DARAJA LA MAGARA KUANZA KUJENGWA MWEZI JULAI

 Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), mkoa wa Manyara Eng. Bashiri Rwesingisa, akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani, wakati alipokuwa akikagua mahali ambapo litajengwa Daraja la Magara lenye urefu wa Mita 84, Wilayani Babati, mkoani Manyara, jana.
 Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani, akitoa maelekezo kwa Mhandisi Christopher Saul (katikati), kutoka Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), mkoa wa Manyara wakati alipokuwa akikagua mahali ambapo litajengwa Daraja la Magara lenye urefu wa Mita 84, Wilayani Babati, mkoani humo, jana.


Serikali imesema ipo katika hatua za mwisho za kumpata mkandarasi atakayejenga Daraja la Magara lenye urefu wa Mita 84 katika barabara ya Mbuyu wa Mjerumani-Mbulu KM 21 lililopo mkoani Manyara ambapo mkataba huo unatarajiwa kusainiwa mwezi Juni mwaka huu.
Akizungumza hayo jana kwa wananchi wa Kijiji cha Mayoka, wilaya ya Babati, mkoani humo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani, amewataka wananchi hao kutoa ushirikiano kwa mkandarasi atakayepatikana ili kurahisisha mradi huo kukamilika kwa wakati.
"Serikali inaendelea kukamilisha taratibu zake ili kumpata mkandarasi, sasa ombi langu kwenu ni kuhakikisha kuwa mnatoa ushirikiano kwa Mkandarasi huyo pindi atakapofika eneo la kazi", amesema Naibu Waziri.
Amebainisha kuwa Serikali imekuwa ikitenga fedha mwaka hadi mwaka ili kuweza kukamilisha mradi huo ambapo kwa mwaka wa fedha 2017/18 zaidi ya Shilingi Bilioni 1 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa KM 1.2 za barabara sehemu ya mlima Magara ambayo itajengwa kwa kiwango cha zege.
Naye, Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), mkoa wa Manyara Eng. Bashiri Rwesingisa amemhakikishia Naibu Waziri huyo kumsimamia mkandarasi atakayepatikana katika ujenzi wa Daraja hilo ili kuondoa kero na adha wanayopata wakazi wa Babati na maeneo jirani.
Ameongeza kuwa ujenzi wa Daraja la Magara pia litahusisha ujenzi wa barabara unganishi zenye urefu wa KM 2 kwa kiwango cha lami na KM 2 kwa kiwango cha Changarawe.
Daraja la Magara ni moja ya Daraja litakaloleta chachu ya maendeleo kwa wakazi wa Arusha, Mbulu na Babati kwani ujenzi wake utarahisisha huduma za usafirishaji na kukuza utalii kwa nchi kupitia Hifadhi ya Mbuga ya Manyara.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.


 Muonekano wa Sehemu ambapo Daraja la Magara lenye urefu wa Mita 84 katika barabara ya Mbuyu wa Mjerumani-Mbulu KM 21 litakapojengwa. Mkataba wa ujenzi wake unatarajiwa kusainiwa mwezi Juni mwaka huu.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani, akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Mayoka kuhusu mkakati wa Serikali katika ujenzi wa Daraja la Magara wilayani Babati, mkoani Manyara, jana.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.


Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI