Yamoto Bendi Yavunjika Rasmi, Kila mmoja kivyake


Bendi ya muziki ya Yamoto Bandi.
NA NA ANDREW CARLOS | UWAZI |MAKALA
DAR ES SALAAM: Kwa mara ya kwanza, usiku wa Jumapili, Septemba 21, mwaka 2014 katika anga la burudani Bongo ndani ya Uwanja wa Taifa wa Burudani, Dar Live jijini Dar, nilipata kushuhudia uzinduzi rasmi wa bendi mpya kabisa ya muziki ya Yamoto Band.

Katika usiku huo, walitambulisha kwa mara ya kwanza wimbo wao wa kwanza ulioitwa Yamoto, niliyeweza kumfahamu kwa harakaharaka alikuwa ni Dogo Aslay, lakini vichwa vingine vilivyounda bendi hiyo (Beka One, Enock Bella na Maromboso) sikuwahi kuviona popote. Nilimsifu sana bosi wao, Said Fella kwa kile alichokuwa amethubutu kukifanya.
 Miezi michache mbele, Yamoto Band ikawa imara na kuwa miongoni mwa bendi za vijana zinazotikisa katika Muziki wa Bongo Fleva.
Staili yao ya kupeana nafasi kila vesi ilikuwa ya kipekee na hata ubora wa sauti ya kila mmoja ilikuwa kivutio kikubwa masikioni mwa mashabiki wao. Yamoto walileta hamasa kubwa kwa wasanii wa Bongo Fleva na makundi mengi ya vijana ambayo yaliibuka yakiwemo Ruby Band, Ocean Classic na mengine kibao ambayo yapo mengine yaliyokuja kupotea. Ukiweka mbali umaarufu waliojizolea ndani ya muda mfupi, Yamoto wamefanikiwa kutoa nyimbo nyingi zilizoweza kutazamwa na mamilioni ya mashabiki katika Mtandao wa Youtube.Fella na Nyumba (2)Mkurugenzi wa Mkubwa na Wanawe ambaye pia ni mmiliki wa Yamoto Band, Said Fella akiongea na wanahabari wakati akitambulisha nyumba mpya watakazomiliki Yamoto Band. Kulia ni Asha Baraka.
Miongoni mwa nyimbo hizo ni Nitakupwelepweta, Su, Mama, Cheza Kwa Madoido, Nisambazie Raha, Nitajuta na nyingine nyingi. Licha ya kufanya vizuri wakiwa kama kundi na shoo zisizo na idadi za nje ya nchi, kwa sasa madai yaliyopo mezani ni kwamba bendi hiyo haipo tena kama zamani. Yamoto imebaki jina lakini wanaoiunda wamesambaratika. Mara ya mwisho kwao kufanya shoo ya hadharani kwa pamoja ilikuwa Aprili 26, mwaka huu katika Sikukuu ya Muungano iliyofanyika mkoani Dodoma.

Yapo madai ya chinichini kuwa hata mualiko huo wa kwenda kutumbuiza ‘walibembelezana’ mmojammoja na hawakuwa tena pamoja kundini. Ilidaiwa kuwa, chanzo cha kugawanyika kwa bendi hiyo ni ubinafsi unaofanywa na kiongozi wao, Fella akisemekana kumpendelea zaidi Aslay kuliko Enock, Maromboso na Beka. Mbali na upendeleo huo, hata zile nyumba walizoahidiwa kupewa inadaiwa kuwa ahadi hiyo imeyeyuka baada ya kusambaratika.
Fella Nyumba (5)
Nyumba za wasanii wa Yamoto Band.
Kila mmoja kwa sasa yupo kivyake, Aslay anadaiwa kubaki na Fella wakati Beka, Maromboso na Enock kila mmoja amepata menejimenti nyingine zinazosimamia muziki wao na tayari wapo waliotoa nyimbo na wengine bado wapo studio. Uwazi Showbiz ilifanikiwa kuonana na Beka Flavour ambaye yupo chini ya menejimenti mpya ya mtu anayefahamika kwa jina la Siraji ambapo projekti yake ya kwanza ni Wimbo wa Libebe. Beka anafunguka kuwa, hawapo pamoja kwa sasa ambapo Aslay amebaki kwa Mkubwa Fella lakini kwa upande wa Maromboso naye amepata menejimenti nyingine na Enock yupo tu hajapata menejimenti yoyote.
ASLAY HUYU HAPA
Kwa upande wa Aslay ambaye ameshaachia nyimbo tatu tangu aipe mgongo Yamoto (Angekuona, Usiitie Doa na Mhudumu) anakiri kuwepo katika wakati mgumu wa bendi hiyo na kwamba kuna kipindi ilifika wakakwama ndiyo maana walirudi nyuma. “Kifupi watambue tu kuna vitu fulani tulifanya mchanganyiko ambavyo siwezi kuvisema vikaturudisha tena nyuma,” anasema Aslay.
FELLA NAYE HUYU HAPA
Fella ambaye ndiye Mkurugenzi wa Mkubwa na Wanawe ambayo chini yake ipo Yamoto anaweka wazi kugawanyika kwa bendi hiyo kwamba ameamua kila mmoja awe kivyake.
“Tumeruhusu kila mmoja afanye kazi yake, hata wewe mwandishi ukitaka mmoja unaweza kupata. Tumesoma alama za nyakati na kuona sasa hivi muziki wao umezidi kuwa mgumu halafu nao wanataka masilahi mazuri. Wamekua sasa, kama wameweza kukaa kwa zaidi ya miaka mitatu kuna wakati nao wanataka kuonekana wakubwa. “Wao walipokuja, walikuja wakiwa mmojammoja (solo) tukaona tumchukue Aslay awatangaze wenziye kama kundi. Vilevile ukiangalia hata Raymond naye alikuwa Mkubwa na Wanawe, tukaona tumruhusu afanye kivyake sasa hivi kama unavyomuona. Sasa hivi muziki wa bendi unaonekana kabisa unapoelekea siyo, sasa siyo kulazimisha ilimradi waonekane ni bendi fulani wakati wanaweza kufanya solo.
“Mtu akihitaji kundi anaweza kuwachukua. Mtu anaweza kuja kuhitaji msanii mmoja afanye shoo na siyo kundi inakuwa rahisi,” anasema Fella. Kuhusiana na madai ya kuwanyima nyumba alizowaahidi, Fella anasema: “Unajua Watanzania wengi hawaamini watu wanaokaa muda mrefu wakifanya mmojammoja wanajua wamegombana. Mbona shoo ya Dodoma walikwenda? Kama wamegombana mbona walienda pamoja? “Hawajahamia kwa sababu hakujachangamka kama mjini ila pakichangamka watahamia. Mbona Chegge ana nyumba yake, nilimpa huku kwangu Kilungule kipindi kile na Nature lakini hajahamia hadi leo ina maana naye amedhulumiwa?

Stori zinazo husiana na ulizosoma

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

ALLY KAMWE AZIMIA KWA MKAPA.

RAIS SAMIA KUZINDUA MKUTANO MKUU WA 79 WA BARAZA LA MICHEZO YA MAJESHI DUNIANI

MIGINGO KISIWA KIDOGO ZAIDI AFRIKA KILICHOGOMBEWA NA UGANDA, KENYA