KUHUSU ACT-WAZALENDO NA ANNA MGHWIRA


Kwa siasa za kistaarabu. Siasa za ujenzi wa jamii na nchi moja kama ambavyo mataifa makubwa yaliyopevuka kidemokrasia hufanya, uteuzi wa Anna Mghwira, Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro ni jambo jema. Tena anapaswa kuungwa mkono na chama chake.
Kwa siasa za ulimwengu wa kwanza, palipo na wanasiasa wenye kutambua maana ya kuwa wanasiasa, uteuzi wa Anna Mghwira, ungeweza kuwa thamani kubwa kwa ACT-Wazalendo, maana inaonekana chama hicho kina viongozi wazuri, kiasi kwamba Rais anavutiwa nao na kuwapa kazi kubwa ili ashirikiane nao kujenga nchi na kutimiza maono yake ya kiuongozi.
Kwa siasa za Afrika, hasa Tanzania. Kwa siasa za CCM ya sasa chini ya Mwenyekiti, Dk John Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, uteuzi wa Anna Mghwira kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro una athari kubwa kwenye chama.
ACT-Wazalendo wasije kujidanganya kuwa watakuwa sahihi kwa Mghwira kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, huku akiendelea kuwa Mwenyekiti wa chama chao, wakifanya hivyo watakuwa wamejidanganya mno.
Siasa zinataka watu na watu ndiyo hufanya chama kiaminike. Hata hivyo, ili chama kipate watu lazima kijidhihirishe dira yake na kiwe chenye kutafsirika. Chama kikiwa kinatupiwa madongo kuwa ni tawi la Chama Tawala na siyo upinzani, inatakiwa madongo hayo yakose mashiko.
Mathalan, wakati ACT inaasisiwa, ilielezwa kuwa chama hicho kimeundwa kwa mkono wa Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa, kwamba akinyimwa nafasi ya kugombea Urais kupitia CCM, angejiunga ACT.
Lowassa alipokatwa jina lake kuelekea uteuzi wa mgombea Urais wa CCM mwaka 2015, moja kwa moja alijiunga na Chadema. Hivyo, kila mmoja alijionea kuwa ACT ilikuwa inasingiziwa kuhusu Lowassa.
Ikiwa chama kinasingiziwa kuwa chenyewe ni tawi la CCM, halafu Rais atokanaye na CCM akawa anateua wasaidizi wake kwenye chama hicho kinachosemwa ni tawi la CCM, hata kama nia ni njema, moja kwa moja athari yake ni kubwa kwenye chama. Maana watu watathibitisha yenye kusemwa hata kama ukweli haupo hivyo.
Hivyo, ACT wanatakiwa kuamua haraka kumwondoa Mghwira kwenye nafasi yake ya uongozi. Kama yeye mwenyewe ataamua kubaki kuwa mwanachama wa kawaida sawa, siyo kuwa kiongozi.
Misimamo ya Rais Magufuli kwa wapinzani inaeleweka. Sasa kwa nini aoneshe mapenzi makubwa kwa ACT kipindi hiki?
Mwaka jana, kada wa ACT, aliyegombea ubunge jimbo la Malinyi mwaka 2015, Hidaya Usanga, alikataliwa kupewa Ukurugenzi wa Halmashauri, baada ya Rais Magufuli kubaini Hidaya ni mwana ACT.
Mwaka huu, Rais Magufuli anateua vichwa vya juu kabisa vya ACT na kuvipa nafasi kwenye Serikali anayoiongoza. Ni hapo ndipo kwenye swali; Ni mapenzi kweli?
RAIS MAGUFULI ANAJUA SIASA
Kiongozi wa ACT, Zitto Kabwe amekuwa kwenye vipindi vya maelewano na wapinzani wenzake, hususan Chadema. Uhusiano mzuri wa Zitto na Chadema, hauwezi kumfurahisha Rais Magufuli.
Zitto amekuwa mstari wa mbele kukosoa sera za Rais Magufuli kwenye masuala mbalimbali katika uongozi wake. Anakosoa sera za Rais Magufuli kuhusu madini, uchumi, udhibiti wa mfumuko wa bei, jinsi ya kukabiliana na majanga ya kitaifa, utawala bora na kadhalika.
Anayoyafanya Zitto siyo matamu kwa Rais Magufuli. Ongezea historia kuwa Rais Magufuli alikuwa na misuguano na Zitto tangu alipokuwa Waziri wa Ujenzi.
Kwa kutafsiri hivyo, unapata jawabu kuwa Rais Magufuli hawezi kuwa na mapenzi makubwa na ACT ya Zitto kiasi kwamba wawe wanapeana viongozi kwa ajili ya nchi, badala yake unagundua kuwa uteuzi wa Rais Magufuli ndani ya ACT ni wa kimkakati zaidi.
Rais Magufuli anajua siasa. Anafahamu hali halisi ya ACT mbele ya macho ya vyama vikubwa vya upinzani chini, hasa Chadema.
Rais Magufuli anafahamu kuwa ili ACT izidi kutoaminiwa na wapinzani wengine ni lazima ionekane inakumbatiwa na Serikali. Hiki ndicho ambacho Rais Magufuli anakifanya kwa sasa.
Rais Magufuli anafahamu kuwa ili kumdhoofisha Zitto kisha hoja zake ziwe zinakosa nguvu na kuishia kupepesuka kwenye masikio ya Watanzania, ni lazima kuifanya ACT iwe inafanana hasa na tawi la CCM. Ndiyo maana anateua tu.
Rais Magufuli anafahamu kuwa ili Chadema na Zitto waache kukumbatiana na kuongeza hali ya kutoaminiana kati yao ni lazima kuitumia ACT ya Zitto kuwafanya Chadema wamuone Zitto ni kiongozi wa upinzani asiyeeleweka.
Katika hili la uteuzi wa Mghwira, Chadema na wapinzani wengine, badala ya kutumia muda wao kuizodoa ACT kuwa ni tawi la CCM, wanatakiwa kujielekeza kutambua siasa ambazo Rais Magufuli anazicheza.
Ni kwamba Rais Magufuli ameamua kutumia sayansi kuwafanya wapinzani wasiaminiane. Ameamua kutengeneza nafasi kubwa kati ya ACT na Chadema. Panapo majaliwa 2020, wapinzani watashtuka na kujikuta walichelewa mno kusoma mchezo.
Uteuzi wa Prof Kitila Mkumbo kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, ulitafsirika tofauti, kwani ilionekana angeishia hapo. Kumtwaa na Mwenyekiti wa chama, hapo kuna shaka kubwa.
NGOJA NIKWAMBIE
Rais Magufuli hana mapenzi na ACT. Huwezi kukipenda chama halafu ukawa unaondoa mihimili yake. Huwezi kupenda nyumba kisha ukawa unabomoa nguzo zake.
Kama Rais Magufuli angekuwa na mapenzi makubwa na ACT, angekuwa anakiwezesha chama hicho kikue ili kiwe chama cha upinzani chenye nguvu halafu kije kikitetemeshe Chadema kisha ukiwadia uchaguzi, kisababishe mchuano wa wapinzani kwa wapinzani. Siyo kukipukutisha.
Anachokifanya Rais Magufuli kwa sasa ni kukielekeza ACT panapovuma upepo mbaya wa kisiasa. Zitto na viongozi wenzake waliobaki wanatakiwa kutumia akili ya juu kulibaini hilo na kulikabili.
Kama mwendo wa ACT utakuwa hivi mpaka 2020, maana yake Rais Magufuli atakuwa amefanikiwa kuhakikisha Chadema ndiyo chama pekee cha upinzani kinachosimama naye kwenye uchaguzi. Wakati huo Chadema ndiyo hao mwenyekiti wao katengenezewa sauti ya mahaba na mrembo Wema Sepetu.
ACT wanatakiwa kupigania uhai na ustawi wao, wasikubali kuchezewa akili. Ni vigumu kumzuia mtu anayeteuliwa na Rais kushika wadhifa fulani. Hata hivyo ni wajibu wa chama kujipangusa madoa na kuenenda kulingana na mazingira ya siasa za Tanzania.
ACT ipo Tanzania na inafanya siasa zake Tanzania, kwa hiyo lazima ijiendeshe kulingana na upepo wa siasa za Watanzania. Kwa maana hiyo, ili kiaminike zaidi kinatakiwa kijitenge na kashfa ya kutumiwa na CCM. Lazima chama kimwache Mghwira akafanye kazi yake halafu kipate mwenyekiti mwingine.
Ndimi Luqman MALOTO
LikeShow more reactions
Comment
0

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

HIVI NDIVYO BIASHARA YA NGONO NAMNA INAVYOTIKISA MOROGORO: SEHEMU YA PILI.

DC MJEMA AONJA ADHA YA MAFURIKO AKIKAGUA ATHARI ZA MAFURIKO ILALA

ZAKIA MEGHJI AWATIA HAMASA GIRL GUIDES, ATAKA WAWE JASIRI

DC MKURANGA AZINDUA MRADI WA MASHAMBA MJI YA NAMAINGO MSOLWA

TGGA WAMUAGA BOSS WA GIRL GUIDES AFRIKA KWA HAFLA KABAMBE

IJUE HISTORIA YA UHASIMU WA KOREA KASKAZINI NA MAREKANI

WAPENZI WANASANA WAKIFANYA MAPENZI GESTI

ANGALIA PICHA NDEGE KUBWA YA ABIRIA DUNIANI ILIYOANZA SAFARI NDEFU ZAIDI!

Wasafi TV kuanza kurusha matangazo yake leo (+video)