BIN KLEB: SIJAREJEA KWENYE UONGOZI WALA KAMATI YOYOTE YANGA


Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
KIONGOZI wa zamani wa Yanga, Abdallah Ahmed Bin Kleb amesema kwamba anaendelea kuisaidia klabu hiyo kama mpenzi na mwanachama, lakini hajarejea kwenye uongozi.
Baadhi ya vyombo vya Habari vimeripoti kwamba Bin Kleb amerejea kwenye Kamati ya Usajili ya klabu hiyo, lakini baada ya kuulizwa leo na Bin Zubeiry Sports – Online, Kleb alisema; “Hizo habari si kweli, tena ninashangaa wamezipata wapi, si kweli”.
Mjumbe huyo wa zamani wa Kamati ya Utendaji ya Yanga na aliyekuwa pia Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano amesema tangu ameondoka kwa kujiuzulu mwenyewe Yanga miaka miwili iliyopita hajawahi kurudi kwenye uongozi wala Kamati yoyote.
Abdallah Bin Kleb amesema hajarejea kwenye uongozi wala Kamati yoyote ya Yanga 

“Mimi nililazimika kuondoka Yanga kutokana na sababu ambazo zilikuwa nje ya uwezo wangu, na bahati mbaya mambo hayajabadilika, kwa hivyo siwezi kurejea kwenye uongozi. Lakini kama mpenzi na mwanachama, ninaendelea kuisaidia timu yangu,”amesema.
Pamoja na hayo, Bin Kleb amewahamasisha wapenzi wote na wanachama wa Yanga, wakiwemo viongozi wa zamani wa klabu kujenga utamaduni wa kuisaidia klabu hiyo, hususan inapokuwa katika wakati mgumu.
“Mimi ni Yanga damu, na ikiwa hii ni timu yangu wakati wowote bila kujali nipo kwenye uongozi au sipo, ninaisaidia, na ningependa wana Yanga wote tuwe na desturi hii, tusiitupe timu yetu, hiki ni kitu ambacho kinatupa furaha,”amesema.
Bin Kleb anakumbukwa kwa mchango wake mkubwa wa hali na mali alipokuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga kati ya mwaka 2011 na 2014, alipoiwezesha klabu kusajili wachezaji nyota walioiwezesha kushinda mataji mbalimbali na kutawala soka ya ukanda wa Afrika Mashariki.
Moja ya matukio ya kukumbukwa Bin Kleb aliwahi kufanya Yanga ni kumzidi kete aliyekuwa Mwenyekiti wa Simba, Alhaj Ismail Aden Rage katika usajili wa beki Mbuyu Twite kutoka APR ya Rwanda.
Twite alifanya kituko cha aina yake, baada ya kwanza kusaini Simba Julai 2012 mjini Kigali, Rwanda akiwa mchezaji wa APR, lakini siku chache baadaye akasaini na Yanga kama mchezaji wa St. Eloi Lupopo ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Rage alikwenda Kigali kumsajili Twite na kumpa dola za Kimarekani 30,000 na akafuata taratibu zote hadi kupewa uhamisho wake na Shirikisho la Soka Rwanda (FERWAFA), lakini baadaye, mchezaji huyo akasaini Yanga na ikaelezwa alikuwa anacheza kwa mkopo kutoka Lupopo ambao ndiyo walikuwa wana haki ya kumhamisha na si APR. 
Mwishowe usajili wa Twite kwenda Yanga kutoka Lupopo ndiyo ukapitishwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na si ule wa Simba kutoka APR. Hata hivyo, baadaye TFF iliamuru Yanga kurudisha gharama zote za Simba dola 32,000. 
Kwa ujumla, Yanga ilikuwa inasajili wachezaji wazuri zaidi wa ndani na nje ya nchi, wakati ambao Bin Kleb alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano. 

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI

KOCHA WA AL.AHLY ASEMA YANGA NI TIMU BORA NA NGUMU