Megawati 5000 kupatikana 2021, Ni baada ya kukamilika kwa mradi wa Stieglers Gorge


Naibu Waziri wa Nishati na Madini Dk. Medard Kalemani ( wa pili kulia mbele) akimwongoza Waziri wa Maji, Nishati na Umwagiliaji kutoka Ethiopia, Dk. Seleshi Bekele (katikati mbele) kwenye ziara ya kukagua eneo la ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia nguvu za maji la Stiegler’s Gorge, Rufiji mkoani Pwani katika ziara hiyo.
Na Greyson Mwase, Rufiji.

Naibu Waziri wa Nishati na Madini Dk. Medard Kalemani amesema Tanzania inatarajia kupata umeme wa uhakika wa Megawati 5000 ifikapo mwaka 2021, mara baada ya kukamilika kwa mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia  nguvu za maji katika maporomoko ya maji ya Mto Rufiji kwenye  eneo la Stiegler’s Gorge  lililopo  Rufiji mkoani Pwani ambao utaongeza umeme wa kiasi cha Megawati 2100 katika  gridi ya taifa.

Dk. Kalemani aliyasema hayo jana tarehe 29 Juni, 2017 katika ziara ya Waziri wa Maji, Nishati na Umwagiliaji kutoka  Ethiopia, Dk. Seleshi Bekele aliyeambatana na wataalam wa masuala ya ujenzi wa mitambo  ya kuzalisha umeme kwa kutumia maji kutoka  Ethiopia kwenye eneo  la mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia maporomoko ya maji ya Mto Rufiji ya Stieglers Gorge wilyani  Rufiji mkoani Pwani.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini Dk. Medard Kalemani akishuka kwenye boti kwa ajili ya kuelekea kwenye eneo la Stieglers Gorge kutakapojengwa mradi huo.

Wengine walioshiriki katika ziara hiyo ni pamoja na wataalam wa masuala ya  umeme na ujenzi wa mabwawa kutoka Tanzania,  Shirika la Umeme  Tanzania (TANESCO) na Wizara ya Nishati na Madini.  Ziara  hiyo inafuatia maombi ya  Rais John Magufuli kwa Waziri Mkuu wa Ethiopia ya kutuma wataalam wa masuala ya ujenzi wa mitambo ya kuzalisha umeme kwa kutumia nguvu za maji kwa ajili ya kubadilishana uzoefu na  wataalam wa masuala ya umeme na ujenzi wa mabwawa kutoka Tanzania.

Dk Kalemani alisema kuwa kupatikana kwa umeme wa uhakika ifikapo mwaka 2021 kutachochea ongezeko la viwanda hivyo kuongezeka kwa fursa za ajira na biashara na kukuza uchumi wa nchi.
Alisema mradi huo mkubwa ni moja ya mikakati ya Serikali  kuhakikisha nishati inakuwa na mchango mkubwa katika  kufikia malengo  ya  Dira ya Maendeleo ya Taifa yenye lengo la kuhakikisha kuwa nchi inatoka katika orodha ya nchi maskini duniani na kuingia katika orodha ya nchi zenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Waziri wa Maji, Nishati na Umwagiliaji kutoka Ethiopia, Dk. Seleshi Bekele (kushoto) akieleza jambo kwa Mhaidrolojia Mwandamizi kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Stanislaus Kizzy (kulia) katika ziara hiyo. Anayesikiliza katikati ni Naibu Waziri wa Nishati na Madini Dk. Medard Kalemani.

Alisisitiza kuwa mbali na mradi huo mkubwa, serikali imeweka mikakati ya kutumia vyanzo vingine vya nishati kama vile Gesi, Makaa ya Mawe, Jotoardhi, Upepo ili kuhakikisha kuwa nchi inapata umeme wa uhakika. Akielezea mafanikio ya mradi huo mbali na upatikanaji wa umeme wa uhakika, Dk. Kalemani alisema kuwa mradi huo utachochea ukuaji wa shughuli za uvuvi katika mkoa wa Pwani.

Alitaja mafanikio mengine kuwa ni pamoja na kukuza sekta ya Utalii katika  mkoa wa Pwani pamoja na kuzuia mafuriko ambayo yamekuwa yakitokea mara kwa mara katika mto Rufiji na kuathiri makazi  ya wakazi waishio pembezoni na mto huo. Akielezea hatua iliyofikiwa ya maandalizi ya ujenzi wa mradi huo mkubwa, Dk. Kalemani alisema baada ya timu ya wataalam kutoka Tanzania na Ethiopia kufanya ziara katika eneo la mradi hatua inayofuatia ni wataalam kukaa vikao mbalimbali kujadili namna bora ya kutekeleza mradi pamoja na kubadilishana uzoefu.
Mhaidrolojia Mwandamizi kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Stanislaus Kizzy (kulia) akifafanua jambo kwa Waziri wa Maji, Nishati na Umwagiliaji kutoka Ethiopia, Dk. Seleshi Bekele ( wa pili kushoto). Katikati ni Naibu Waziri wa Nishati na Madini Dk. Medard Kalemani.

Alisema mara baada ya ujenzi wa mradi huo kukamilika, moja ya kazi zitakazofanywa ni pamoja na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme hadi Chalinze yenye urefu wa kilomita 200 na njia ya kusafirisha umeme kutoka  eneo la Mradi hadi  Singida yenye urefu wa kilometa 800.

Waziri Kalemani aliwataka wananchi na taasisi mbalimbali kuunga mkono  juhudi za Serikali  ya Awamu ya Tano  ikiwa ni pamoja na kulinda vyanzo vya maji  hususan katika mto Rufiji.
Wakati huohuo, katika  ziara hiyo Waziri wa Maji, Nishati na Umwagiliaji kutoka  Ethiopia, Dk. Seleshi Bekele alisema kuwa mradi huu mkubwa ni mzuri na unatekelezeka na kuongeza kuwa  Ethiopia ipo tayari kutoa ushirikiano mkubwa kupitia wataalam wake lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa mradi unafanikiwa na kukamilika kwa wakati.
Kaimu Kamishna wa Nishati na Masuala ya Petroli, Mhandisi Innocent Luoga (kulia) akipokewa na Meneja Mkuu wa Hoteli ya Serena Mivumo River Lodge, Ellieta Mbisse (kushoto) mara bada ya kuwasili katika uwanja mdogo wa Stiegler’s Gorge, Rufiji mkoani Pwani kabla ya kuanza kwa ziara ya Waziri wa Maji, Nishati na Umwagiliaji kutoka Ethiopia, Dk. Seleshi Bekele aliyeambatana na wataalam wa masuala ya ujenzi wa mitambo ya kuzalisha umeme kwa kutumia maji kutoka Ethiopia pamoja na wataalam wa masuala ya umeme na ujenzi wa mabwawa kutoka Tanzania wakiongozwa na mwenyeji wao Naibu Waziri wa Nishati na Madini Dk. Medard Kalemani.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini Dk. Medard Kalemani akishuka kwenye helikopta, mara bada ya kuwasili katika uwanja mdogo wa Stieglers Gorge, Rufiji mkoani Pwani kabla ya kuanza kwa ziara ya Waziri wa Maji, Nishati na Umwagiliaji kutoka Ethiopia, Dk. Seleshi Bekele aliyeambatana na wataalam wa masuala ya ujenzi wa mitambo ya kuzalisha umeme kwa kutumia maji kutoka Ethiopia pamoja na wataalam wa masuala ya umeme na ujenzi wa mabwawa kutoka Tanzania.
Kaimu Kamishna wa Nishati na Masuala ya Petroli, Mhandisi Innocent Luoga (kushoto) akielezea maandalizi ya mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia nguvu za maji wa Stieglers Gorge kwa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Ethiopian Construction Design and Supervision kutoka Ethiopia, Dk. Negede Kassa (kulia) katika ziara hiyo.
Kipimo cha kupimia kina cha maji (water gauge) katika sehemu ya mto Rufiji uliopo katika wilaya ya Rufiji mkoani Pwani.
Waziri wa Maji, Nishati na Umwagiliaji kutoka Ethiopia, Dk. Sileshi Bekele ( wa tatu kushoto) akieleza jambo katika ziara hiyo.
Sehemu ya Mto Rufiji kutakapojengwa mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia nguvu za maji katika eneo la Stieglers Gorge wilayani Rufiji mkoani Pwani.
Waziri wa Maji, Nishati na Umwagiliaji kutoka Ethiopia, Dk. Seleshi Bekele (wa saba kulia) na Naibu Waziri wa Nishati na Madini Dk. Medard Kalemani (wa nane kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na timu ya wataalam kutoka Tanzania na Ethiopia katika ziara hiyo.
0

HABARI ZILIZOSOMWA ZAIDI

MATOKEO YA KIDATO CHA PILI, DARASA LA SABA YATANGAZWA ZANZIBAR

HIVI NDIVYO BIASHARA YA NGONO NAMNA INAVYOTIKISA MOROGORO: SEHEMU YA PILI.

ZAIDI YA WANANCHI 500 KUSHIRIKI MAFUNZO YA MKIKITA YA KILIMO CHA PAPAI SALAMA

MKIKITA YATOA OFA KWA KILA HEKA YA PAPAI SH. MIL. 2 KUTANDAZA MIUNDOMBINU YA UMWAGILIAJI

DIAMOND AITWA NA NYOTA YAJAA GOMS

WATEJA WA NSSF DAR WATIMULIWA KWA MTUTU WA BUNDUKI

MATOKEO YA DARASA LA SABA YATANGAZWA

KAMISHNA MARIJANI AZINDUA CHAMA CHA WAFUGAJI MBWA TANZANIA (TCA)