YANGA YAIPIGA PRISONS 2-0

 Wachezaji wa Yanga wakishangilia ushindi wa bao la pili dhidi ya Tanzania Prisons katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam leo. (PICHA NA KHAMISI MUSSA)
 Mchezaji wa Yanga, Geofrey Mwashiuya (kulia), akigombea mpira na Nurdin Chona katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam . Yanga ilishinda mabao 2-0.


Wanayanga wakishangilia ushindi. PICHA ZOTE NA KHAMISI MUSSA

Habari kwa hisani ya Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
YANGA SC imerudi kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Tanzania Prisons ya Mbeya jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Pongezi kwa Mrundi, Amissi Joselyn Tambwe aliyefunga bao la kwanza na kuseti la pili katika mchezo wa leo na sasa Yanga inafikisha pointi 59 baada ya kucheza mechi 26 na japo wanalingana kwa pointi na Simba iliyocheza mechi 27, lakini wanakwenda juu kwa wastani wao mzuri wa mabao. 

Katika mchezo huo uliochezeshwa na marefa, Suleiman Kinugani wa Morogoro aliyesaidiwa na Makame Mdogo wa Shinyanga na Gasper Kato wa Arusha, dakika 45 za kipindi cha kwanza zilikuwa ngumu kwa mabingwa watetezi, kutokana na wageni kucheza kwa kujihami zaidi.

Yanga walishindwa kabisa kuifungua ngome ya timu ya Jeshi la Magereza iliyoongozwa na Salum Kimenya, huku kikwazo zaidi kikiwa ni kipa Aaron Kalambo aliyeonyesha umahiri wa hali ya juu kwa kuokoa michomo mingi ya hatari.  

Na kipindi cha pili, Prisons walikianza vizuri pia wakiendelea kuwabana Yanga, kiasi cha mashabiki wa timu ya Jangwani kuanza kuhofia matokeo mabaya.

Hata hivyo, mambo yalibadilika baada ya mabadiliko yaliyofanywanna kocha Mzambia, George Lwandamina kuwaingiza beki Juma Abdul na kiungo Haruna Niyonzima kwenda kuchukua nafasi za beki Hassan Kessy na kiungo Said Juma ‘Makapu’ kipindi cha pili.

Yanga ikabadilisha mipango ya kuishambulia ngome ya Prisons na kuanza kucheza gonga safi za kuoana vizuri, badala ya mashambulizi ya kulazimisha.

Na ukawadia wakati wa zamani wa Vital’O ya Burundi na Simba ya Dar es Salaam, Amissi Joselyn Tambwe kuwainua vitini mashabiki wa Yanga kwa bao zuri la kichwa, akimalizia krosi maridhawa ya beki wa kulia, Juma Abdul Mnyamani dakika ya 70. 

Na kabla Prisons hawajaweka akili zao sawa, Tambwe akammiminia krosi nzuri kiungo mshambuliaji kutoka Zambia, Obrey Chirwa kuifungia Yanga bao la pili dakika ya 70.

Hadi hapo shughuli ikawa kama imeisha, na Prisons wakaanza kucheza kwa kujizuia kuruhusu mabao zaidi.

Kikosi cha Yanga kilikuwa; Benno Kakolanya, Hassan Kessy/Juma Abdul dk59, Mwinyi Mngwali, Kevin Yondan, Vincent Bossou, Said Juma ‘Makapu’/Haruna Niyonzima dk65, Simon Msuva, Thabani Kamusoko, Amissi Tambwe, Obrey Chirwa/Matheo Anthony dk81 na Geoffrey Mwashiuya.

Tanzania Prisons; Aaron Kalambo, Benjamin Asukile, Michael Ismail, James Mwasote, Nurdin Chona, Jumanne Elfadhil, Salum Kimenya, Mohammed Samatta/Nchinjay Kazungu dk86, Victor Hangaya/Kassim Hamisi dk63, Lambert Sibiyanka na Meshack Suleiman.


Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KINANA ASIMIKWA KUWA MMOJA WA MACHIFU WA WAPARE, SAME MAGHARIBI

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI