Zitto Kabwe
Wizara
ya Nishati ya Kenya imepiga marufuku gesi ya kupikia kutoka Tanzania
kuingia nchini humo. Tamko la Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati ya Kenya
linasema ' ndani ya siku 7 kuanzia juzi tarehe 24 Aprili 2017, itakuwa
ni marufuku Kwa Kenya kuagiza Gesi ya kupikia kutoka Tanzania '.
Uamuzi
huu wa Kenya ni kinyume na misingi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo
Tanzania na Kenya ni wanachama. Kwa mujibu wa Itifaki ya Soko la
Pamoja, bidhaa za nchi zetu zinaruhusiwa kusambaa ndani ya jumuiya bila
vikwazo.
Gesi ya
kupikia kuingia Kenya hutokea Tanzania Kwa sababu Tanzania ni nchi pekee
katika ukanda huu ambayo imewekeza mitambo ya kupokea Gesi na kuiweka
kwenye mitungi.
Bandari ya Dar Es salaam na mfumo mzuri zaidi wa kupokea
gesi kuliko Bandari ya Mombasa na hivyo kuifanya gesi inayotoka
Tanzania kuwa na gharama nafuu nchini Kenya kuliko gesi inayoagizwa
kupitia bandari ya mombasa.
Uamuzi wa kuzuia Gesi kutoka Tanzania ni
uamuzi wenye kulenga kuilinda bandari ya Mombasa Kwa kuvunja mkataba wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki na Kwa kutaka kuifanya Tanzania iendelee
kuwa muuzaji wa malighafi kwenda Kenya badala ya bidhaa zilizokamili
Kama gesi ya kupikia.
Uamuzi
huu wa Serikali ya Kenya una lengo la kuathiri urari wa biashara kati
ya Tanzania na Kenya ambapo Kwa miaka ya hivi karibuni Tanzania imekuwa
ikiuza bidhaa nyingi zaidi huko Kenya kuliko inazoagiza kutoka nchi
hiyo.
Ninamsihi
Waziri wa Biashara na Viwanda wa Tanzania afuatilie suala hili na
kuzungumza na mwenzake wa Kenya ili waondoe vikwazo Hivi vya biashara
ambavyo havina maana yeyote na vinazuia raia wa kenya kupata bidhaa
nafuu kutoka Tanzania.
Viwanda vingi vya Kenya hutegemea malighafi
kutoka Tanzania, kuzuia gesi ya kupikia na kuendelea kuagiza malighafi
za kuendesha viwanda vyao ni sera ya Kenya kuifanya Tanzania kuwa chanzo
cha malighafi tu na sio chanzo cha bidhaa zilizoongezwa thamani.
Serikali
ya Tanzania isikubali hili na ianze mazungumzo mara moja na Serikali ya
Kenya ili Watanzania wanaouza gesi ya kupikia huko Kenya waendelee
kuuza na kutumia Bandari ya Dar Es Salaam.
Kama Serikali ya Kenya
ikiendelea na msimamo wake basi Tanzania ichukue msimamo kama huo Kwa
bidhaa za Kenya Kama maziwa ambayo yamejaa kwenye soko letu.
Zitto Kabwe, Mb
Kigoma mjini
26/4/2017
Comments