LWANDAMINA AWASIHI WACHEZAJI YANGA KUWEKA MATATIZO KANDO WAPIGANIE UBINGWA


Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
KOCHA Mzambia wa Yanga, George Lwandamina amesema kwamba anaamini vijana wake wakiweka matatizo yao kando na kuelekeza nguvu zao uwanjani watashinda mechi zote zilizosalia za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na kutetea ubingwa.
Yanga imerejea jana usiku mjini Dar es Salaam kutoka Geita ilipokwenda kuweka kambi fupi na kucheza mchezo mmoja wa kirafiki, ikitokea Mwanza ambako Jumapili iliyopita ilivuliwa ubingwa wa Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), michuano inayojulikana kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) kwa kufungwa 1-0 na wenyeji, Mbao FC katika Nusu Fainali.
Na baada ya kutua Dar es Salaam, kocha Lwandamina akasema sasa anaelekeza nguvu zake kwenye mechi za Ligi Kuu na anaamini anaweza kuchukua taji kama vijana wake hawatamuangusha.
Kocha George Lwandamina anaamini Yanga inaweza kutetea ubingwa wa Ligi Kuu kama vijana wake wataweka matatizo yao kando  

“Tunahitaji kuwa kitu kimoja kwa sasa, tuweke matatizo yetu kando kwa ajili ya heshima zetu na tumalizie msimu vizuri kwa furaha kwa kuchukua angalau ubingwa wa Ligi Kuu, naamini vijana wanaelelewa umuhimu wa hilo,”alisema Lwandamina jana.
Yanga inatarajiwa kushuka dimbani kesho Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kumenyana na Prisons ya Mbeya katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Mchezo huo ni mmoja kati ya viporo vyake viwili vilivyoweka ili kuwapa nafasi ya kushiriki vyema michuano ya Afrika mwezi uliopita – mwingine ukiwa ni dhidi ya Toto Africans ya Mwanza. Mechi nyingine za Yanga ni dhidi ya Mbeya City, Mbao FC na Kagera Sugar. Na zote itacheza nyumbani Dar es Salaam kasoro wa Mbao FC pekee, ndiyo watarejea Mwanza. 
Kwa sasa Yanga inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu, ikiwa na pointi 56 baada ya kucheza mechi 25, nyuma ya vinara, Simba SC wenye pointi 59 za mechi 27.
Azam FC inafuatia kwa mbali kabisa nafasi ya tatu kwa pointi zake 46 za mechi 27, sawa na Kagera Sugar yenye pointi 46 pia za mechi 26.
Changamoto kubwa inayoikabili Yanga katika kampeni zake za kutetea ubingwa ni hali mbaya ya kifedha tangu Mwenyekiti na mfadhili wa klabu, Yussuf Manji aingie kwenye matatizo na Serikali Januari, mwaka huu.
Wachezaji wamekuwa wakigoma mara kwa mara kushinikiza walipwe malimbikizo yao ya mishahara taangu Desemba. Lakini inaonekana matatizo ya Manji yamekwisha kwa sasa na anatarajiwa kurudisha nguvu zake katika timu muda si mrefu kwa mujibu wa viongozi wa Yanga wenyewe. 

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI

KOCHA WA AL.AHLY ASEMA YANGA NI TIMU BORA NA NGUMU