JPM AIKATAA MIALIKO 60 YA KWENDA NJE YA NCHI

celina Mathew
RAIS John Magufuli jana alitumia siku yake ya kwanza ya ziara ya siku tatu mkoani Pwani kueleza sababu za kutopenda kusafiri nje ya nchi, akisema “kwanza nataka kusafisha nchi.”

 Huku akituma salamu kwa watu wanaofanya uvamizi na kuua watu katika wilaya za Rufiji na Kibiti mkoani humo kuwa sasa wameanza kushughulikiwa,

Rais alisema tangu alipoapishwa Novemba 5 mwaka juzi, amepata mialiko zaidi ya 60 lakini ameikataa. Kiongozi Mkuu huyo wa nchi alitoa kauli hiyo jana katika mkutano wa hadhara Bwawani wilayani Kibaha mkoani humo na kufafanua kuwa ikiwa atasafiri nje, viongozi atakaowaacha watabweteka.

 Tangu awe Rais, Dk Magufuli alisafiri nje ya nchi si zaidi ya mara tano, ikiwa ni tofauti na mtangulizi wake, Jakaya Kikwete ambaye mpaka anatimiza miaka miwili ya uongozi, alikuwa amesafiri nje ya nchi zaidi ya mara 30.

Huku akiapa kupambana na viongozi wachache wenye tamaa na rasilimali za nchi na kusababisha nchi kuwa masikini wakati ni tajiri, alisema: “Nimepewa mialiko mingi lakini sijahudhuria hata mmoja si kwamba sitaki au sipendi kusafiri, ninachofanya kwa sasa nasafisha kwanza hapa nchini. “Nikisema nisafiri watendaji watakaobaki watabweteka. Kumekuwa na changamoto nyingi zilizofanywa na vion
gozi wachache wa awamu zilizopita. Hawa walikuwa wakitumia rasilimali vibaya.” Alisema Tanzania haikupaswa kuwa masikini na kubainisha kuwa ni ya pili kwa vivutio duniani nyuma ya Brazil. “Zipo changamoto nyingi, lakini kubwa zimesababishwa na viongozi wachache wenye tamaa za hovyo na kusababisha wananchi kuendelea kuwa masikini, hivyo naahidi nitalala nao mbele na kupambana nao kwa nguvu zangu zote ili maisha yabadilike,” alisema. Alisema nchi ya Tanzania Mungu ameipa utajiri si umasikini, lakini jambo la kushangaza ni kuwa viongozi wachache wenye uchu wa madaraka wakautumia kwa kuuza Watanzania na kudhulumu haki zao jambo ambalo ni tatizo. “Watu wachache wamekosa uzalendo na huruma hata kwa wazazi wao waliowazaa, wapo wengine ni viongozi tuliwaamini wakawawakilishe, lakini wakaenda kuwakilisha wengine wenye maslahi yao binafsi,” alisema na kuongeza: “Naomba wananchi mniruhusu nilale nao mbele kwa mbele hadi mwisho ili rasilimali hizo zinazochezewa na wachache zirudi kwenye mikono yenu na kuwanufaisha.” Salamu kwa wauaji Katika hatua nyingine, Rais Magufuli alituma salamu kwa watu wanaojihusisha na mauaji ya viongozi wasio na hatia eneo la Kibiti na Rufiji kuwa hawatapita salama. Pia aliwataka wananchi wa Kibiti na Rufiji kuhakikisha wanatoa ushirikiano kwa vyombo vya ulinzi na usalama, ili watu wanaofanya matukio ya mauaji wanakamatwa kwa kuwa wanawajua. “Tumesikia, kwamba Rufiji na Kibiti hakuna viwanda, nani atakwenda kuwekeza wakati watu wanauawa hovyo, hivyo naomba tutambue tunaochelewesha naendeleo ni sisi wenyewe na wanaofanya vitendo hivyo mnawajua, lakini hamtaki kuwataja, tunaomba mtambue kuwa Serikali  hii si ya kuchezea, moto umeanza na wanauona,”alisema. Aliwataka kuacha tabia hiyo, kwa kuwa ni wachache hivyo watanyooka na watambue kuwa hawatapita hivyo hivyo kwa vitendo hivyo vya kihuni, hivyo kama wapo kwenye mkutano huo wapeleke salamu kwa wengine. “Naomba wanaofanya vitendo hivyo waache, maana ni wachache nawahakikishia watanyooka na kama wapo hapa wanasikiliza, wapelekeeni salamu huko waliko kuwa hawapiti, kwa kuwa vitendo hivyo havifai katika jamii na wanachelewesha maendeleo,” alisema. Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo alisema hali ya ulinzi na usalama katika mkoa huo ni shwari licha ya vitendo vichache vya kihalifu  vinavyofanyiwa kazi. Alisema licha ya hayo kuwepo, viwanda zaidi ya 370 kuna changamoto ambazo ni pamoja na kukosekana nishati ya umeme wa uhakika ambapo kwa sasa kuna megawati 20 wakati mahitaji ni 60 hivyo kuna upungufu wa megawati 20, nishati ya gesi, maji ya uhakika na barabara.

Comments

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MAKABILA 10 YENYE WANAWAKE WAREMBO TANZANIA

HAKUNA BINADAMU ALIYESALIMIKA NA UPOFU HUU...

SERIKALI KUWACHUKULIA HATUA WATANZANIA WATAKAOVAA JEZI ZA MAMELODI AU AL AHLY

CHATANDA AFUNGUA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO MADIWANI WANAWAKE WA MIKOA 11

KOCHA BENCHIKHA AMESEPA

MASHUSHUSHU WA MAMELODI WALIKUJA KUTUPELELEZA: HERSI

KOCHA WA AL.AHLY ASEMA YANGA NI TIMU BORA NA NGUMU