MAKONDA ANAKIMBIZANA NA WATU AKIWA AMEVAA TAULO


Uswahilini kwetu bafu na choo huwa mbali kabisa. Ukitaka huduma ya choo au bafu inabidi upige hatua za kutosha. Hayo maisha ya choo na bafu ndani kwa ndani ni huko kwenu.
Sasa basi, utaratibu wetu ni kwamba unapokwenda kuoga unatoka bafuni kifua wazi huku umevaa kaptula yako, utaenda kujifuta maji vizuri na kubadili nguo kwa nafasi ukiwa chumbani.
Ukiona mtu anakwenda kuoga akiwa amejifunga taulo, ujue huyo ana mke wake au ndiye baba mwenye nyumba. Wewe kijana msela, unavaa taulo jeuri hiyo kakupa nani? Taulo lina hadhi yake Uswahilini kwetu.
Kuhusu mwenye mke wake au baba mwenye nyumba, kwa kawaida maji hutangulizwa bafuni, kisha ndipo mhusika hutembea kwa mikogo na taulo lake kwenda kuoga. Wewe msela huwezi kupelekewa maji bafuni, utajibebea mwenyewe ndoo ya maji.
Hata hivyo, taulo kwa baba mwenye nyumba au mwenye mke wake katika nyumba za kupanga Uswahilini, huonesha ufahari na kuwatambia tu wale ambao hawajaoa, maana wengine huvaa mpaka kanga za wake zao. Ni mbwembwe tu, kulingishiana tu!
Unakuta kanga imeandikwa: “Fahari ya ndoa hii, usiyeoa kazi kwako Bashite.” Huyo anakatiza uwanjani kwa mbwembwe kuelekea bafuni kuoga.
Pamoja na tambo zote, ukweli unabaki kwamba taulo au kanga ambayo mtu huvaa kwenda kuoga huwa haitaki mbwembwe, maana kwa kawaida ndiyo hubaki vazi la mwisho mwilini.
Stara ya mvaa taulo huwa lile taulo alilovaa. Na inafahamika kuwa taulo hufungwa kiunoni. Taulo huwa halina vifungo vya kushikia wala taulo si kama msuli kusema unaweza kulifunga mkanda ili lisivuke.
Ukivaa taulo shika safari ya kuoga na ukimaliza ingia ndani ukavae. Taulo si vazi la kuketi nalo sebuleni unaangalia runinga au kukaa nalo kwenye meza ya chakula, litakuaibisha tu!
Ukiwa umevaa taulo hata ukisikia muziki unaoupenda hutakiwi kucheza. Maana unaweza kunogewa na kibega, ukakitikisa kwa juu huku chini taulo si lako, matokeo yake unabaki wa mnyama. Watu weweee!
Usipende utani na watoto ukiwa umevaa taulo. Unaweza kujifanya unamrusha mtoto kwa juu, huku chini kanga aliyokupa mkeo ukaogee na ujifute maji, ikakudondoka, mambo yakawa hadharani.
Uswahilini kwetu wanawake ndiyo huwa wajanja, maana wao huvaa kanga kisha taulo hufuata kwa juu. Ile kanga hufungwa kifuani, wenyewe huita passport size, halafu taulo ndiyo hufuata ambalo hufungwa kiunoni. Hivyo, taulo likimdondoka mwanamke, anakuwa habaki mtupu jumla.
MASHARTI YA TAULO
Bila shaka umeshaona kuwa taulo au kanga ya kuogea kwa kawaida ni vazi la mwisho ambalo halihitaji mbwembwe, kwa hiyo unapobaki nalo unapaswa kuwa makini zaidi ya neno lenyewe.
Huwezi kuvaa taulo halafu ulifungue kiunoni kisha ujifute jasho mbele za watu, matokeo yake utaonesha video ya utupu. Wenye kuona watapayuka: “Amemwaga radhii!”
Msisitizo ni kuwa hata kama jasho linakukera kiasi gani, hakikisha taulo linabaki mahala pake. Umeshaambiwa kuwa stara ya mvaa taulo au kanga ya kuogea ni lile taulo au kanga, inategemea mvaaji kavaa nini.
Jambo lingine ni kuwa taulo huwa halitaki mashindano. Siyo umelivaa halafu unataka kushindana mbio na watu, gharama yake ni kubwa mno. Taulo litakuvuka na radhi utamwaga, mwisho utaumbuka halafu waungwana watapaza sauti zao “watu wewee!” Na huwezi kuwazuia watu kushangilia.
Hata unapomwona mwizi, kama umevaa taulo hutakiwi kumkimbiza. Nakumbusha taulo siyo bukta, utapiga hatua mbili na lenyewe litadondoka, mwizi utamkosa na radhi utakuwa umeshazimwaga.
Ukivaa taulo usigombane wala usiamulie ugomvi wa watu, mwisho kabisa itakugharimu tu! Ukivaa taulo wewe jifanye hupendi makuu hata kama hayo makuu unayatamani.
Subiri ukishavaa nguo zako ndipo unyanyuke ukapambane au ukaamulie ugomvi. Ukishavua taulo na kuvaa nguo zako, hapo sasa unaruhusiwa kwenda kukimbizana na wezi au kuamulia ugomvi. Ukishavaa nguo ndiyo ukacheze muziki unaoupenda au kashindane mbio na vyovyote unavyotaka.
MAKONDA NA TAULO
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, katika mapito yake ya kiuongozi na hatua aliyofikia, ni wazi alikuwa amesitiriwa na vazi la mwisho, mithili ya mvaa taulo au kanga ya kujifutia maji Uswahili.
Kutokana na hali aliyokuwa nayo, alipaswa kuwa makini katika maneno na matendo yake pengine kuliko kiongozi mwingine yeyote ndani ya Serikali ya Rais wa Tano wa Tanzania, Dk John Magufuli.
Umakini wa Makonda unatakiwa kufanana na ule wa mvaa taulo, kwamba hapaswi kukimbizana na watu hovyo, wala hatakiwi kuonesha mbwembwe. Hata anaposikia muziki na kutamani kuucheza, mazingira yanamlazimisha azibe masikio, maana anaweza kuadhirika.
Mbinu mbovu za ukamataji wa watu aliowaita wauza dawa za kulevya kisha kuwatangaza hadharani bila ushahidi, matokeo yake kuishia kuchafua majina ya watu ambao waliachiwa huru, wengi wao bila kufikishwa hata mahakamani ni kashfa moja.
Zikaibuka tuhuma kuwa Makonda katika kushughulika na watu aliowaita wauza dawa za kulevya, alibagua sana. Kwamba shabaha yake ililenga watu wa aina fulani, wale waliokuwa karibu naye hakuwagusa japo majina yao yanatajwa kwa muda mrefu.
Zikawepo tuhuma kwamba Makonda anafadhiliwa na watuhumiwa wa dawa za kulevya. Kwamba wamempa magari ambayo anayatumia. Wengine wanamfadhili kwa mambo mbalimbali ya kimaisha.
Yapo magari matatu ambayo yapo kwenye mashitaka aliyofungua Meya wa Ubungo, Boniface Jacob kwenye Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma dhidi ya Makonda, kwamba amezawadiwa magari na watu aliowatuhumu kuwa wauza dawa za kulevya.
Magari hayo ni BMW X6, Toyota Lexus Land Cruiser V8 na Ford Ranger. Magari hayo kwa nyakati tofauti, Makonda ameonekana nayo na hakuwahi kutokeza hadharani kukanusha tuhuma hizo dhdi yake au kuthibitisha uhalali wa yeye kumiliki magari hayo.
Tuhuma nyingine ni kuwa Makonda anamiliki utajiri mkubwa ambao amejipatia ndani ya muda mfupi. Hili pia hata mara moja hajawahi kutokeza na kufafanua mali zake halali na kukana anazotajwa nazo lakini siyo zake ili kuuthibitishia umma kwamba anasingiziwa.
SAKATA LA BASHITE
Wakati mambo yakiwa moto hasa, likaibuliwa jambo lingine ambalo ni utata wa elimu ya Makonda. Ndipo lilipoibuka jina la Daud Albert Bashite (DAB), kwamba Makonda jina lake la kwanza ni Daud na baba yake mzazi ni Albert Bashite.
Maelezo ni kuwa Makonda alilichukua jina la Paul Christian kutoka kwa mtu ambaye alifaulu vizuri mtihani wa kidacho cha nne. Kwamba Makonda alinunua cheti cha Paul Christian ambacho kilimuwezesha kusoma elimu ya juu.
Mwenye cheti anaitwa Paul Christian Malanja, kwamba cheti kiliandikwa Paul Christian M, kisha Makonda akaapa mahakamani, ile M akaiongezea ikawa inasomeka Makonda.
Tuhuma hii ya Makonda ni kubwa sana. Hoja kubwa ni kwamba Makonda alifanya udanganyifu ambao ni uhalifu. Tuhuma ni kughushi cheti ambayo adhabu yake ni kifungo jela. Mtu mwenye sifa ya kuwepo jela hapaswi kuwa kiongozi katika ofisi ya umma.
Taarifa nyingi ziliibuliwa zenye kuthibitisha kuwa Makonda ni Daud Albert Bashite. Kipindi chote hayo yakiibuliwa, Makonda alinyamaza kimya na hakutokeza popote kuthibitisha kuwa yeye ni Paul Makonda na siyo Daud Bashite.
Yapo magazeti yaliamua kuuchimba ukweli kwa kufanya uchunguzi wa kina mpaka Kijiji cha Koromije, Misungwi, Mwanza ambako inaelezwa ndiyo asili ya Makonda na yote yalitokeza yakiwa na ripoti zinazofanana kuwa Makonda ni Daud Albert Bashite.
Mkanganyiko wa majibu ya Shule ya Sekondari Pamba, Mwanza ambako inadaiwa Makonda alisoma na kupata matokeo mabaya yaliyomfanya anunue cheti kwa Paul Christian, ni sababu ya habari za Makonda kudaiwa kughushi cheti kupata nguvu kubwa.
Suala la Makonda kudaiwa kughushi cheti liliibuliwa wakati mbaya, maana ndiyo kipindi ambacho Serikali ilikuwa inajinasibu kupambana na uwepo wa watu wenye elimu bandia. Taifa likawa macho, maana ilionekana Makonda hawezi kupona.
UVAMIZI CLOUDS TV
Makonda akiwa amenyamazishwa na mashambulizi ya kumiliki cheti cha kughushi, akiwa mpole na asiye na makeke aliyozoeleka nayo, kumbe upole wake ulikuwa wa kobe aliyeinama kutunga sheria.
Mbeba bango mkuu wa sakata la kughushi cheti alikuwa Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Askofu Josephat Gwajima. Kumbe Makonda naye alikuwa anamtafutia majibu Gwajima.
Ikapatikana video (sina uhakika kama ni ya kweli au ya kughushi) yenye kumwonesha mwanamke analalamika kuzaa na Gwajima lakini askofu huyo amemtelekeza bila kumpa matunzo.
Nyuma ya kupatikana kwa video hiyo, inadaiwa yupo Makonda. Kwamba alikuwa kiungo muhimu kuhakikisha kituo cha Clouds TV kinapata video hiyo na kushawishi kirushwe hewani kupitia kipindi cha Shilawadu ambacho hupatikana kila Ijumaa usiku.
Kwamba Ijumaa ya Machi 17, mwaka huu, Makonda akiwa ametega akitazama televisheni, akifuatilia kipindi cha Shilawadu hakuona video hiyo ya mama akilalamika kuzaa na Gwajima ikirushwa hewani.
Ndipo usiku huo, Makonda alivamia Clouds TV na askari wenye bunduki ambako inadaiwa aliwatisha watangazaji na mwandaaji wa kipindi cha Shilawadu. Zipo taarifa kuwa askari waliwapiga watangazaji na mwandaaji wa kipindi.
Suala la Makonda kuvamia Clouds TV lilikuwa kubwa mno. Lilivuka mipaka ya maadili ya uongozi wa umma kwa kiwango cha juu kabisa. Watu wengi waliamini hakukuwa na namna yoyote kwa Makonda kubaki ofisini.
Matarajio yalikuwa kwamba ama Makonda mwenyewe ajiuzulu kumsaidia Rais Magufuli ambaye ndiye mteuzi wake au Rais Magufuli kumwondoa kazini, maana kitendo alichokifanya siyo tu kinachafua na kusiliba taka sifa ya uongozi, bali pia kumlinda ni kushusha hadhi Urais wake.
Kamati iliyoundwa na aliyekuwa Waziri Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, ilitoka na ripoti inayothibitisha kuwa ni kweli Makonda alifanya uvamizi Clouds TV na kutoa vitisho.
Vitisho hivyo ni pamoja na kuwaambia watangazaji na mwandaaji wa kipindi cha Shilawadu kuwa kama wasingerusha hewani video hiyo ya mwanamke anayelalamika kuzaa na kutelekezwa na Gwajima, angewaingiza kwenye orodha ya wauza dawa za kulevya, pamoja na mabosi wao, vilevile wadhamini wa kipindi chao.
Kitisho hicho cha kuwaingiza kwenye orodha ya wauza dawa za kulevya, kilirejesha mjadala kuhusu Makonda na majina yake ya wauza unga, kwani yalikuwepo malalamiko makubwa kuwa wengi walikuwa wakitajwa kwa mikwara.
Siku moja baada ya Nape kupokea ripoti ya kamati aliyoiunda, Rais Magufuli alimfukuza kazi na nafasi yake kujazwa na Dk Harrison Mwakyembe aliyetokea Wizara ya Katiba na Sheria, kisha Waziri wa Katiba na Sheria akateuliwa Prof Palamagamba Kabudi.
TAULO LA MAKONDA
Mpaka hapo ni wazi kuwa Makonda alikuwa ameshafanya mengi yenye kutosha kumweka kando katika nafasi yake ya uongozi. Ni Rais Magufuli ndiye ambaye anamfanya aendelee kukaa kwenye kiti chake.
Kwa mantiki hiyo, Makonda tayari alikuwa amebaki na nguo moja ya mwisho mwilini, yaani taulo, kwani kila upande alishavuruga na kuchafuka, kwa hiyo amebaki kwa pendezo la Rais Magufuli.
Hivyo, kipindi ambacho Makonda amebaki kutegemea nguvu ya Rais Magufuli ili kubaki ofisi ya umma mithili ya mvaa taulo anavyotegemea stara yake kupitia taulo alilovaa, anapaswa kuwa makini na kujiepusha na mashindano pamoja na malumbano.
Mtu ukibaki na taulo na likakusitiri unapaswa kuliheshimu na ujue kuwa likivuka unaadhirika. Makonda alishabaki na nguo ya mwisho (taulo) katika uongozi wake baada ya kupoteza uhalali katika maeneo mengi, hivyo alipaswa kuboresha umakini wake.
Kwa takriban miezi miwili tangu kuvamia Clouds TV kisha Rais Magufuli kumkingia kifua kuwa hapangiwi mtu wa kufanya naye kazi kisha kumtimua Nape, Makonda alijitahidi kubaki kimya. Hilo lilimsaidia kwa kiasi kikubwa.
Kipindi ambacho Makonda alinyamaza, aliwafanya wale ambao walikuwa wakimshambulia nao kunyamaza, maana hawakuwa na mengine ya kumsema. Kama ni vyeti tayari walishasema, magari na utajiri kila kitu kilishazungumzwa, uvamizi Clouds TV yalishapita na mengine mengi.
Kama Makonda angekuwa na washauri wazuri, wangemweleza ukweli kuwa ukimya wake ulichochea amani aliyokuwa nayo. Ukinyamaza unawafanya wanaokutafutia sababu wakose sababu mpya, maana mengine yote ya zamani walishayamaliza.
Kitendo cha Makonda kuibuka na kufanya mahojiano kujibu mapigo ni kuonesha kuwa anajisahau kuwa yeye amebaki na vazi la mwisho mwilini (taulo), hivyo hapaswi kushindana na watu wengine.
Baada ya majibu yake, sasa ni wazi amewapa sababu ya kusema wale wote waliokuwa wanamshambulia. Tutasikia upya mashambulizi ya Gwajima na wengine ambao wasingekuwa na hoja kama Makonda angeendelea kubaki kimya.
Upo wakati unaweza kupata hisia kuwa Makonda anapenda kushambuliwa na akina Gwajima, maana alichokifanya ni kuchokoza ili washambuliaji warejee kazini kumwanika kama kawaida yao.
Katika hili, kosa kubwa ambalo Makonda amelifanya ni kuibuka kujibu mapigo akiwa hajajipanga na bila kuwa na hoja za msingi. Unawezaje kusema uvamizi Clouds TV ni igizo? Makonda amekuwa muigizaji?
Akasema anayajua mengi ya Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji wa Clouds Media Group, Ruge Mutahaba, kwamba ni tapeli na ni mtunzi tu wa nyimbo. Makonda ni mkuu wa mkoa, ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Dar es Salaam, kama unafahamu mtu ni mhalifu, kwa nini usiagize vyombo vimshughulikie?
Kama Makonda ulikuwa unasimama kisha unaagiza vigogo wakubwa ukutane nao Kituo Kikuu cha Polisi (Central) Mkoa wa Dar es Salaam, inashindikana nini kumwambia na Ruge ukutane naye Central ukabiliane naye kisheria? Maneno ya vijembe ya nini?
Mwisho kabisa unaona kuwa Makonda haijui pumzi yake kipindi hiki inasababishwa na nini. Ameamua kuichezea huku akitambua kuwa gharama yake ni kubwa. Mengine mengi sasa yatasemwa maana ameamua kuyachokoza.
Gwajima atasema halafu atajitetea kuwa Makonda amechokoza dude! Nyakati ngumu kama anazopitia Makonda, akiwa ameshachafuka kila upande, huku pia akiwa ameshavurugana na vyombo vya habari, anapaswa kutumia akili kuliko hisia.
Makonda ameamua kuongozwa na hisia, kwa hiyo ameamua kucheza muziki akiwa na taulo. Hisia zinamtuma kukimbizana na watu akiwa amevaa taulo. Hatoi nafasi ya kutosha kwa akili yake. Gharama yake ni kubwa mno mbele ya safari.
Ndimi Luqman MALOTO

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

ALLY KAMWE AZIMIA KWA MKAPA.

RAIS SAMIA KUZINDUA MKUTANO MKUU WA 79 WA BARAZA LA MICHEZO YA MAJESHI DUNIANI

MIGINGO KISIWA KIDOGO ZAIDI AFRIKA KILICHOGOMBEWA NA UGANDA, KENYA