wanyamapori wa Pori la Akiba la Selous,  Kanda ya Kaskazini Mashariki  Kingupira  baada ya kutelekezwa kwa muda wa  siku tano na mtu mmoja waliyemtaja kwa  jina maarufu la Mzigua aliyewarubuni kwa kuwaonyesha njia za mkato ndani ya Pori hilo ( Picha na Lusungu Helela-Wizara ya Maliasili na Utalii) 
  Baadhi ya Mzoga wa ngombe uliopatikana ndani ya Pori la Akiba la Selous,  Kanda ya Kaskazini Mashariki  Kingupira  baada ya Wafugaji 50  waliotelekezwa kwa muda wa  siku tano na mtu mmoja waliyemtaja kwa  jina maarufu la Mzigua aliyewarubuni kwa kuwaonyesha njia za mkato ndani ya Pori hilo na kisha kuwakimbia( Picha na Lusungu Helela-Wizara ya Maliasili na Utalii)
   Mmoja wa  wafugaji aliyepotea na  kutelekezwa ndani ya Pori la Akiba la Selous,  Bw. Lisesi Cherehani aliyekuwa na ng’ombe 180 na punda mmoja akiangalia mmoja wa ng'ombe wake aliyekufa kwa kukosa  maji ya kunywa kwa muda  wa siku tano kwenye Kanda ya Kaskazini Mashariki katika Pori la Akiba la Selous ( Picha na Lusungu Helela-Wizara ya Maliasili na Utalii)
 Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Maj. Gen. Gaudence  Milanzi (katikati) akipata taarifa kutoka kwa  Meneja wa Mradi wa Pori la Akiba la Selous    Bw. Enock Msocha (wa tatu kushoto)  mara baada ya  kuwasili kwa ajili ya kuwatembelea  Wafugaji 50 waliokolewa na Askari wanyamapori baada ya kutelekezwa  na mtu mmoja waliyemtaja kwa  jina maarufu la Mzigua aliyewarubuni kwa kuwaonyesha njia ya mkato ndani ya Pori hilo na kisha kuwakimbia ( Picha na Lusungu Helela-Wizara ya Maliasili na Utalii)

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI